Tafuta

Mama Kanisa tarehe 12 Julai 2026 anaadhimisha Dominika ya Utume wa Bahari, fursa makini kwa Familia ya Mungu sehemu mbalimbali za dunia: Kumwomba, kumtukuza, kumshukuru na kumwomba Mungu kwa zawadi ya Mabaharia Mama Kanisa tarehe 12 Julai 2026 anaadhimisha Dominika ya Utume wa Bahari, fursa makini kwa Familia ya Mungu sehemu mbalimbali za dunia: Kumwomba, kumtukuza, kumshukuru na kumwomba Mungu kwa zawadi ya Mabaharia  (AFP or licensors)

Ujumbe wa Dominika ya Utume wa Bahari 12 Julai 2026

Mama Kanisa tarehe 12 Julai 2026 anaadhimisha Dominika ya Utume wa Bahari: Siku ya:Kumwomba, kumtukuza, kumsifu na kumshukuru Mungu, kwa huduma na mchango mkubwa unaotolewa na mabaharia pamoja na wavuvi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.Ni siku maalum ya kutambua: mchango na sadaka ya watu hawa, ambao wakati mwingine, utu na heshima yao vinahatarishwa kutokana na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo kila siku.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Utume wa Bahari, “Opus Apostolatus Maris” unaojulikana na wengi kama “Stella Maris” ulianzishwa tarehe 4 Oktoba 1920 na waamini walei wanaoshiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu unaopata chimbuko lake kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo. Ni jukumu na wito wa waamini walei kuutafuta Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika kweli na uzima; ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani; huku wakiyashughulikia mambo ya dunia, na kuyaelekeza kadiri ya mpango wa Mungu. Waamini walei wanaitwa kuyatimiza majukumu yao wenyewe wakiongozwa na roho ya Kiinjili, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa imani, matumaini na mapendo thabiti! Ili kuonesha na kushuhudia ukaribu wa Kanisa kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao, Papa Pio XI tarehe 17 Aprili 1922 aliridhia kuanzishwa kwa Utume wa Bahari “Opus Apostolatus Maris.” Leo hii kuna jeshi kubwa la watu wanaojisadaka zaidi kuwadumia mabaharia na wavuvi katika bandari 300 kwa kutembelea meli zisizopungua 70,000 kwa mwaka. Mama Kanisa anawashukuru kwa dhati Mitume hawa wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. Wadau wa Utume wa Bahari wamekuwa ni mashuhuda na vyombo vya uinjilishaji wa kina kwa kuwafunulia watu wa Mungu, ile sura pendelevu ya Mama Kanisa: kwa kuonesha ukaribu wake kwa watu watakatifu wa Mungu, na hivyo kuwahamasisha kujisikia kuwa ni sehemu hai ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Takribani miaka 100 iliyopita, Dominika ya Utume wa Bahari imekuwa ni kipindi muafaka cha ujenzi wa misingi ya majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, kutokana na mwingiliano wa watu kutoka katika dini, tamaduni na Mataifa mbalimbali duniani.

Mabaharia na wavuvi wanachangia sana katika ustawi na mafao ya wengi
Mabaharia na wavuvi wanachangia sana katika ustawi na mafao ya wengi   (AFP or licensors)

Papa Pio XI alitamani sana kuona kwamba, Utume wa Bahari unaendelezwa kwenye Bahari na fukwe mbalimbali za dunia. Roho Mtakatifu, kwa maombezi ya Bikira Maria aendelee kupyaisha utume na huduma hii mintarafu mahitaji ya ulimwengu mamboleo! Kuna mabaharia ambao dhamiri zao zinahangaika sana na mara nyingi Mapadre wa maisha ya kiroho kwa mabaharia na wavuvi wamekuwa ni msaada mkubwa. Mabaharia ni watu wanaofanya kazi zao katika mazingira magumu na hatarishi; mara nyingi nje ya nchi, makazi na familia zao! Mapadre washauri wa kiroho katika muktadha kama huu, wanakuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya matumaini kwa mabaharia na wavuvi waliopondeka na kuvunjika moyo! Mapadre wanapaswa kuwa ni watu wenye huruma, wapole na wanyenyekevu wanapowahudumia mabaharia, wavuvui pamoja na familia zao.

Mama Kanisa anawapongeza Mabaharia na Wavuvi kwa mchango wao
Mama Kanisa anawapongeza Mabaharia na Wavuvi kwa mchango wao   (DAVID DEE DELGADO)

Mama Kanisa tarehe 12 Julai 2026 anaadhimisha Dominika ya Utume wa Bahari, fursa makini kwa Familia ya Mungu sehemu mbalimbali za dunia: Kumwomba, kumtukuza, kumsifu na kumshukuru Mungu, kwa huduma na mchango mkubwa unaotolewa na mabaharia pamoja na wavuvi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Ni siku maalum ya kutambua na kuthamini: mchango na sadaka ya watu hawa, ambao wakati mwingine, utu na heshima yao vinahatarishwa kutokana na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wakati wa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa jamii. Maadhimisho haya kwa Mwaka 2026 yananogeshwa na kauli mbiu: “Zaidi ya bidhaa na biashara: sura ya kibinadamu ya bahari” ni kauli mbiu inayokumbushia dhamana na wajibu mkubwa unaotekeleza na mabaharia na wavuvi sehemu mbalimbali za dunia. Mlango Bahari wa Hormuz (Strait of Hormuz) ni moja ya njia muhimu na nyeti zaidi za Bahari kwa uchumi na biashara ya kimataifa, kwani inakadiriwa kupitisha zaidi ya asilimia 20% ya mafuta na gesi asilia duniani. Kufungwa kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz kunachochea mfumuko wa bei na kupunguza ukuaji wa uchumi wa Dunia na katika hali mbaya zaidi kusababisha ongezeko la umaskini kwa watu milioni 32 na njaa kali kwa watu zaidi ya milioni 45. Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu linasema, hii inaonesha ni kwa jinsi gani binadamu kwa asilimia kubwa anategemea huduma ya bahari kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Katika Maadhimisho ya Utume wa Bahari, Mama Kanisa anawakumbuka na kuwaombea mabaharia na wavuvi walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wana utu, heshima na haki zao msingi wanavyotekeleza dhamana na utume wao katika mazingira yenye matumaini na hofu, mizigo na ustahimilifu, mahusiano na ndoto zinazostahili kuonekana, kuheshimiwa, na kuthaminiwa.

Dominika ya Utume wa Bahari: Mabaharia, Wavuvi na Familia zao
Dominika ya Utume wa Bahari: Mabaharia, Wavuvi na Familia zao   (@Vatican Media)

Bahari, ambayo imewaunganisha watu na Mataifa kwa muda mrefu, inazidi kuwa na mvutano na kinzani; ukosefu wa usalama, vita, na hofu. Mabaharia na wavuvi sio tu kwamba wanapitia katika mazingira hatari ya bahari na njia za maji lakini pia hivi karibuni wameathiriwa na migogoro ya silaha ambayo imesababisha kufungiwa kwao kwenye meli,  na haivyo kukumbana na: Uhaba wa chakula, na hata hofu ya maisha yao. Hii imeongeza hisia zao za upweke, kutengwa kwao na jamii kwa ujumla, kutengana kwao na wapendwa, na uchovu wao wa kihisia. Kwa kushangaza, hata katika enzi ya maendeleo makubwa ya mawasiliano ya kidijitali, mabaharia na wavuvi wengi bado wanaendelea kutengwa. Ule ukaribu wa kibinadamu unazidi kuwa nadra. Ni katika muktadha huu, mabaharia na wavuvi wanahitaji kuhisi uwepo, kutambua kwamba, wanakumbukwa, wanapendwa, wakakaribishwa na kusikilizwa.   Waraka wa kwanza wa Kitume wa Baba Mtakatifu Leo XIV: “Magnifica humanitas” yaani: “Ubinadamu wa ajabu" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde” unaonya kwamba, kamwe katika maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili unde, kamwe binadamu asigeuzwe kuwa kama “mashini, takwimu au biadhaa” bali utu, heshima na haki zake msingi zinapaswa kuzingatiwa. Mabaharia na wavuvi ni kielelezo cha ushuhuda wa watu kutoka katika Mataifa, tamaduni na imani bado wana uwezo wa kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu, mshikamano, kwa kuheshimiana pamoja kuishi kwa amani. Kimsingi Bahari inapaswa kuwa ni daraja la kuwakutanisha walimwengu; watu kutoka katika Mataifa, tamaduni, dini na chumi mbalimbali na hivyo kutoa fursa ya ushirikiano na mshikamano; amani na utulivu na hivyo Mabaharia hawawezi kusahaulika na wala kuelemewa na upweke hasi. Walimwengu wanakumbushwa kwamba, Bahari ni sehemu ya kazi ya uumbaji, ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu awajibike na kuitunza, kwani Bahari ni chemchemi ya lishe na ni nyumba ya wote. Inasikitisha kuona kwamba, leo hii bahari imegeuka kuwa ni shimo la takataka, ukwapuaji mkubwa wa rasilimali za dunia na matokeo yake ni uharibifu wa mazingira nyumba ya wote.

Siku ya Utume wa Bahari: Mabaharia, Wavuvi na Familia zao
Siku ya Utume wa Bahari: Mabaharia, Wavuvi na Familia zao   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, maendeleo ya binadamu hayana budi kuongozwa na kanuni ya: Utu, heshima, haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni katika muktadha huu, ulinzi na tunza ya mazingira haina budi kwenda sanjari na ulinzi na tunza ya binadamu na kwamba, huu ni wajibu msingi wa kimaadili na utu wema, ili kujenga na kudumisha moyo wa ushirikiano na mshikamano, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili kulinda mazingira, utu, na heshima ya binadamu. Kristo Yesu katika Maandiko Matakatifu anawaalika wafuasi wake kamwe wasiogope, akiwepo kati yao, dhoruba inatulizwa bila shaka. “Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado? Mk 4:40. Hata leo hii, Kristo Yesu bado anaendelea kuambatana na mabaharia na wavuvi, wanaokabiliana na hali ya kutokuwa na uhakika wa usalama wa maisha yao, watu wanaokabiliana na uchovu, hatari mbalimbali sanjari na kutengwa na familia zao. Kwa kuwa Kanisa limeitwa kuendeleza utume wa Kristo Yesu ulimwenguni, nalo haliwezi kukaa mbali na hali halisi ya maisha ya wafanyakazi wa sekta ya bahari. Bwana, aliyepanda kwenye mashua pamoja na wanafunzi wake, anaendelea kuwa karibu na wale wanaosafiri baharini na kwenye njia za maji za ndani katika nyakati hizi; na Kanisa limeitwa kudhihirisha ukaribu huo kupitia uwepo wake na huduma yake. Limeitwa kupanda kwenye mashua: kuandamana, kusikiliza, kufariji, kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu, na kuwa ishara dhahiri ya matumaini na mahali pa kuhisi nyumbani katikati ya dhoruba za maisha ya mwanadamu. Kupitia huduma za kiroho bandarini, huduma kwa watu wa baharini, na uwepo wa kibinadamu wa unyenyekevu unaozingatia mapokeo ya muda mrefu ya Utume wa Bahari kwamba, wahusika wote wanakumbukwa, wanathaminiwa na kamwe hawako peke yao. Na kwamba hii ni huduma inayowakumbatia na kuwaambata watu wote wa Mungu.

Mabaharia na wavuvi wanachangia sana katika kukuza uchumi wa dunia
Mabaharia na wavuvi wanachangia sana katika kukuza uchumi wa dunia

Mama Kanisa anawashukuru na kuwapongeza wote wanaotoa huduma ya: Sala, huduma ya kichungaji na Sakramenti kwa mabaharia Wakatoliki ambao kimsingi ni sehemu kubwa ya wafanyakazi na maofisa wanaotua nanga zao za matumaini wanapofika bandarini, wakiwa mbali na nyumba, familia; na mahali pao pa kawaida pa Ibada. Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu linawashukuru mabaharia, wavuvi na wafanyakazi wote wa sekta ya bahari na familia zao sehemu mbalimbali za dunia, kwa kazi na utu wao na kwamba, dhabihu na sadaka zao zinategemeza biashara ya kimataifa, usalama na uhakika wa chakula;  ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baraza linawashukuru wahudumu wa maisha yao kwa uaminifu wao, kwa kujenga na kudumisha urafiki; kwa sala, usikilizaji na msaada wa hali na mali bandarini na katika meli sehemu mbalimbali za dunia. Dominika ya Utume wa Bahari ipyaishe ndani ya waamini wote azimio la dhati kabisa la kuwa karibu, kwa kushikamana, kwa kujali kazi ya uumbaji pamoja na watu wote wanaofanya kazi Baharini na kwenye njia za maji za ndani. Baraza linawakabidhi wote hawa mikononi mwa Bikira Maria, Nyota ya Bahari, kwa kuomba usalama, heshima, amani na matumaini kwa wote wanaosafiri na kufanya kazi majini.

Utume wa Bahari 2026
09 Julai 2026, 15:18