Tafuta

Papa Leo XIV anawaalika waamini kusali kwa ajili ya kuombea heshima kwa maisha ya binadamu, ambayo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayoakisi Uso wake, tangu kutungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika mtu. Papa Leo XIV anawaalika waamini kusali kwa ajili ya kuombea heshima kwa maisha ya binadamu, ambayo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayoakisi Uso wake, tangu kutungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika mtu.  

Nia za Baba Mtakatifu Leo XIV Kwa Mwezi Julai 2026: Heshima Kwa Maisha ya Binadamu

Papa Leo XIV anawaalika waamini kusali kwa ajili ya kuombea heshima kwa maisha ya binadamu, ambayo ni zawadi kutoka kwa Mungu, inayoakisi Uso wake, tangu kutungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika mtu. Papa Leo XIV anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya kutambua, kulinda na kudumisha thamani ya utu, heshima na maisha ya binadamu; Awakirimie uwezo wa kujifunza kupokea Injili ya uhai bila masharti; kutetea wasio na sauti!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane Paulo II katika Wosia wake wa Kitume, “Evangelium vitae” yaani “Injili ya uhai” kwa ufupi anakazia kuhusu: Thamani ya maisha, ukuu, utu, heshima na haki msingi za binadamu kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni Injili ya upendo wa Mungu kwa binadamu; Utu na heshima yake, mambo msingi yanayofumbatwa katika Injili. Katika ulimwengu mamboleo kuna mambo ambayo yanaendelea kutishia Injili ya uhai kwa kukumbatia utamaduni wa kifo. Haya ni matokeo ya watu kukengeuka pamoja na kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema. Kuna sera na mikakati mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inayotishia Injili ya uhai, ustawi na maendeleo ya wengi. Mtakatifu Yohane Paulo II anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete: kuheshimu, kulinda na kuhudumia Injili ya uhai, ili kukuza na kudumisha haki, maendeleo fungamani ya binadamu, uhuru wa kweli, amani na furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika sakafu ya maisha ya mwanadamu. Waamini wanapaswa kujipambanua kuwa ni watu wanaotetea Injili ya uhai kwa ajili ya maisha. Hata leo hii bado kuna damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumlilia Mwenyezi Mungu. Haya ndiyo mauaji ya kimbari na vita.

Sala kwa ajili ya kuombea heshima kwa maisha, utu na haki msingi
Sala kwa ajili ya kuombea heshima kwa maisha, utu na haki msingi   (@VATICAN MEDIA)

Kuna sera za utoaji na uzuiaji mimba; kifo laini pamoja na uzalishaji wa binadamu kwa njia ya chupa. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yamepelekea hata mauaji ya watoto wenye ulemavu kuanzia tumboni mwa mama zao. Yote haya ni matokeo ya uhuru unaoshindwa kutambua: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kumbe, kuna haja kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kutambua uwepo angavu wa Mungu na kuzingatia kanuni maadili na utu wema, kwa kuimarisha matumaini pamoja na maboresho katika huduma ya tiba ya mwanadamu. Jitihada hizi hazina budi kwenda sanjari na mchakato wa kupinga adhabu ya kifo na kwamba, umefika wakati wa kuachana na dhana ya “vita halali na ya haki”, ili kujenga na kudumisha kanuni maadili zinazolenga kukuza na kudumisha misingi ya haki na amani, pamoja na kupambana dhidi ya mauaji ya kimbari.

Athari za vita ni kubwa sana katika maisha ya binadamu
Athari za vita ni kubwa sana katika maisha ya binadamu

Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, Kristo Yesu ni chemchemi ya utimilifu wa maisha, mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya uhai, kwa sababu maisha ni tunu adhimu inayofumbatwa katika maadili na maisha ya kiroho. Ikumbukwe kwamba, utukufu wa Mungu unang’aa katika sura ya mwanadamu kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ufunuo wa utimilifu wa upendo wake, ambao ni zawadi ya maisha ya uzima wa milele. Hii ni changamoto kwa waamini kudumisha upendo kwa Injili ya uhai, kwa kuwajibika barabara kulinda na kudumisha maisha. Utu, heshima na haki msingi za watoto ambao hawajazaliwa zinapaswa kulindwa na wote. Maisha yana thamani hata katika mateso, magonjwa na uzee kama yanavyofafanuliwa katika Amri za Mungu. Huu ni mwaliko wa kuendelea kuwa waaminifu katika Sheria na Injili ya uhai. Kristo Yesu, kwa mateso, kifo na ufufuko wake ameonesha kilele cha ufunuo wa Injili ya uhai. Msalabani, Kristo Yesu alionesha ukuu na utukufu wake, chemchemi ya maisha mapya na mwaliko kwa Wakristo kusimama kidete kulinda Injili ya uhai.

Maisha ya binadamu yanapaswa kulindwa tangu mtoto anapotungwa mimba
Maisha ya binadamu yanapaswa kulindwa tangu mtoto anapotungwa mimba   (@Vatican Media)

Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, Usiue kwa sababu maisha ya mwanadamu ni matakatifu na yasioharibika na kwamba, Mwenyezi Mungu ni chanzo na utimilifu wa maisha ya binadamu. Kanisa linalaani vitendo vyote vya utoaji mimba, kifo laini au watu kujinyonga kwa sababu hii ni dhambi dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huruma na upendo ni urithi na amana ya ubinadamu. Mwanadamu anapaswa kuheshimu Sheria na Amri za Mungu, kanuni maadili na utu wema. Upendo kwa Mungu na jirani, usaidie kulinda na kudumisha Injili ya uhai. Mtakatifu Yohane Paulo II analihamasisha Kanisa kujenga na kudumisha utamaduni mpya wa maisha kwa kulinda na kutetea Injili ya uhai; kwa kutangaza na kuadhimisha Injili ya upendo unaomwilishwa katika huduma, ili kuenzi: ukuu na utakatifu wa maisha. Injili ya uhai iwe ni sehemu ya maisha ya sala ya kila siku, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa pamoja na Liturujia ya Mwaka wa Kanisa. Huu ni mchakato wa ushuhuda wa imani tendaji unaozingatia mpango wa uzazi kwa njia ya asili. Kwa kutambua kwamba, familia ni tabernakulo ya Injili ya uhai; kwa kuwalinda na kuwahudumia watu wanaoteseka kwa uzee na magonjwa ya muda mrefu.

Familia ni Tabernakulo ya kwanza ya maisha
Familia ni Tabernakulo ya kwanza ya maisha   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, Baba Mtakatifu Leo XIV katika Nia zake kwa Mwezi Julai 2026 zinazosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Mawasiliano Jamii, anawaalika waamini kusali kwa ajili ya kuombea heshima kwa maisha ya binadamu, ambayo ni zawadi takatifu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayoakisi Uso wake, tangu kutungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika mtu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya kutambua, kulinda na kudumisha thamani ya utu, heshima na maisha ya binadamu, awakirimie uwezo wa kujifunza kupokea Injili ya uhai bila masharti; kwa kujali kwa upole udhaifu wa binadamu, ili hatimaye, kuambatana na kila hatua ya maisha kwa heshima na kuwatetea kwa ujasiri watu wasiokuwa na sauti. Baba Mtakatifu Leo XIV anasali na kuomba msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu pale binadamu anapoangukia katika hali ya kutojali au kuelemewa na utamaduni wa kifo, kwa kushindwa kuona ndani ya wengine kiumbe aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu anayestahili upendo. Anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi ili awajalie moyo mpya, ulio tayari daima kuchagua Injili ya uhai na mikono ya ukarimu inayolinda kwa matendo halisi.

Adhabu ya kifo imepitwa na wakati
Adhabu ya kifo imepitwa na wakati

Baba Mtakatifu Leo XIV analiombea Kanisa ili liwe ni chombo na shuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; nyumba iliyo wazi na ambamo uhai unaadhimishwa; utu unaheshimiwa na kulindwa daima. Waamini wajalie fadhila ya kuupenda uhai kama Kristo Yesu mwenyewe anavyoupenda: kwa upole, uaminifu na majitoleo ya nafsi zao. Waamini wawe ni mashuhuda na vyombo vya kutangangaza na kushuhudia kwa maneno lakini zaidi kwa njia ya matendo, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kitume, “Evangelium vitae” yaani “Injili ya uhai” alipinga adhabu ya kifo na hatimaye, Katekisimu ya Kanisa Katoliki ikafanyiwa marekebisho na kwamba, adhabu ya kifo ingeweza kutumika ikiwa kama njia zisizohusisha umwagikaji wa damu zinatosha kutetea na kulinda maisha ya watu, amani na usalama wao dhidi ya adui, kwa kweli njia hizi karibu haziko kabisa. Adhabu ya kifo ni ukatili mkubwa na usio wa lazima! Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la “Amnesty International” linasema katika kipindi cha Mwaka 2025 watu 2,707 walipoteza maisha kutokana na utekelezaji wa adhabu ya kifo katika nchi 17 duniani, idadi kubwa kuwahi kutoka duniani tangu mwaka 1981, hili ni ongezeko la asilia 78%, ndiyo maana Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujizatiti kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa unatekeleza dhamana na wajibu wake katika nchi zaidi ya 90 sehemu mbalimbali za dunia, mtandao unaowaunganisha watu zaidi ya milioni 22 wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa dhhidi ya utamaduni wa kifo.

Nia Mwezi Julai 2026
07 Julai 2026, 13:42