Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Makanisa Ishara ya Amani, Umoja na Mshikamano!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, katika Sherehe ya Watakatifu Petro aliyeteuliwa na Kristo Yesu kuwa Mchungaji mkuu wa Kondoo wake na Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa; wote wawili ni Miamba wa imani ya Kanisa, Jumatatu tarehe 29 Juni 2026, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, akabariki Pallio Takatifu na kuwavisha Maaskofu wakuu wapya 35 walioteuliwa katika kipindi cha Mwaka 2025-2026. Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake ametaja sifa kuu na udhaifu wa watakatifu Petro na Paulo katika maisha na utume wa Kanisa, changamoto na mwaliko kwa wakristo kuwa ni wajenzi wa umoja wa Kanisa, huku upendo wa Mungu na jirani zao ukipewa kipaumbele cha kwanza, kama njia ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kwa Pallio Takatifu waamini pia wawe tayari kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu kuubeba Msalaba ambao mwili na ulimwengu “Caro et mundus” huwatwisha mebegani mwao wote watafutao haki na amani. Waamini wanahimizwa na Mama Kanisa kusadaka nguvu, muda, mateso na hata maisha yao, ili Injili iweze kuwafikia watu wote na ndani mwake waweze kupata amani na utulivu.
Baba Mtakatifu Leo XIV alitambua uwepo na ushiriki wa ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli ukiongozwa na Askofu mkuu Emmanuel Adamakis wa Jimbo kuu la Calcedonia. Ujumbe huu, Jumanne tarehe 30 Juni 2026 umekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV ambaye katika hotuba yake amegusia kuhusu: Hija yake ya Kitume nchini Uturuki kuanzia tarehe 27 hadi tarehe 30 Novemba 2025 iliyonogeshwa na kauli mbiu: “Bwana mmoja, Imani na Ubatizo Mmoja,” Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso Mkuu wa Nicea uliofanyika Asia Ndogo kunako Mwaka 325. Katika zama zenye vita, kinzani na migawanyiko inayozidi kukua na kupanuka: kitamaduni na kijamii, Wakristo waliopatanishwa wao kwa wao, wakaungana na kukiri imani yao moja kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, wanaitwa kuwa ni ishara ya kuaminika ya amani, kwa kuchangia juhudi kubwa za watu wa Mungu katika ujenzi wa amani.
Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli katika Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, katika barua yake kwa Papa Leo XIV amegusia kuhusu: hija ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Uturuki kuanzia tarehe 27 hadi tarehe 30 Novemba 2025 hija iliyonogeshwa na kauli mbiu: “Bwana mmoja, Imani na Ubatizo Mmoja.” Baba Mtakatifu Leo XIV alikazia pamoja na mambo mengine: Umuhimu wa uinjilishaji, Utangazaji na ushuhuda wa Injili yaani “Kerygma” kuhusu: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chemchemi ya wokovu. Utengano kati ya Wakristo ni kikwazo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo Yesu. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kutembea kwa pamoja katika hija ya maisha ya kiroho kuelekea Maadhimisho ya Mwaka wa Ukombozi, yaani miaka 2033 ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, huko mjini Yerusalemu. Hapa ni mahali ambapo Kristo Yesu aliadhimisha Karamu ya Mwisho, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, Siku ile ya Pentekoste, ili kujenga na kuimarisha umoja wa Wakristo huku akirejea kwenye kauli mbiu yake ya Kiaskofu: "In illo Uno Unum" yaani "Ingawa Sisi Wakristo ni Wengi, Katika Kristo Mmoja Sisi ni Wamoja.” Hili ni tukio la kihistoria, ambalo litawakusanya Wakristo kutoka sehemu mbalimbali za dunia.
Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema tarehe 7 Desemba 1965 Papa Paulo wa sita, alibahatika kukutana na kuzungumza na Patriaki Athenagoras I (1886-1972), baada ya miaka mingi ya kinzani, chuki na migawanyiko ya Kikanisa kuanzia mwaka 1054 hadi mwaka 1965. Viongozi wakuu wa Makanisa wakakutana kwa pamoja mjini Yerusalem, kwenye chemchemi ya Injili na kufungua ukurasa mpya wa Majadiliano ya Kiekumene, unaoendelea kufanyiwa kazi kwa zaidi ya miaka 60 kwa sasa, ili wote waweze kuwa ni wamoja chini ya Kristo Yesu mchungaji mkuu. Hii ni changamoto ya kupyaisha majadiliano ya kiekumene, ili kushuhudia umoja wa Kanisa unaoonekana, kama ushuhuda wa Injili ya upendo na mantiki ya Mwenyezi Mungu anayejifunua miongoni mwa wadogo. Makanisa haya mawili yanaendelea kufanya majadiliano ya kiekumene katika ukweli na uwazi ili kuganga na kuponya madonda ya utengano, ili hatimaye, kurejesha tena ushirika kamili na maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II na Patriaki Demetrios wanaendelea kubaki kuwa ni nguzo za majadiliano ya kiekumene.
Patriaki Bartolomeo wa kwanza anaendelea kusema, hivi karibuni Tume ya Pamoja ya Kiekumene kwa Ajili ya Majadiliano ya Kitaalimungu kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox “Joint International Commission for Theological Dialogue Between the Catholic Church and the Orthodox Church,” chombo rasmi kilichoanzishwa kunako mwaka 1980 kwa lengo la kutafuta umoja kamili na upatanisho wa kiimani kati ya Makanisa haya mawili, hivi karibuni wajumbe wake walikutana ili kupitia na kupyaisha rasimu ambayo inaendelea kujikita katika dhana ya “Papal infallibility.” Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Kwanza wa Vatican uliofanyika kunako mwaka 1870 walitamka kwamba, Baba Mtakatifu hulindwa na Roho Mtakatifu anapofundisha kwa uhakika masuala ya imani na maadili. Tume hii imechambua mwelekeo wake wa Kitaalimungu na kihistoria. Haya ni kati ya masuala yaliyopelekea Makanisa haya mawili kutengana, kumbe, waamini waendelee kumwomba Roho Mtakatifu ili awaongoze katika ukweli, ili hatimaye, Makanisa haya yaweze kuungana tena.
Patriaki Bartolomeo wa kwanza anamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kuhudhuria na hatimaye kushiriki katika,” Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso Mkuu wa Nicea uliofanyika Asia Ndogo kunako Mwaka 325, kielelezo cha utashi wa kutaka kujenga umoja kamili wa Kanisa, jambo ambalo Makanisa yanaendelea kusali na kulifanyia kazi. Katika Ulimwengu mamboleo ambao umegubikwa na vita, kinzani, ubaguzi, chuki dhidi ya wageni “Xenofobia,” kiu ya kutaka kutawala; uchumi unaoongozwa na kuratibiwa na faida kubwa pamoja na ukwapuaji wa rasilimali za dunia, walimwengu wanataka kuona Makanisa yakiwa ni vyombo na mashuhuda wa amani, umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu, sanjari na kuendelea kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Kumbe, kuna umuhimu kwa Makanisa kushirikiana na kushikamana “na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani.” Efe4:3. Ni mapendekezo ya Patriaki Bartolomeo wa kwanza kuanzisha Tume itakatoratibu Maadhimisho ya Sherehe za Makanisa, kama inavyosomeka katika Tamko lao la Pamoja lililotolewa Mwezi Novemba 2025 huko Phanar. Mwishoni, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli anatoa heri na baraka kwa watu wa Mungu walioko Jimbo kuu la Roma.
