Tafuta

Tarehe 4 Julai 2026 Marekani imeadhimisha kumbukizi ya Miaka 250 tangu ilipojipatia uhuru wake wake kutoka kwa Mwingireza, tarehe 4 Julai 1776 Tarehe 4 Julai 2026 Marekani imeadhimisha kumbukizi ya Miaka 250 tangu ilipojipatia uhuru wake wake kutoka kwa Mwingireza, tarehe 4 Julai 1776   (2026 Getty Images)

Papa Leo XIV: Ujumbe Kumbukizi Miaka 250 ya Uhuru wa Marekani

Papa Leo XIV kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 250 tangu Marekani ijipatie uhuru wake amewaandikia barua watu wa Mungu nchini Marekani, akiwapongeza kwa Maadhimisho, yanayofumbatwa katika misingi ya uhuru, usawa, utafutaji wa furaha ya kweli, haki na serikali huru na ya kidemokrasia. Wamarekani wamekuwa wakifanya kazi kwa pamoja, ili kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao kanuni msingi zinazotekelezwa kwa sadaka na majitoleo makubwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Marekani ni Taifa linaloundwa na majimbo 50 na linakalia sehemu kubwa ya Bara la Amerika. Miji yake muhimu zaidi ni pamoja na: New York, Washington DC, ambao ndiyo mji mkuu, Los Angeles na Chicago. Tarehe 4 Julai 2026 Marekani imeadhimisha kumbukizi ya Miaka 250 tangu ilipojipatia uhuru wake wake kutoka kwa Mwingireza, tarehe 4 Julai 1776 ambapo viongozi wa makoloni 13 wakiwemo Thomas Jefferson na Benjamin Franklin walisaini “Tamko la Uhuru” wakitangaza kwamba wanajitenga na Uingereza; tukio linalosimulia hadithi ya ndoto kubwa, uongozi wa kuthubutu, na safari endelevu ya kutafuta uhuru na fursa. Kwa miaka 250, Marekani imehamasisha ubunifu, imeimarisha ushirikiano, na imeunganisha watu duniani kote. Rais Donald Trump wa Marekani amehutubia taifa kuelekea katika kilele cha Maadhimisho ya Kumbukizi ya miaka 250 ya uhuru wa Marekani. Amesisitiza kwamba: Marekani ndiyo Jamhuri ya kale zaidi, yenye uhuru mkubwa, na yenye nguvu zaidi katika historia ya mwanadamu, huku akisifu katiba yao thabiti na mafanikio makubwa ya kipekee yaliyopatikana kwa baraka na neema ya Mungu duniani. Kanuni maadili na utu wema wa kila nchi ni mambo yanayofumbatwa kwa Serikali kulinda na kudumisha Injili ya uhai, hususan kwa watu wanyonge ndani ya jamii.

Papa Leo XIV akisherehea Miaka 250 ya Uhuru wa Marekani.
Papa Leo XIV akisherehea Miaka 250 ya Uhuru wa Marekani.   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV amekubali kupokea Medali ya Uhuru iliyotolewa na Kituo Kikuu cha Katiba, nchini Marekani, huko Philadelphia. “Liberty Medal of the National Constitutional Center.” Kumbe, haki ya mtu kuishi na uhuru wa kweli ni mambo msingi katika matumaini ambayo yameendelea kulitegemeza Taifa la Marekani, lakini kwa bahati mbaya uhuru huu umetafsiriwa vibaya kwa watu kufanya yale wanayotaka kufanya. Lakini uhuru wa kweli unakita mizizi yake kwa mwanadamu kusimamia ukweli na kile kilicho chema, ili kutafuta na hatimaye kuambata furaha ya kweli katika maisha; hii ni sadaka safi sana kwa watu wa Marekani ambao wamesadaka maisha yao kwa ajili ya kusimamia ukweli wa Injili ya maisha na hatima yake, kumjua Mwenyezi Mungu na ukuu pamoja na utukufu wake na kwamba, kwa miaka mingi, Marekani imekuwa ikiongoza katika kutafuta na kudumisha uhuru wa kidini.

Papa Leo XIV amekubali kupokea Medali ya Miaka 250 ya Uhuru wa USA
Papa Leo XIV amekubali kupokea Medali ya Miaka 250 ya Uhuru wa USA   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 250 tangu Marekani ijipatie uhuru wake kutoka kwa Mwingereza, amewaandikia barua watu wa Mungu nchini Marekani, akiwapongeza kwa Maadhimisho, yanayofumbatwa katika misingi ya uhuru, usawa, utafutaji wa furaha ya kweli, haki na serikali huru na ya kidemokrasia. Katika kipindi chote hiki Wamarekani wamekuwa wakifanya kazi kwa pamoja, ili kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao kanuni msingi zinazotekelezwa kwa sadaka na majitoleo makubwa; kwa njia ya huduma, ubunifu na ushiriki wa raia wote. Ni wakati muafaka wa kutafakari na kupembua wajibu wa watu wa Mungu nchini Marekani na kizazi kijacho kitakachorithi matunda ya uhuru kwa siku za usoni. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walitangaza “declarat” kwamba binadamu anayo haki ya uhuru wa dini. Uhuru huo ndio huu, kwamba, kila binadamu lazima akingiwe na shurutisho la mtu mmoja mmoja, la makundi ya kijamii, au la mamlaka yoyote ya kibinadamu. Hivyo kwamba, katika mambo ya dini mtu yeyote asishurutishwe kutenda dhidi ya dhamiri yake, wala asizuiliwe, katika mipaka inayokubalika kutenda kulingana na dhamiri yake binafsi au hadharani, peke yake au katika muungano na wengine. Haki ya uhuru wa dini msingi wake ni utu na hadhi ya binadamu ijulikanayo kwa njia ya Neno la Mungu lililofunuliwa na ya akili. Haki hii ya binadamu ya uhuru wa dini yatakiwa kuzingatiwa katika sheria za jamii ili iwe haki ya raia. Rej. DH 2.

Kumbukizi ya Miaka 250 ya Uhuru wa Marekani
Kumbukizi ya Miaka 250 ya Uhuru wa Marekani   (ANSA)

Katika maadhimisho haya kutambua na kuenzi uhuru wa kidini ni kiini cha ahadi za Wamekani ya kulinda utu wa mtu binafsi, haki, amani na utulivu wa watu mbalimbali wanaoishi nchini Marekani. Uhuru wa kidini umeliwezesha Kanisa Katoliki nchini Marekani kuzamisha mizizi ya maisha na utume wake nchini Marekani, kwa kujikita katika Injili ya upendo, kwa kujitahidi kumwilisha ndani mwao Habari Njema ya Wokovu kila siku ya maisha yao: “Maana, upendo wa Kristo watubidisha; maana tumehukumu hivi, ya kwamba mmoja alikufa kwa ajili ya wote, basi walikufa wote; tena alikufa kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao.” 2Kor 5:14-15. Ni katika muktadha huu, Kanisa limekuwa mstari wa mbele kuchagia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Marekani katika sekta ya elimu, afya, huduma kwa maskini, ustawi na maendeleo ya jamii. Na kwamba, raia wa Marekani wanawajibika kikamilifu kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kama anavyosema Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa kwa Timotheo kwamba, ajitahidi kukabidhi mafundisho ya kweli za Kiinjili kwa watu wengine. “Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine.” 2Tim 2:2. Wakatoliki nchini Marekani wanahimizwa kutoa huduma kwa Taifa kama chachu ya utamaduni wa upendo inayosababisha mabadiliko ya ndani yenye nguvu, ili kuleta matokeo makubwa: “Akawaambia mfano mwingine; Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia.” Mt 13:33.

Kanisa limechangia sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi USA
Kanisa limechangia sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi USA   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika Barua yake anakazia: Thamani ya maisha, ukuu, utu, heshima na haki msingi za binadamu kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni Injili ya upendo wa Mungu kwa binadamu; Utu na heshima yake, mambo msingi yanayofumbatwa katika Injili. Katika ulimwengu mamboleo kuna mambo ambayo yanaendelea kutishia Injili ya uhai kwa kukumbatia utamaduni wa kifo. Haya ni matokeo ya watu kukengeuka pamoja na kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema. Kuna sera na mikakati mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inayotishia Injili ya uhai, ustawi na maendeleo ya wengi. Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Injili ya uhai anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete: kuheshimu, kulinda na kuhudumia Injili ya uhai, ili kukuza na kudumisha haki, maendeleo fungamani ya binadamu, uhuru wa kweli, amani na furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika sakafu ya maisha ya mwanadamu. Waamini wanapaswa kujipambanua kuwa ni watu wanaotetea Injili ya uhai kwa ajili ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika. Maskini na wanyonge katika jamii wanapaswa kuoneshwa huruma, upendo na mshikamano anasema Baba Mtakatifu Leo XIV.

Papa Leo XIV anawakumbuka na kuwaombea Wamarekani
Papa Leo XIV anawakumbuka na kuwaombea Wamarekani   (@Vatican Media)

Kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai kuna maanisha: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Huu ni mwaliko wa kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji ambao wamefika nchini Marekani wakitafuta uhuru, fursa na mahali pa kuhisi kuwa ni kwao wamesaidia kuunda utambulisho wa Taifa la Wamarekani. Kuwapokea kwa huruma na ukarimu ni kutambua heshima na hadhi anayostahili kila binadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika watu wa Mungu nchini Marekani kufanya kazi kwa umoja, ushirikiano na upendo, ili kuchochea ustawi na maendeleo ya mwanadamu yanayohitaji wajibu na uwajibikaji, ili kwa pamoja walimwengu waweze kukabiliana na changamoto mamboleo. Huu ni wakati kwa Wamarekani kujizatiti zaidi katika ujenzi wa uhuru, haki, fursa na demokrasia; wakiendeleza maono ya waliowatangulia, huku wakiendelea kujikita katika kuimarisha Jumuiya zao, kwa kuheshimu tofauti zao msingi na hivyo kufanya kazi ili kujenga umoja mkamilifu. Maadhimisho ya Miaka 250 ya Uhuru wa Marekani iwe ni fursa kwa Wamarekani kuendelea kujikita katika matumaini na umoja, ili kuelekea mapambazuko mapya. Baba Mtakatifu Leo XIV amewahakikishia Wamarekani wote sala na sadaka yake, ili kutekeleza katika maisha yao kanuni msingi zilizowaongoza waasisi wa Marekani walipokuwa wanaanzisha nchi yao. Mwishoni mwa Barua yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaweka Wamarekani wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mwombezi na Msimamizi wa Amerika ya Kaskazini, ili aendelee kuwalinda na kuwatunza Wamarekani wote wanaoishi nchini humo.

Miaka 250 ya Uhuru wa Marekani
06 Julai 2026, 14:01