Mwenyeheri Patriaki Elias Boutros Hoyes Kuanzia Mwaka 1899-1931
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 26 Julai 2026, kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo amesema kwamba Patriaki Elias Boutros Hoyek, wa Kanisa la Wamaroniti wa Antiokia alizaliwa kunako tarehe 4 Desemba 1843 huko Helta, Lebanon. Kunako mwaka 1870 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 14 Desemba 1889 akawekwa wakfu kuwa Askofu mkuu mwenye dhamana ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Tarehe 6 Januari 1899 akachaguliwa kuwa ni Patriaki wa Kanisa la Wamaroniti wa Antiokia na kuthibitishwa rasmi tarehe 19 Juni 1899. Akafariki dunia tarehe 24 Desemba 1931 akiwa na umri wa miaka 80 huko Bkerkè. Ni Muasisi wa Shirika la Watawa wa Maroniti wa Familia Takatifu. Akabahatika kuliongoza Kanisa kwa kipindi cha miaka 30 kwa sadaka na majitoleo makubwa katika shughuli za kichungaji. Kwa hakika anasema, Baba Mtakatifu Leo XIV alikuwa ni Mtu wa majadiliano na chemchemi ya matumaini; mwanga angavu na kielelezo na rejea katika maisha ya Kanisa, Kisiasa na Kijamii kiasi hata cha watu kuthubutu kumwita “Baba wa Lebanon Kubwa.” Sala za Mwenyeheri mpya ziwaongoze na kuwasindikiza watu wa Mungu nchini Lebanon kutafuta na kuambata amani ya kudumu.
Wakati huo huo, Kardinali Béchara Boutros Raï, Patriaki wa Kanisa la Wamaroniti wa Antiokia anasema, kutangazwa kwa Mtumishi wa Mungu Patriaki Elias Boutros Hoyek, Jumamosi tarehe 25 huko Dimane, nchini Lebanon, ni tukio ambalo limewakusanya watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia, ili kusherehekea kazi ya Mungu katika maisha na utume wa Patriaki Elias Boutros Hoyek, aliyesadaka maisha yake yote kwa uongozi wa Kimungu, akabahatika kuwa ni mwanga angavu katika historia ya Kanisa na Taifa la Lebanon. Hili ni tukio linaloshuhudia utukufu wa Mungu uliotendeka ndani mwake, zawadi ya utakatifu ambayo Mwenyezi Mungu huwakirimia waja wake wanaoishi kwa uaminifu na uadilifu tunu msingi za Kiinjili hadi dakika ya mwisho ya maisha yao. Hii ni siku ambayo mwangwi wake utabaki umeandikwa katika akili na nyoyo za watu wa Mungu nchini Lebanon, kama anavyosema Nabii Isaya: “Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi. Litachanua maua mengi, na kufurahi, naam, kwa shangwe na kuimba; litapewa uzuri wa Lebanoni, utukufu wa Karmeli na Sharoni; watauona utukufu wa Bwana, ukuu wa Mungu wetu.” "Gloria Libani Data Est Ei.” Isa 35:1-2.
Mwenyeheri Patriaki Elias Boutros Hoyek, kwake Dimane ni mahali ambapo alisadaka maisha katika utume, Mwenyezi Mungu akazisiliza sala zake, akatangaza na kushuhudia ukuu na utakatifu wa Mungu kwa machozi yake, akapambana bila kuchoka kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo na kwamba, leo hii, watu wa Mungu nchini Lebanon wanashuhudia kiongozi wao wa maisha ya kiroho akitangazwa kuwa ni Mwenyeheri, kwani tangu awali, walitambua ndani mwake kuwa ni: Baba, Mchungaji na Mwombezi wao, Mtu aliyekabidhiwa kwao kwa neema na baraka za Mwenyezi Mungu. Hili ni tukio kubwa la kumtukuza, kumshukuru na kumshangilia Mwenyezi Mungu kwa matendo makubwa anayotenda katika maisha ya watakatifu wake, ari na mwamko kwa waamini pia kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, bila kusahau kuwarithisha amana na utajiri huu, vijana wa kizazi kipya.
Ibada ya Misa Takatifu ya kumtangaza Mtumishi wa Mungu Patriaki Elias Boutros Hoyek, kuwa Mwenyeheri kwa niaba ya Baba Mtakatifu Leo XIV imeongozwa na Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, kiungo muhimu kati ya Kanisa la Wamaroniti na Kanisa Katoliki, katika kutangaza na kushuhudia uaminifu katika imani ya Kanisa takatifu, katoliki na la mitume; sanjari na uaminifu wa Kanisa la Wamaroniti huko Mashariki ya Kati. Tukio hili ni baraka na neema kwa watu wa Mungu nchini Lebanon na Injili ya matumaini kwa vijana wa kizazi kipya. Mwenyeheri Patriaki Elias Boutros Hoyek, alikuwa makini katika kutekeleza sera na shughuli za kichungaji, alibahatika kuwa na hekima na busara ya shughuli za kichungaji, moyo wa kibaba na imani thabiti ya Mtakatifu wa Mungu, huku akiongozwa na kauli mbiu yake ya Kiaskofu “Deus meus, voluntas tua” yaani “Mungu wangu, mapenzi yako yatimizwe.” Hii ni kauli mbiu iliyomzamisha katika fadhila ya unyenyekevu, katika maisha na utume wake, akajitahdi kutafuta kutekeleza mapenzi ya Mungu; ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu; akawa ni kielelezo na shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu matunda ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na matendo ya huruma: kiroho na kimwili.
Kila msimamo uliouchukua ulitokana na dhamiri nyofu iliyoangaziwa na imani thabiti na iliyojengwa juu ya uadilifu, haki, na unyenyekevu. Mwaka 1916 wakati wa baa kubwa la njaa nchini Lebanon, alisimama kidete kuhakikisha kwamba, watu wake wanapata chakula, kiasi cha kutajwa kuwa ni “Baba wa maskini na watu wanaokandamizwa. Alijahidi kuwekeza katika majadiliano ya kiekumene na kidini, ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; uhuru wa kidini na uhuru wa dhamiri. Ni kiongozi aliyechangia kuzaliwa kwa Nchi ya Lebanon mpya inayosimikwa katika demokrasia, maisha ya kiroho, elimu makini na utakatifu wa maisha. Ndiye Muasisi wa Madhabahu ya Mama Yetu wa Harissa, nchini Lebanon yaliyojengwa mwaka 1905 na kufunguliwa rasmi mwaka 1907, mahali pa sala na chemchemi ya matumaini kwa watu wa Mungu nchini Lebanon. Mwenyeheri Patriaki Elias Boutros Hoyek, alikuwa ni Mtu wa Sala, aliyewapenda watu wake upeo, mjenzi mwenye hekima na busara; kiongozi aliyekuwa na maono na kutokana na sifa hizi, sasa amekuwa ni shule ya imani, ukurasa angavu wa historia ya Kanisa inayoendelea kumwilishwa katika maisha ya watu wa Mungu nchini Lebanon. Mama Kanisa amemtangaza Mwenyeheri Patriaki Elias Boutros Hoyek mbele ya walimwengu kwamba ni Baba aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya Mungu, huduma kwa watu wake na uzalendo kwa nchi yake ya Lebanon. Maisha na utume wake ni mfano bora wa kuigwa na vijana wa kizazi kipya sanjari na wale wote wote wanaotaka kupyaisha imani yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi pamoja na ujenzi wa nchi yao.
