Borgo Laudato si':Papa atakula chakula na maskini 200 wa Jimbo kuu la Roma,Julai 11
Vatican News
Takriban watu 200 walio katika hali ya udhaifu wa kijamii kutoka Jimbo Kuu la Roma watashiriki katika tukio la "Chakula cha Mchana na Papa" Jumamosi, tarehe 11 Julai 2026. Siku ya kukaribisha na ushirika huko Borgo Laudato Si', katika Bustani za Kipapa za Castel Gandolfo. Ratiba hiyo inajumuisha Maadhimisho ya Ibada ya Misa pamoja na Liturujia ya Utunzaji wa kazi ya Uumbaji, kipindi cha kukaribisha na kuburudisha, ziara ya kuongozwa kwenye Bustan za Borgo Laudato Si', na hatimaye chakula cha mchana kitakachomuona Papa Leo XIV akishiriki nao.
Ni mpango huu unatokana na uzoefu wa mnamo tarehe 17 Agosti 2025, wakati Papa Leo XIV alipokula chakula cha mchana na watu wanaopitia umaskini kutoka Jimbo la Albano. Kutokana na uzoefu huo, tukio la kila mwaka linaloandaliwa na Kituo cha Mafunzo ya Juu cha Laudato si', ambacho husimamia maendeleo ya mpango wa Borgo Laudato si', lilizaliwa. Kila mwaka, Jimbo Kuu la Roma litaalikwa kuwashirikisha watu wanaopitia umaskini, wakimbizi, wahamiaji, na makundi mengine yaliyo hatarini kijamii, likiwapatia siku inayozama katika uzuri wa uumbaji na fursa ya kukutana na Papa. Tukio la mwaka huu 2026 ni matokeo ya ushirikiano kati ya Kituo cha Mafunzo ya Juu cha Laudato si', Baraza la Kipapa la Huduma ya upendo na Jimbo kuu la Roma.
Kanisa lililo karibu na walio katika mazingira hatarishi
"Borgo Laudato si' iliundwa ili kuonesha kwamba ulinzi wa uumbaji na utunzaji wa mtu binafsi ni utume mmoja," alisema Kardinali Fabio Baggio, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Juu cha Laudato si'. "Baada ya kutembelea Lampedusa, siku hii inawakilisha hatua mpya katika safari ya Papa Leo XIV kuelekea pembezoni mwa jamii za wakati wetu. Katika Borgo Laudato si', Baba Mtakatifu atakutana na watu wanaoishi katika mazingira magumu, akithibitisha tena kwamba Kanisa limeitwa kuishi katika maeneo ambapo utu wa binadamu unahitaji usikivu, ukaribu, na matumaini."
Safari hii inawakilisha huduma ya Kanisa kwa maskini, kama ilivyosisitizwa na Askofu Mkuu Luis Marín de San Martín, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo. "Chaguo la Baba Mtakatifu," alielezea "linathibitisha kwamba upendo unajumuisha ukaribu, kukutana, na kushiriki. Kanisa linapowaweka walio hatarini zaidi katikati, linaifanya Injili ionekane na kushuhudia kwamba hakuna mtu aliyetengwa katika moyo wa Mungu." "Tulitaka wahusika wakuu wa siku hii wawe watu wanaosindikizwa kila siku na parokia, Caritas, na mashirika mengi ya kikanisa na ya ushirika ya Jimbo Kuu la Roma.
Mkutano na Baba Mtakatifu unarejesha umuhimu kwa wale ambao mara nyingi hubaki wametengwa na kuwakumbusha jumuiya nzima ya Kikristo kuhusu jukumu la kuwakaribisha," aliongeza Kardinali Baldassare Reina, Makamu wa Papa Jimbo Kuu la Roma.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.
