Hija ya 4 ya Kitume ya Papa:'El Escorial,’Moyo wa kiagostino wa Hispania unaungana na ziara ya Papa Leo XIV
Na Lorena Pacho – Mwakilishi-Madrid.
Sehemu chache zinawakilisha historia ya kidini ya Hispania kama vile Monasteri ya Kifalme ya Mtakatifu Lorenzo de El Escorial. Inapatikana katika Sierra de Guadarrama, jengo hili kubwa lina historia ya karne nyingi, imani, utamaduni, mafunzo, na sala ndani ya kuta zake. Ikizingatiwa kuwa moja ya vito vya thamani zaidi vya urithi wa Hispania, kutembea katika nafasi zake za kuvutia ni kama kuchukua safari kupitia historia ya nchi hiyo na, hasa, utawala wa Philip II, mtawala aliyeagiza ujenzi wake katika karne ya 16.
Monasteri inatunzwa na Waagostiniani
Papa Leo XIV alilijua mahali hapa vizuri. Kwake yeye, ilikuwa karibu nyumba ya familia, kwani monasteri imekabidhiwa kwa Shirika la Mtakatifu Agostino kwa zaidi ya karne moja na ni moja ya sehemu kuu za marejeo kwa familia ya Waagostiniani nchini Hispania. Ingawa kwa zaidi ya karne tatu, ilikaliwa na watawa wa Hieronymite tangu 1885 jengo hilo limekabidhiwa kwa watawa wa kiagostiniani, ambao wanaendelea kudumisha dhamira yake ya kidini, kielimu, na kiutamaduni. Leo hii, wanaume na wanawake arobaini na wawili watawa huleta uhai wa jengo hilo la ajabu kila siku, wakiendelea kufuata wazo lililoanzishwa na Mfalme Philip II: kutafuta maelewano kati ya sababu na imani, utamaduni na dini katika mambo yote.
Kwaya katika Misa ya Papa huko Madrid
Ni katika Muktadha wa ziara ya Papa huko Madrid, monasteri hiyo itachukua nafasi ya kwanza tena. Hii ni kwa sababu ‘Escolanía’ yake maarufu, yaani kwaya ya Monasteri ya Mtakatifu Lorenzo de El Escorial, itashiriki katika Misa ya “Corpus Christi”- Mwili na Damu ya Yesu itakayoongozwa na Papa Leo XIV tarehe 7 Juni 2026, ikileta sauti ya moja ya jumuiya za kidini zenye uwakilishi mkubwa nchini katika mji mkuu. Kundi hilo linaundwa na vijana wanaonufaika na ufadhili wa masomo unaotolewa na Waagostiniani ili kusaidia elimu yao ya kitaaluma na muziki. Wakati wa mwaka wa masomo, huamsha sherehe za kiliturujia Jumamosi na Dominika kwa uimbaji wao.
Hii ni kulingana na Padre Pedro Alberto Sánchez, mpiga kinanda na mkuu wa kwaya wa monasteri. "Walipata habari za ziara ya Papa Leo XIV nchini Hispania na fursa ya kushiriki katika sherehe zilizoandaliwa Madrid kwa hisia maalum. Wanajua kwamba Papa ni Muagostino , na wengi wao walipata fursa ya kukutana naye huko Roma alipokuwa bado Askofu, hata kabla ya kuteuliwa kuwa Kardinali. Wakati wa tamasha jijini, Padre Prevost wa wakati huo alikuwa mkarimu wa kutosha kutumia muda nasi na kupigwa picha na kikundi hicho," Padre alisimulia katika mahojiano na vyombo vya habari vya Vatican.
Imani na Utamaduni
Padre Sánchez pia alisisitiza umuhimu mkubwa wa Escolanía: "Kwaya hii inawakilisha kiungo hai kati ya imani na utamaduni. Papa Benedikto XVI alisema kwamba imani huzalisha uzuri, na vijana hawa hujumuisha uhusiano huu na historia. Kwa karne nyingi, Kanisa limeunda urithi mkubwa wa kisanii na muziki, utamaduni ambao si wa zamani tu bali unaendelea kuishi leo kupitia mipango kama hii. Ni mchango wetu kwa ulimwengu wa kibinadamu zaidi ambao Papa Leo XIV anatualika.”
Ziara kama Jenerali wa Awali wa Waugustini
Mkuu wa kwaya pia alikumbuka ziara nyingi ambazo Papa Leo XIV alifanya kwenye monasteri wakati wa miaka yake kama Mkuu wa awali wa Shirika la Waagostiniani. “Alipata nyakati za furaha hasa hapa. Ziara alizofanya kama Mkuu wa Shirika wa awali zilikuwa fursa muhimu za kupata uelewa wa karibu wa maisha na kazi ya ndugu zake. Wakati mmoja, alichagua El Escorial kama mahali pa Mkutano Mkuu wa Shirika, ishara dhahiri ya upendo na heshima aliyokuwa nayo kwa mahali hapa,” alielezea. Kwa Padre Sánchez, Monasteri ya Mtakatifu Lorenzo de El Escorial inawakilisha vile vile “sura ya Kikatoliki ya Hispania.”
Kito kilichotangazwa kuwa Eneo la Urithi wa Dunia
Ikizingatiwa kuwa mojawapo ya maonesho makubwa ya urithi wa kidini na kiutamaduni wa Hispania, Monasteri hiyo imejumuishwa katika orodha ya Urithi wa Dunia wa (Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni(UNESCO.) Kanisa lilijengwa na Mfalme Philip II katika karne ya 16 kama shukrani kwa Mungu kwa ushindi wa Vita vya Mtakatifu Quentin, vilivyopiganwa kwenye siku ya Mtakatifu Lorenzo mnamo 1557. Wakati huo huo, ilikusudiwa kuwezesha kazi nyingi: monasteri, makao ya kifalme, pantheon ya wafalme, maktaba, na kituo cha masomo. Kwa kuundwa na Juan Bautista de Toledo na kukamilishwa na mwanafunzi wake Juan de Herrera, jengo hilo linachukuliwa kuwa moja ya kazi bora za Kuzaliwa upya kwa Ulaya na moja ya sehemu zenye nembo zaidi za Kanisa nchini Hispania. Zaidi ya hayo, Licha ya ukuu wake wa usanifu, El Escorial inahifadhi urithi wa ajabu wa kisanii na kiutamaduni: kazi za Titian, El Greco, Velázquez, na Tintoretto, hati za maadhishi za thamani za enzi za kati, na moja ya maktaba muhimu zaidi za kihistoria barani Ulaya. Hazina inayoakisi kusudi la asili la monasteri: kuwa mahali pa wakati huo huo pa maombi, maarifa, na uzuri.
Imesasishwa tarehe 5 Juni 2026 saa 4.40 asubuhi na Angella Rwezaula.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here
