Papa Leo XIV: Kumbukizi ya Miaka 25 ya Tamasha la Halleluiya!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Tamasha la Halleluya ni tukio la kila mwaka la Muziki na Sanaa za Kikatoliki linalofanyika Fortaleza, nchini Brazil, kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “The Party That Never Ends" Yaani "Sherehe Isiyo na Mwisho." Hili ni tukio kubwa la maisha ya kiroho linaloadhimishwa huko Amerika ya Kusini. Kwa mara ya kwanza lilianza kuonesha cheche zake kunako mwezi Julai 1995 na kuanza kushika kasi yake ya sasa kunako mwaka 1997. Hili ni tamasha za muziki wa Kikatoliki linalokita mizizi yake katika: Maonesho ya: Muziki, dansi na ngoma; vipindi vya sala, na shughuli za kitamaduni sanjari na maonesho ya sanaa ya jamii. Huu ni mkusanyiko wa furaha ya maisha ya kiroho unaosherehekea, kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake.Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, leo hii imani haina budi kutangazwa, kushuhudiwa na kutamadunishwa kwani huu ni mchakato wa uinjilishaji wa tamaduni na utamadunisho wa Injili unaoiwezesha Habari Njema ya Kristo Yesu kuingia na kupenyeza mizizi yake katika tamaduni mbalimbali, ikiikubali, ikiisafisha, na kuipatia maana mpya bila kuharibu utambulisho wa watu mahalia. Lengo ni kuifanya Injili ya Kristo Yesu uwe ni ujumbe unaozungumza lugha, uzoefu na tajiriba ya watu mahalia. Tamasha la Halleluya kwa mwaka 2026 linaadhimisha kumbukizi ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake tangu tarehe 22 hadi 26 Julai 2026. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV amewatumia ujumbe wa video washiriki wa Tamasha hii ambalo tangu kuanzishwa kwake limegusa sakafu ya mioyo ya watu wengi mintarafu muziki, nyimbo na ibada na hivyo kuwa ni chemchemi ya uinjilishaji na utamadunisho; toba na wongofu wa ndani na kwamba, kwa vijana wengi, tamasha hili limekuwa ni chemchemi ya miito ya Kipadre na Kitawa.
Tamasha hili ni muhimu sana kwa maisha ya vijana kwani ni chachu inayoamsha ari mpya ya kitume miongoni mwa waamini na hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe 28 Julai 2025 alizindua maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa vijana wa kizazi kipya, na kuhitimishwa tarehe 3 Agosti 2025 akiwataka vijana kuwa ni vyombo, wajenzi na mashuhuda wa amani na upatanisho. Alikazia umuhimu wa mawasiliano na ushuhuda wa imani kama nyenzo msingi za ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika: Umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV aliwakumbusha vijana kwamba, wao ni mashuhuda na mahujaji na kwamba vijana : “Ninyi ni chumvi ya dunia… Ninyi ni nuru ya ulimwengu.” Mt 5: 13-16. Baba Mtakatifu Leo XIV anakiri kwamba, katika hija zake za kitume hivi karibuni na wakati wa Maadhimisho ya Jubilei ya Vijana wa kizazi kipya aliona na kushuhudia nguvu muhimu ya kimisionari inayopania kuleta mabadiliko kwa njia ya mwanga na tunu za Kiinjili.
Baba Mtakatifu anawataka vijana kukuza na kudumisha chachu hii ya kimisionari; muhimu kwa wabatizwa wote, tayari kutangaza na kushuhudi Habari Njema ya Wokovu, ili watu watambue kwamba, Kristo Yesu ndiye majibu muafaka ya matamanio yao halali kutoka katika undani wa mioyo yao, kwa kuwafunulia ukweli juu ya ubinadamu wao. Baba Mtakatifu anawataka vijana wa kizazi kipya kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa ari, moyo mkuu na ujasiri kwamba maisha bila Kristo ni maisha bila neema! Yeye ndiye Njia, Kweli, na Uzima. Re Yn 14:6; Kristo Yesu ndiye anayetoa maana ya uwepo wa mambo yote na kwamba, hii ndiyo imani inayowasukuma waamini kuwashirikisha wale wawapendao zaidi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata hivyo, inawezekana kwamba shauku iliyojitokeza wakati wa tamasha hili ikapungua kadiri muda unavyopita. Ili kudumisha mwali wa imani na kushuhudia ufufuko kwa marafiki zao na wale wanaokutana nao katika hija ya maisha yao, ni lazima vijana waendelee kuwapo katika uwepo wa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, ili kujenga na kudumisha uhusiano wa kweli na Kristo Yesu.
Huu ni uhusiano unaohitaji uthabiti, uvumilivu na uhakika kwamba, Baba wa mbinguni kamwe hawezi kuwaacha na anakuja kukutana nao katika Mwana wake mpendwa Kristo Yesu. Basi, vijana wasimwogope Kristo Yesu! Yeye haondoi chochote; Yeye hutoa kila kitu, kama anavyosema Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI. Kwa vijana wale wanaojikabidhi kwa Kristo Yesu hupokea mara mia zaidi. Rej. Mk 10:29-30) na daima huibuka kidedea na wakiwa washindi. “Katika michezo, tunaona furaha ya mshindi lakini pia huzuni ya aliyeshindwa. Pamoja na Kristo, sisi hushinda daima” Rej. Rum 8:37! Watakatifu ni mashuhuda wa jambo hili” anasema, Baba Mtakatifu Leo XIV anayewaalika vijana kupata msukumo kutoka kwa mfano wa Mtakatifu Carlo Acutis: yeye anawaonesha jinsi ya kumweka Kristo Yesu katikati ya kila jambo, hata katika matumizi yao ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, awe ni kielelezo na mfano bora wa kuigwa katika matumizi bora zaidi, yenye kiasi na nidhamu ya teknolojia ya akili unde. Vinginevyo mwanadamu anaweza kuvutwa katika ulimwengu usio kweli, ambapo mambo ya muda mfupi, sura ya nje tu, na udanganyifu huchukua nafasi ya tunu za kweli na mambo yenye umuhimu wa kweli. Hatimaye, Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake kwa washiriki wa Tamasha la Halleluya kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake, anawaalika vijana wa kizazi kipya kumpatia nafasi Roho Mtakatifu awashe ndani mwao upendo mkuu zaidi, upendo wenye uwezo wa kubadili ujana wao kuwa ni nguvu ya uinjilishaji na hivyo kumfanya kila kijana kuwa ni jiwe hai katika ujenzi wa "mji wa amani" wanaoutamani sana, au, kama Mtakatifu Augustino alivyosema, “Mji wa Mungu uliopo ndani ya mji wa wanadamu.” Huku akimwomba Mwenyezi Mungu awaimarishe katika nyakati za majaribu na kuwasaidia kuishi wito wao wa utakatifu kwa uaminifu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa baraka zake za kitume kwa washiriki na waandaaji wa Tamasha la Halleluya.
