Tafuta

Papa Leo XIV akipata chakula cha pamoja na maskini na wale wote wanaotengwa na jamii kutokana na sababu mbalimbali. Papa Leo XIV akipata chakula cha pamoja na maskini na wale wote wanaotengwa na jamii kutokana na sababu mbalimbali.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV: Chakula Cha Pamoja na Maskini: Njaa ya Haki na Upendo

Papa Leo XIV amesema amekwenda kati yao akiwa na kiu na njaa ya haki, upendo wa kweli; njaa ya Kanisa linalothubutu kufungua malango yake, ili kuwapokea na kuwakirimia watu wote wa Mungu; upendo wake usiokuwa na kifani; mahali ambapo watu wote wanajisikia kuwa ni ndugu wamoja; mahali ambapo waamini wanaishi fadhila ya upatanisho, msamaha na amani ya kweli. Maskini ni amana na utajiri wa Mama Kanisa walengwa wakuu wa Uinjishaji wa kina!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema, Kanisa linawategemea sana maskini katika maisha na utume wake, kwani maskini ni amana na utajiri wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kimsingi, maskini ndio walengwa wakuu wa Injili. Dhana ya umaskini inajikita katika umaskini wa hali na mali; maadili na utu wema; kwani wote hawa, Kristo Yesu amejisadaka kwa ajili ya kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu. Wakristo wanapaswa kuwajali, kuwathamini na kuwapenda maskini na watu wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama afanyavyo mama mzazi kwa watoto wake. Kanisa linatoa huduma ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa maskini, kwa kujali na kuthamini utu, heshima na haki zao msingi, kwani hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mababa wa Kanisa kwa namna ya pekee, wanawaalika Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza kutoka kwenye shule ya maskini kwani kati ya maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum, humu humu kuna watakatifu na watu ambao wanaweza kuwafundisha wengine tunu msingi za maisha ya kijamii, kiutu na kiroho. Maskini si mzigo bali ni shule makini kwa watu wa Mungu. Kumbe, kuna umuhimu wa kusimama kidete: Kulinda na kutetea: Utu, heshima na haki msingi za maskini; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Maskini ni kielelezo cha Kristo Yesu kati ya watu wake. Katika shule ya upendo, watu wanatafuta faraja, mahusiano na mafungamano; utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, waamini wanaweza kujifunza kutoka kwa maskini kwa kuwakaribisha, kuwasikiliza, kuwakirimia na kuwahudumia kwa upendo na nidhamu ya hali ya juu.

Papa Leo XIV akisalimiana na Makardinali.
Papa Leo XIV akisalimiana na Makardinali.   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi mchana tarehe 11 Julai 2026 amepata chakula cha mchana na maskini 200 kutoka Jimbo kuu la Roma. Chakula hiki cha hisani limeandaliwa kwa awamu ya pili kwa ushirikiano kati ya: Jimbo kuu la Roma; Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo sanjari na Kituo cha Mafunzo ya Juu cha Borgo Laudato si' kilichoanzishwa huko Castel Gandolfo, Italia, kwa matakwa ya Papa Francisko. Kituo hiki kinalenga kukuza na kudumisha: elimu ya ikolojia fungamani ya binadamu, utunzaji bora wa kazi ya uumbaji, na kuoanisha maendeleo, uchumi, na heshima kwa utu wa mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu mintarafu kanuni za Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si”, yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Baba Mtakatifu Leo XIV akizungumza na Maskini wa Jimbo kuu la Roma, Kwenye Bustani za Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, amewaambia kwamba, amekuja kati yao akiwa na kiu na njaa ya haki, upendo wa kweli; njaa ya Kanisa linalothubutu kufungua malango yake, ili kuwapokea na kuwakirimia watu wote wa Mungu; upendo wake usiokuwa na kifani; mahali ambapo watu wote wanajisikia kuwa ni ndugu wamoja; mahali ambapo waamini wanaishi fadhila ya upatanisho, msamaha na amani ya kweli. Itakumbukwa kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro ni Daraja kwa watu wote wa Mungu, ili waweze kuishi katika haki, amani, upendo na mshikamano huku wakijitahidi kung’olea mbali mambo yote yanayosababisha ukosefu wa haki, kwa kuishi katika umoja, kama kielelezo cha watu kukutana, ili kujenga ulimwengu tofauti kabisa; yaani ni mwaliko wa kujenga Ulimwengu unaosimikwa katika Injili ya matumaini, mwanga wa Mataifa; mahali ambapo hapana vita, chuki, uhasama wala mifumo mbalimbali ya ubaguzi. Hii ndiyo tajiriba ya Mama Kanisa katika mang’amuzi ya ujenzi wa haki, amani na upendo.

Mshikamano wa upendo na maskini
Mshikamano wa upendo na maskini   (@Vatican Media)

Kardinali Fabio Baggio Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu, Kardinali Baldassare Reina, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma pamoja na Askofu Mkuu Luis Marín de San Martín ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo (Dicastery for the Service of Charity), walitoa Neno la kumkaribisha Baba Mtakatifu Leo XIV, ili kuzungumza na maskini pamoja na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Kabla ya Mlo huu wa mchana, walengwa wamehudhuria Ibada ya Misa Takatifu, sanjari na Liturujia ya Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote na baadaye, wakatembelea Kituo cha Mafunzo ya Juu cha Borgo Laudato si.” Katika mahibiri yake Kardinali Fabio Baggio amekazia umuhimu wa watu kuishi kwa umoja na upendo kama familia moja ya binadamu; kwa kuheshimu na kutunza mazingira bora nyumba ya wote; kwa kushikamana na kusaidiana kwa upendo. Baba Mtakatifu Leo XIV katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anataka kuonesha mshikamano wa udugu wa kibinadamu na maskini wote, kwa kutambua Uso wa Kristo Yesu kati ya maskini. Amewapongeza watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma kwa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji katika maisha ya jumuiya inayowapatia ifadhi na usalama wa maisha. Hiki ni kielelezo cha Injili ya huduma kwa maskini, mfano hai kutoka kwa Kristo Yesu mwenyewe. Rej. Yn 13:15. Kwa hakika, maskini wanahitaji kila siku faraja kutoka kwa Kristo Yesu.

Papa Leo XIV ana kiu na njaa ya haki na amani
Papa Leo XIV ana kiu na njaa ya haki na amani   (@Vatican Media)

Askofu mkuu Luis Marín de San Martín ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo amekazia sera na mikakati ya Mama Kanisa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini kwani ni kwa njia hii, Kanisa linaendelea kuwa ni shuhuda mwaminifu na mkweli wa Injili ya upendo na ukarimu; mwaliko wa kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora, kama sehemu ya kazi ya Uumbaji. Hizi ni tunu zinazowafanya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kuwa ni waaminifu kwa Injili ya Kristo na washiriki waaminifu wa tunu msingi za Kiinjili, kwa kujenga na kudumisha ujirani mwema na kutembea kwa pamoja kama familia Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika mchakato wa utunzaji bora wa nyumba ya wote sanjari na kugawana pamoja na kushirikishana mema ya nchi kwa moyo wa upendo na ukarimu.

Chakula na Maskini
12 Julai 2026, 15:40