Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 12 Juni 2026 anafanya Hija ya 4 ya Kitume nchini Hispania kwa kunogeshwa na kauli mbiu: "Alzad la mirada" Yaani "Inua macho yako.” Yn 4:35. Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 12 Juni 2026 anafanya Hija ya 4 ya Kitume nchini Hispania kwa kunogeshwa na kauli mbiu: "Alzad la mirada" Yaani "Inua macho yako.” Yn 4:35.   (ANSA)

Hija ya 4 ya Kitume ya Papa Leo XIV Hispania: Ratiba Elekezi

Papa Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 12 Juni 2026 anafanya Hija ya 4 ya Kitume nchini Hispania kwa kunogeshwa na kauli mbiu: "Alzad la mirada" Yaani "Inua macho yako.” Yn 4:35. Baba Mtakatifu anatembelea mji mkuu wa Madrid ambako atapata nafasi ya kuzungumza na viongozi wa Serikali, vyama vya kiraia pamoja na wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi zao huko Hispania na Dominika kuadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 12 Juni 2026 anafanya Hija ya 4 ya Kitume nchini Hispania kwa kunogeshwa na kauli mbiu: "Alzad la mirada" Yaani "Inua macho yako.” Yn 4:35. Baba Mtakatifu anatembelea mji mkuu wa Madrid ambako atapata nafasi ya kuzungumza na viongozi wa Serikali, vyama vya kiraia pamoja na wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi zao huko Hispania. Jioni atatembelea Kituo cha “Cedia 24 Horas Social Project” kinachoendeshwa na kusimamiwa na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Hispania, Caritas. Hii ni sehemu muhimu sana ya huduma za kijamii zinazotolewa na Kanisa nchini Hispania. Ni mahali pa watu kupata ushauri nasaha, msaada wa kisaikolojia na kwamba, hapa maskini wa Jiji na Madrid wanaweza kupata huduma msingi, ili kukuza na kudumisha utu, heshima na haki zao msingi. Kanisa linajengwa na waamini wanaosimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo, kama kielelezo makini cha imani tendaji na sehemu muhimu ya kuyatakatifuza malimwengu kwa chachu ya Injili.Adui mkubwa wa Kanisa aliwahi kusema, Papa Francisko kwamba ni pale uchu wa mali na madaraka vinapoingia kwa kupitia mlango wa nyuma. Maskini ni hazina, amana na utajiri wa Kanisa, hawa ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu.

Viongozi kutoka Hispania wakizungumza na Kardinali Pietro Parolin
Viongozi kutoka Hispania wakizungumza na Kardinali Pietro Parolin   (@Vatican Media)

Matendo ya huruma ndicho kigezo kikuu ambacho Kristo Yesu atakitumia Siku ya Hukumu ya Mwisho. Waamini wawe makini dhidi ya uchu wa mali na madaraka, mambo ambayo yanaweza kuhatarisha hata maisha yao ya kiroho na kujikuta wametumbukia katika kiburi, ubinafsi na hatimaye kumezwa na malimwengu. Lakini, ikumbukwe kwamba, haya ni mapambano endelevu katika maisha ya kiroho! Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV katika hija hii ni kwamba, maskini na watu dhaifu ndani ya jamii wanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika sera na mikakati ya kijamii na kikanisa. Vijana wanapaswa kushirikishwa katika mchakato wa kujadili, kuamua na kutekeleza mambo msingi katika maisha yao, kwa kuwajengea uwezo wa uongozi, ili kuchangia: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika ngazi mbali mbali. Wapewe malezi ya kutosha, ili hatimaye, kwa njia ya mifano bora ya maisha, waweze kuchangia karama, vipaji na taaluma yao kwa ajili ya ustawi wa wengi. Vijana wanataka kuwa kweli ni wamisionari wenye furaha wanaotaka kushiriki katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa kwa ari na moyo mkuu; kwa kushirikiana na wazee katika maisha na utume wa Kanisa.

Mkesha wa Sala Kati ya Papa Leo XIV na Vijana wa Hispania
Mkesha wa Sala Kati ya Papa Leo XIV na Vijana wa Hispania   (@Vatican Media)

Vijana wanataka kushiriki katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu, lakini wanapaswa kuwezeshwa kielimu na kiuchumi. Kanisa lithubutu kuwatafuta na kuwafuata vijana kwenye mitandao ya kijamii, ili kusaidia mchakato wa maboresho ya kijamii na kiutu, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi! Sera na mikakati mbalimbali inapaswa kuendelezwa ili kuwawezesha vijana kujenga uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao. Kwanza kabisa watambue umuhimu wa Sakramenti za Kanisa, maisha ya sala, ushiriki mkamilifu wa liturujia na kwamba, wanapaswa kuwa ni mashuhuda na walinzi wa imani katika ulimwengu mamboleo unaogubishwa na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Vijana waandaliwe vyema ili kushiriki katika Sakramenti za Kanisa, hususan: Sakramenti ya Ndoa kwa kutambua maana, umuhimu, changamoto, uzuri na utakatifu wake. Sakramenti ya Upatanisho, iwaonjeshe vijana huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao. Matukio mbalimbali yawasaidie vijana kukuza imani, matumaini, mapendo na mshikamano wao wa udugu wa kibinadamu. Mwelekeo wa maisha na utume wa Kanisa katika masuala ya kijamii na maisha ya kiroho, yasaidie mchakato wa uinjilishaji mpya miongoni mwa vijana dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya; kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kushikamana dhidi ya biashara ya binadamu na utumwa mamboleo pamoja na uhamiaji wa shuruti!

Papa Leo XIV anaadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu
Papa Leo XIV anaadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi usiku tarehe 6 Juni 2026 anafanya mkesha na vijana wa kizazi kipya kutoka Hispania, kama sehemu ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe ya Mwili na Damu ya Kristo, yaani Ekaristi Takatifu: “Corpus Domini” au “Corpus Christi” kwa lugha ya Kilatini inayoadhimishwa Dominika tarehe 7 Juni 2026. Hii ni fursa makini kwa waamini kutangaza na kushuhudia imani ya Kanisa kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, yaani uwamo wa Kristo katika maumbo ya Mkate na Divai. Mababa wa Kanisa wanathibitisha kwamba, kwa nguvu ya imani ya Kanisa na uwezo wa Neno la Kristo Yesu, na tendo la Roho Mtakatifu, kwamba, mageuzo ya Mkate na Divai yanakuwa ni Mwili na Damu Azizi ya Kristo. Huu ni mwaliko kwa waamini kupyaisha imani yao katika Fumbo hili kuu la Ekaristi Takatifu, kwa kuunganisha sauti za nyimbo kama kielelezo cha moyo wa shukrani, kwa uwepo angavu wa Kristo Yesu katika Kanisa lake. Ni wito kwa waamini kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi, kwani Mwenyezi Mungu kwa wingi wa baraka na neema zake ni Mhusika mkuu, lakini anategemea pia ushiriki wa waamini katika kuganga na kuponya magonjwa ya waamini kiroho na kimwili. Kristo Yesu ni daktari wa roho na mwili! Baba Mtakatifu Leo XIV amesema, Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu ni fursa ya kuzama zaidi katika imani katika Fumbo la Ekaristi Takatifu na hivyo kuendelea kupyaisha upendo kwa Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Dominika tarehe 7 Juni 2026 Baba Mtakatifu Leo XIV atakutana na kuzungumza kwa faragha na Wanashirika la Mtakatifu Augustino wanaofanya utume wao nchini Hispania. Na baadaye jioni na washiriki wa mkutano wa ujenzi wa mtandao wa kijamii katika ulimwengu wa utamaduni, sanaa, uchumi na michezo.

Diplomasia ya Vatican inakita mizizi yake katika utu, heshima na haki msingi
Diplomasia ya Vatican inakita mizizi yake katika utu, heshima na haki msingi   (AFP or licensors)

Jumatatu tarehe 8 Juni 2026 Baba Mtakatifu Leo XIV atakutana na Waziri mkuu wa Hispania na kuhutubia Bunge la Hispania, jioni atashiriki katika Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Almudena “Santa María de la Almudena” ni Mlinzi na Mwombezi wa Jimbo kuu la Madrid, Hispania na kila mwaka ifikapo tarehe 9 Novemba, anakumbukwa na Mama Kanisa nchini Hispania. Baadaye usiku, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na Jumuiya ya Jimbo kuu la Madrid, Hispania. Jumanne, tarehe 9 Juni 2026, akiwa mjini Barcelona, Baba Mtakatifu ataongea na watu wa kujitolea na kusali Sala ya Malaika wa Bwana na jioni atashiriki katika mkesha wa Sala. Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa Jimbo kuu la Barcelona tarehe 10 Juni 2026 atapata fursa ya kukutana na wafungwa wa Gereza la “Brians wa Kwanza.” Itakumbukwa kwamba, huduma kwa wafungwa ni sehemu ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu ndilo ambalo limekabidhiwa dhamana ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya wafungwa magerezani, ili kuonesha wasiwasi na ukaribu wa Mama Kanisa kwa wafungwa wanaoteseka magerezani. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ni dhamana na wajibu wa Kanisa zima kama sehemu ya utekelezaji wa utume wake unaomwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha ya watu. Wakati wa hukumu ya mwisho, watu watahukumiwa kadiri walivyowatendea ndugu zake walio wadogo, na kwa kufanya vile, walimtendea Kristo Yesu mwenyewe. (Rej. Mt. 25:40) Kristo Yesu anajitambulisha kuwa kati ya watu wenye njaa, kiu, wageni, watu walio uchi, wagonjwa na wale walioko kifungoni. Baba Mtakatifu atasali Rozari Takatifu, atakutana na kuzungumza na wafanyakazi katika vyama na mashirika ya huduma nchini Hispania na jioni ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya watu wa Mungu Jimbo kuu la Barcelona.

Kanisa Kuu la Sagrada Familia, Jimbo kuu la Barcelona, Hispania
Kanisa Kuu la Sagrada Familia, Jimbo kuu la Barcelona, Hispania

Baba Mtakatifu Leo XIV, Alhamisi tarehe 11 Juni 2026 atatembelea Kisiwa cha “Las Palmas De Gran Canaria.” Hii ni nafasi kwa Papa Leo XIV kukutana na kuzungumza na Mashirika yanayowahudumia wakimbizi na wahamiaji. Sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha! Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto ya Kimataifa. Kuna Biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo ambayo ni saratani ya kijamii na uhalifu mkubwa unaosigina: utu, heshima na haki msingi za binadamu; mambo ambayo wakati mwingine yanafumbiwa macho na jamii. Wahusika wakuu anasema Baba Mtakatifu Leo XIV ni vijana wanaotafuta fursa, lakini Serikali mbalimbali kwa kukazia utawala wa sheria zinaweza kudhibiti wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, kwani wakati mwingine watu hawa wanapokuwa vizuizini wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kuliko hata kule walikotoka. Je, nini kinaweza kufanyika ili kudhibiti wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia? Anauliza Baba Mtakatifu Leo XIV. Mchana Baba Mtakatifu atakutana na Makleri, Watawa na Majandokasisi na baadaye jioni ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.

Papa Leo XIV atakutana na kuzungumza na wakimbizi na wahamiaji
Papa Leo XIV atakutana na kuzungumza na wakimbizi na wahamiaji   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV, Ijumaa tarehe 12 Juni 2026 Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ambaye kwa huruma, upendo, upole na unyenyekevu wa Moyo wake Mtakatifu, aliinuliwa pale juu Msalabani, akawa ni chemchemi ya huruma, upendo na uzima kwa watu wote wa Mungu. Kristo Yesu anatufahamu na anatupenda sisi sote, na kila mmoja wakati wa maisha yake. Hofu yake ya kifo katika bustani ya Mizeituni, na mateso yake yametolewa kwa ajili ya kila mmoja wetu: “Mwana wa Mungu… ambaye alinipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.” Ametupenda wote kwa moyo wa kibinadamu. Kwa sababu hiyo, Moyo Mtakatifu wa Yesu, uliotobolewa kwa sababu ya dhambi zetu, na kwa ajili ya wokovu wetu, unachukuliwa kama alama na ishara kuu ya mapendo yake yasiyo na mipaka ambayo kwayo Mkombozi, ambaye ni Mungu, anampenda Baba wa milele na watu wote bila kikomo.” KKK 478. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako Mwaka 2002 aliitenga Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kuwa ni Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre, ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wakleri watambue kwamba, wao ni viongozi na wachungaji wa watu wa Mungu. Wanatumwa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wamepakwa mafuta ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili na faraja inayobubujika kutoka katika upendo na huruma ya Mungu. Kwa kupakwa mafuta, Mapadre wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, Kanisa na watu wake, kwa unyenyekevu, ari na moyo mkuu. Mapadre watoe kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili hata wao waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Mapadre wasikubali kumezwa na malimwengu, bali: utii, useja na ufukara, viwe ni dira na mwongozo katika maisha na utume wao.

Wakimbizi na wahamiaji watunzwe na kuheshimiwa
Wakimbizi na wahamiaji watunzwe na kuheshimiwa   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu akiwa “Las Palmas De Gran Canaria – Santa Cruz De Tenerife” atakutana na Mashirika yanayojishughulisha na kuwaingiza wakimbizi na wahamiaji kwenye maisha ya watu wa Mungu nchini Hispania; ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na hatimaye, kuagana na wenyeji wake na anatarajiwa kuwasili Roma majira ya Saa mbili kwa Saa za Ulaya sawa na Saa tatu kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati. Radio Vatican itakuwa nawe bega kwa bega ili kukushirikisha yale yanayojiri katika hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia Jumamosi tarehe 6 hadi 12 Juni 2026 kwa kunogeshwa na kauli mbiu: "Alzad la mirada" Yaani "Inua macho yako" Yn 4:35.

Hija ya Kitume Hispania
04 Juni 2026, 17:40