Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV anasikitika kuona kwamba, pepo za vita zinavuma tena huko Mashariki ya Kati, Ukraine na Urusi sanjari na sehemu mbalimbali za dunia Baba Mtakatifu Leo XIV anasikitika kuona kwamba, pepo za vita zinavuma tena huko Mashariki ya Kati, Ukraine na Urusi sanjari na sehemu mbalimbali za dunia 

Papa Leo XIV: Pepo za Vita Zinavuma Tena Uko Mashariki ya Kati, Ukraine na....

Baba Mtakatifu Leo XIV anasikitika kuona kwamba, pepo za vita zinavuma tena huko Mashariki ya Kati, Ukraine na Urusi sanjari na sehemu mbalimbali za dunia, ambako pepo hizi za vita zinapanda mbegu ya vurugu, hofu na vifo na kuendelea kuwaathiri watu wasiokuwa na hatia. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoruhusu pepo hizi za vita kuzima mwali wa matumaini na amani, hata pale mwali huu unapoonekana kuwa dhaifu na usio imara. Majadiliano!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maandiko Matakatifu yanasema, Mwenyezi Mungu baada ya kukamilisha kazi yake ya uumbaji alijipatia siku ya mapumziko, changamoto kwa binadamu kufurahia siku za likizo na mapumziko, ili kupata nafasi ya kutafakari na kujiwekea sera na mikakati kwa siku za usoni. Lakini kutokana na uchu wa mali na faida ya haraka haraka, leo hii binadamu amegeuzwa kuwa ni mtumwa wa kazi na wala hana hata wakati wa kujipumzisha. Ikumbukwe kwamba, Kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu, kumbe, inapaswa kuwa na uhusiano na sehemu nyingine za maisha ya binadamu. Likizo iwe ni fursa ya kuendeleza utamaduni, ari na moyo wa sala katika maisha. Kiwe ni kipindi cha kupyaisha na kunogesha maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili!

Vita imepelekea ongezeko la baa ya njaa, magonjwa na umaskini
Vita imepelekea ongezeko la baa ya njaa, magonjwa na umaskini   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV, mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 12 Julai 2026 amewashukuru watu wa Mungu mjini Castel Gandolfo kwa moyo wao wa ukarimu na mapendo, wakati huu wa likizo yake ya Kipindi cha Kiangazi. Ametumia fursa hii kuwakaribisha waamini, mahujaji na wageni wote waliofika kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, ili kuweza kukutana naye. Likizo ni nafasi muafaka ya kujenga, kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati na Mwenyezi Mungu, kwa kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu, lakini zaidi kwa kuongozwa na Amri Kumi za Mungu kama dira na mwongozo wa maisha.

Likizo ni kipindi cha sala, mapumziko na kujisomea
Likizo ni kipindi cha sala, mapumziko na kujisomea   (@Vatican Media)

Ni nafasi ya kutafakari kuhusu Fumbo la maisha ya binadamu, ili kubainisha ikiwa kama maisha yana alama na chapa ya uwepo endelevu na angavu wa Mwenyezi Mungu, ambaye kamwe hachoki kuwaongoza waja wake katika mapito ya maisha. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Likizo ya Kipindi cha Kiangazi, anaitumia kwa ajili ya: Mapumziko, Kusali, Kujisomea na Kujiandaa kwa ajili ya maisha na utume wake kwa siku za mbeleni. Ameonesha nia ya kutembelea nchini Mexico na Perù, ambako kama mmisionari ameishi na kufanya kazi huko kwa takribani miaka ishirini lakini bado mipango inaendelea kufanyika!

Papa Leo XIV yko kwenye mapumziko ya Kiangazi
Papa Leo XIV yko kwenye mapumziko ya Kiangazi   (@Vatican Media)

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Leo XIV anasikitika kuona kwamba, pepo za vita zinavuma tena huko Mashariki ya Kati, Ukraine na Urusi sanjari na sehemu mbalimbali za dunia, ambako pepo hizi za vita zinapanda mbegu ya vurugu, hofu na vifo na kuendelea kuwaathiri watu wasiokuwa na hatia. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoruhusu pepo hizi za vita kuzima mwali wa matumaini na amani, hata pale mwali huu unapoonekana kuwa dhaifu na usio imara. Baba Mtakatifu Leo XIV ameonesha kwamba: majadiliano katika ukweli na uwazi; utamaduni wa watu kukutana na diplomasia inayofuatili kwa ustahimilivu; hii “ndiyo njia pekee inayoweza kuleta amani ya haki na ya kudumu; ambapo watu wanaweza kuishi wakiwa wamepatanishwa, katika usalama wa pande zote na kwa kuheshimu utu wa kila mtu.”

Likizo Kiangazi
13 Julai 2026, 16:38