Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe 29 Juni 2026 amemwandikia ujumbe Mheshimiwa Padre Davide Pagliarani, Mkuu wa Jumuiya ya Mapadre wa Mtakatifu Pio X : Majadiliano Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe 29 Juni 2026 amemwandikia ujumbe Mheshimiwa Padre Davide Pagliarani, Mkuu wa Jumuiya ya Mapadre wa Mtakatifu Pio X : Majadiliano  (@Vatican Media)

Barua ya Papa Leo XIV kwa Jumuiya ya Mapadre wa Mtakatifu Pio X: Umoja wa Kanisa

Papa Leo XIV akiwa amefungwa na upendo wa Kikristo, anasali na kuwaomba kwa moyo wake wote, kurejea katika mapito yao! Waangalie kwa umakini mafao ya kiroho kwa ajili ya waamini kwa sababu utengano na Kanisa, utakuwa ni kuzuizi cha waamini wao kupokea kwa halali Sakramenti za Kanisa, wanazopenda kupokea kama njia ya kujitakatifuza. Mama Kanisa yuko tayari kuanza mchakato wa majadiliano yanayowezeshwa na kufanikishwa na Roho Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema Kanisa ni Sakramenti ya wokovu na ni chombo cha upatanisho, umoja na mshikamano wa Kitaifa na Kimataifa. Jumuiya ya Mapadre wa Mtakatifu Pio X (kwa Kilatini: Fraternitas Sacerdotalis Sancti Pii X - FSSPX), “The Priestly Society of Saint Pius X (SSPX)” ilianzishwa na Askofu Marcel Lefebvre kunako mwaka 1970. Jumuiya hii inajulikana kwa kusimamia Mapokeo ya Kikatoliki, kuheshimu Ibada Misa Takatifu katika lugha ya Kilatini, na kukataa mabadiliko yaliyoletwa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Kumekuwepo na juhudi za makusudi za kutaka kuirudisha Jumuiya ya Mapadre wa Mtakatifu Pio X katika ushirika kamili na Kanisa Katoliki, tangu wakati wa uongozi wa Baba Mtakatifu Benedikto XVI, hadi wakati huu wa uongozi wa Baba Mtakatifu Leo XIV, juhudi zote hizi bado zinagonga mwamba na kwamba, Jumuiya imetanga mpango mkakati wa kuwaweka wakfu mapadre wanne kuwa Maaskofu, tarehe 1 Julai 2026 bila idhini ya Khalifa wa Mtakatifu Petro ambaye kwa wakati huu yuko katika nafsi ya Baba Mtakatifu Leo XIV huko Écône, nchini Uswissi. Kitendo hiki kitapelekea Jumuiya hii kujitenga moja kwa moja na Kanisa Katoliki na hivyo kuzidisha kinzani na mivutano ya miaka mingi isiyokuwa ya lazima.

SSPX kutoa Daraja Takatifu ya Upadre bila kibali cha Papa ni batili
SSPX kutoa Daraja Takatifu ya Upadre bila kibali cha Papa ni batili   (@Vatican Media)

Ni katika jitihada hizi, Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe 29 Juni 2026 amemwandikia ujumbe Mheshimiwa Padre Davide Pagliarani, Mkuu wa Jumuiya ya Mapadre wa Mtakatifu Pio X na kwa njia yake, Maaskofu, Mapadre, Majandokasisi na waamini walei wanaovutwa kufuata mtindo wa maisha ya Jumuiya hii. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, anamwadikia ujumbe huu, akifahamu fika dhamana na wajibu wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mama Kanisa anatambua na kuthamini maisha ya kiliturujia, malezi na majiundo ya Mapadre, ari na mwamko wa shughuli za kichungaji pamoja na shauku ya kutaka kuendelea kuwa waaminifu kwa Mapokeo ya Kanisa, hali inayohitaji uelewa mpana, jambo ambalo watangulizi wake walilipatia kipaumbele cha pekee.

Papa Leo XIV anawasihi wana wa Pio 10 kuachana na mpango wao
Papa Leo XIV anawasihi wana wa Pio 10 kuachana na mpango wao   (@VATICAN MEDIA)

Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa amefungwa na upendo wa Kikristo, anasali na kuwaomba kwa moyo wake wote, kurejea katika mapito yao! Waangalie kwa umakini mkubwa mafao ya kiroho kwa ajili ya waamini kwa sababu utengano na Kanisa, utakuwa ni kuzuizi cha waamini wao kupokea kwa halali Sakramenti za Kanisa, wanazopenda kupokea kama njia ya kujitakatifuza. Mama Kanisa yuko tayari kuanza mchakato wa majadiliano ya kina yanayowezeshwa na kufanikishwa na Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasali na kuwaomba kwamba, “wasichane nguo ya Kristo Yesu” kwani hii ni dhambi nzito. Kristo Yesu apende kuziangazia dhamiri zenu, aamshe nyoyo zenu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema kwa uchungu mkubwa kwamba, kwa mamlaka aliyopewa na Kristo Yesu, na kwa moyo uliosheheni machungu, lakini bado akiwa na matumaini anahisi ndani mwake, kuwaomba kuachana na nia ya kuwawekwa wakfu Maaskofu wapya; anaweka nia zote hizi chini ya Moyo Safi wa Bikira Maria, Mama wa Shauri Jema.

Papa Leo Umoja Kanisa

 

30 Juni 2026, 15:20