Tafuta

Papa alituma ujumbe kwa njia ya video. Papa alituma ujumbe kwa njia ya video.  (@VATICAN MEDIA)

Papa Leo XIV:Kugundua upya urithi wa zawadi ya imani katika historia ya Marekani

Kanisa nchini Marekani liendelee kuitumikia na kuinjilisha jamii,ndiyo wito wa ujumbe kwa njia ya video alioutuma Papa Leo XIV katika fursa ya kuhitimisha Hija ya Kitaifa ya Ekaristi chini Marekani."Ni muhimu kugundua upya urithi unaotambua thamani ya yaliyopita lakini pia unatazama wakati ujao, kama chanzo cha upyaisho na umoja."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe kwa njia ya video uliotolewa Dominika tarehe 5 Julai 2026, ukielekezwa kwa washiriki wa Hija ya Kitaifa ya Ekaristi iliyohitimishwa katika nchi yake ya asili, Marekani na alisisitiza thamani ya "Imani ambayo imejaza taifa zima ikiwakilisha urithi kutoka zamani, lakini pia lenzi ya kutazama wakati ujao, ikiboresha kujitolea kwa kuitumikia jamii katika nyanja zote za jamii, kuanzia elimu hadi huduma ya afya. Papa Leo XIV alikumbuka umuhimu wa hija, ambayo ilipitia makoloni mengi ya awali kumi na matatu ya Marekani wakati wa maadhimisho ya miaka 250 ya Azimio la Uhuru. Aliomba umoja, upyaisho, na uponyaji kwa nchi, chini ya kauli mbiu: "Taifa Moja Chini ya Mungu." Nia hizi pia ni za thamani kwangu,” Papa alieleza.

Urithi wa Ekaristi nchini  Marekani,upyaishwe

Baba Mtakatifu Leo XIV kadhalika alikumbuka jukumu la imani katika historia ya taifa, ambalo "linatambua ukuu wa Mungu hata kabla ya kuanzishwa kwake rasmi." Kisha alirudi kwenye uzinduzi wa hija, iliyofanyika Mtakatifu  Augustino, Jimbo Kuu la  Florida, ambapo mnamo tarehe 8 Septemba 1583, katika Sherehe ya Kuzaliwa kwa Bikira Maria, wapelelezi na walowezi wa Kihispania walisherehekea Misa ya Shukrani walipofika, ikifuatiwa na siku kuu  iliyohudhuriwa na kabila la Seloy la eneo hilo. Tukio hilo la kihistoria, pamoja na mengine mengi, linashuhudia urithi wenye nguvu, lakini ambao haujulikani sana, wa Ekaristi huko  Marekani. Urithi huu, mbali na kusahaulika, lazima uendelee kutumika kama chanzo cha upyaisho na umoja.

Nguvu inayotokana na sala: watakatifu

Kifungo ambacho kimepitishwa hadi vizazi vilivyofuata vya Wakatoliki wa Marekani, kikiwatia moyo wanaume na wanawake kushuhudia Injili "kwa njia kubwa." Papa Leo XIV  aliwataja mashahidi wa New York na Georgia: Watakatifu Kateri Tekakwitha, Elizabeth Ann Seton, Katharine Drexel, John Neumann, na Mtumishi wa Mungu Fulton Sheen atakayetangazwa kuwa mwenyeheri hivi karibuni. Tusimsahau Mtakatifu Francisca Xavier Cabrini, mwanzilishi wa Masista Wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, ambaye alisaidia mahitaji ya kiroho na kimwili ya wahamiaji maskini zaidi. Kazi kubwa ya kitume ya wanaume na wanawake hawa watakatifu, na wengine kama wao, isingewezekana bila nguvu waliyopata kila siku kutokana na nyakati za maombi ya kimya kimya mbele ya hema la Ekaristi.

Thamani ya Ekaristi, uwepo wa Yesu

Papa Leo XIV pia alitambua jinsi maadhimisho ya Misa, maandamano ya Ekaristi, na kuabudu Sakramenti Takatifu, ambayo iliashiria hatua mbalimbali za hija, inavyounda "urithi mkubwa wa imani," unaowezesha kupata uzoefu wa  jinsi "Mwili na Damu ya kweli ya Bwana wetu Yesu Kristo ilivyo maisha ya Kanisa la hija duniani." Katika suala hilo, alinukuu maneno ya Mtakatifu Yohane Paulo II katika waraka  wa Kitume wa Ecclesia de Eucharistia: Ekaristi, uwepo wa Yesu unaookoa katika jumuiya ya waamini na lishe yake ya kiroho, ni zawadi ya thamani zaidi ambayo Kanisa linaweza kuwa nayo katika safari yake katika historia. Akirejea tena sherehe za maadhimisho ya miaka 250 ya kuanzishwa kwa Marekani, hatimaye Papa alionesha matumaini kwamba uzoefu wa hija utawasaidia washiriki kuendelea kutazama mbinguni, wakikumbuka kwamba "Ekaristi ni zawadi ya thamani, lishe yetu muhimu." Ni kwa kutambua na kukumbatia zawadi hii hasa ndipo Kanisa nchini Marekani litapata nguvu ya kuendelea na huduma yake ya upendo  kwa jamii kwa ujumla zaidi, hasa katika maeneo ya elimu, huduma za afya na huduma msingi za kijamii, huku likiendelea na dhamira yake ya uinjilishaji.

PAPA UJUMBE WA VIDEO KWA MAREKANI

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

05 Julai 2026, 17:27