Ujumbe wa Papa Leo XIV Kwa Siku ya 6 ya Bibi, Babu na Wazee Kwa Mwaka 2026
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani ni matunda yanayobubujika kutoka katika Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” uliozinduliwa rasmi tarehe 19 Machi 2021 na ukahitimishwa wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kumi ya Familia Duniani hapo tarehe 26 Juni, 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu.” Siku ya Mababu, Mabibi na Wazee ni muda wa kuserebuka, kutoa faraja na kuonesha upendo kwa wazee, ili kujenga na kudumisha: Umoja, udugu wa kibinadamu, upendo na faraja tunu msingi katika maisha ya kijamii. Ni muda kwa waamini kujifunza sanaa ya kupenda na kupendwa na katika muktadha huu, wazee wanaweza kuwa magwiji kwa vijana wa kizazi kipya! Ndoto, kumbukumbu na sala ni kielelezo cha uwepo endelevu na angavu wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake. Wazee wawe ni wadau katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji katika maisha na utume wa Kanisa. Wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo mizizi ya jamii; mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ni imani na mang’amuzi ya maisha. Inapendeza ikiwa kama wazee watakutana na wajukuu zao, ili kuendeleza amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha yao! Inasikitisha kuona kwamba, mara nyingi wazee wanasahauliwa sana katika jamii na kuonekana kama mzigo mzito wa kutua. Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yatakuwa yanakaribiana sana na Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria. Kila mwaka Kanisa Katoliki Kiulimwengu huadhimisha siku ya Babu, Bibi na Wazee Ulimwenguni kila ifikapo Dominika ya Nne ya Mwezi Julai. Siku hii ilianzishwa na Papa Francisko kunako mwaka 2021 kwa lengo la kutambua mchango mkubwa wa kizazi cha wazee katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake.
Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria, inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Julai. Hii ndiyo familia ambamo Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa amechota fadhila mbalimbali zilizomwezesha kupata upendeleo wa pekee mbele ya Mwenyezi Mungu. Kumbe, Ibada na heshima kwa watakatifu Joakim na Anna ni mwendelezo wa Ibada kwa Bikira Maria na hatimaye, Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Ni nafasi muafaka ya kutafakari changamoto, fursa na matatizo yaliyopo na kuendelea kuyafanyia kazi na hatimaye, kuyapatia majibu muafaka kwa mwanga wa tunu msingi za Kiinjili na kiutu. Changamoto ya kwanza ni kuubali na kuupokea Wosia ambao umesheheni maneno ya ujasiri, chachu ya mabadiliko na upyaisho wa maisha na utume wa ndoa na familia sanjari na mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi na watu wa Mungu. Kimsingi, familia zinahitaji sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, zitakazowawezesha wanandoa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia katika ujumla wake. Familia inapaswa kusimikwa katika upendo wenye huruma, kwa kutambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, linayotangaza na kushuhudia uwepo mwanana wa Mwana wa Mungu. Katika shida na magumu, familia zisaidiwe kwa hali na mali, ili kuweza kupita vipindi hivi vigumu kwa kusindikizwa na upendo wenye huruma. Familia zinazoogelea kwenye shida na ugumu wa maisha zisikilizwe na zisaidiwe. Wazazi na walezi wanayo dhamana kubwa ya kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha misingi ya imani kama sehemu ya mchakato wa ukomavu wa imani miongoni mwa watoto wao. Wazazi na walezi warithishe imani hii kwa njia ya maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu; kwa kutambua na kuenzi kweli msingi za maisha kadiri ya upendo na mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu; watoto wasaidiwe kupata mwanga na ufunuo wa Mungu katika hija ya maisha yao.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa Maadhimisho ya Siku ya Sita ya Babu, Bibi na Wazee duniani tarehe 26 Julai 2026 unanogeshwa na kaulimbiu: "Sitakusahau kamwe." Rej. Isa 49:15. Hii ni siku maalum ya kuwakumbuka, kuwashukuru na kuwapongeza wazee kwa hekima na upendo wao, mwaliko kwa jamii kushikamana kwa dhati na wazee. Mwenyezi Mungu anaahidi kwamba, kamwe hatamsahau mja wake kwani amechora sura yake kwenye kiganja cha mikono yake na kwamba, upendo wake ni mkuu kuliko upendo kwa mama kwa mtoto wake. Mwenyezi Mungu anazungumza na waja wake kama rafiki, na kila mtu binafsi na kwa watu wote katika ujumla wao na hata leo hii maneno yake yanawahusu hata watu katika ulimwengu mamboleo: "Sitakusahau kamwe" yakisemwa moja kwa moja kwa kila mtu. Haya ni maneno yanayowajaza watu faraja na matumaini. Ni jibu kwa hisia chungu inayousumbua moyo: "Bwana ameniacha; Bwana wangu amenisahau" (Isa 49:14). Mara ngapi katika Maandiko Matakatifu, hasa katika Zaburi, sala hutokana na kukata tamaa kwa wale wanaohisi kuwa maisha yao hayana thamani kwa mtu yeyote na kwamba wanapuuzwa! Kwa bahati mbaya, hisia chungu ya kusahaulika inashikiriwa na watu wengi, na miongoni mwao wamo wazee wengi. Upendo wa Mungu, ambao humkumbuka kila mtu, unajitokeza kama tendo la haki na jibu kwa hali ya kutoonekana au kusahaulika ambamo maisha ya binadamu mara nyingi hupotea. Maisha ya wazee wengi, hasa, yanaonekana kufunikwa na pazia linaloficha sura zao na kuwatumbukiza katika kusahaulika. Hivi ndivyo inavyotokea katika nyumba ambazo upweke hutawala, na pia katika vituo vya kutunzia wazee ambapo upekee wa kila mtu unaweza kupoteza thamani yake na kubaki kuwa namba ya kitanda au ugonjwa tu.
Maadhimisho ya Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani ni fursa ya kugundua upya kwamba Kanisa limeitwa kuwa Mama kwa wote na kwamba, katika umri wowote, inawezekana kujitambua kama watoto wa Mungu. Hivyo basi, siku hii na iwe chachu kwa kila mtu hasa kwa vijana wa kizazi kipya kufufua desturi njema ya kuwatembelea babu na bibi zao, wazee wa familia, na hata wale wasio na mtu wa kuwatembelea. Kupitia ujumbe huu na uwepo wao Baba Mtakatifu Leo XIV anawaomba vijana wa kizazi kipya kuwafikishia ukaribu na upendo wake kwani kwa njia hii, wazee wataweza kukutana na upendo na huruma ya Mungu. "Katika zama zinazothamini kasi na kutengana, mwanadamu bado ana kiu ya kupata uangalizi na kuthaminiwa kupitia fikra makini, maneno ya fadhili, na mikono yenye uwezo wa kuonesha upendo na huruma. Utamaduni wa kidijitali huongeza mawasiliano na kutoa fursa mpya za kushirikiana; hata hivyo, moyo wa mwanadamu bado unahitaji lisiloweza kuondolewa la kuwa na ukaribu wa kweli" Rej.Waraka wa Kitume, Magnifica humanitas, 239. Kanisa linaelewa mateso ya watoto wake walio wazee; linajua vyema kwamba mara nyingi hutazamwa kwa mitazamo potofu na kuhesabiwa kuwa mzigo; linatambua kuwa uchumi unaolenga faida hudhoofisha uhusiano wa kifamilia; linajua kuwa wazee wengi huachwa nyuma na watoto wanaolazimika kuhama au, katika baadhi ya matukio, kwenda vitani. Kwa sababu hizi zote, Kanisa linatangaza kwa furaha ahadi ya Bwana: "Lakini sitakusahau kamwe!"
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, ni furaha, katika umri wowote lakini zaidi katika uzee kwamba, wao wanakuwa ni wapokeaji wa upendo usiochujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu anawataza daima, hata wakati ambapo kuonaonekana kuwapo na giza, kwani Mungu ni Baba na Mama ya waja wake, kwani hata katika uzee, bado binadamu ataendelea kuwa ni mwana mpendwa wa Mungu, changamoto na mwaliko ni kurejea tena mikononi mwa Mwenyezi Mungu ambaye upendo wake ni wa kibaba na kimama, na kwamba, unasalia kuwa na thamani kubwa katika umri wowote. Kwa watu wengi, ugunduzi wa huruma na upole wa Mungu hutokea katika kipindi cha maisha yao, wakati mwingine hata katika hatua zake za mwisho. Hakika, tofauti na hapo awali, linazidi kuwa jambo la kawaida kufikia uzee bila kuwa na uzoefu wa kweli wa imani. Katika hali kama hizo, uzee ukianzia na maswali yanayojitokeza kwa haraka zaidi katika kipindi hiki cha maisha unaweza kuwa ni muda muafaka wa kuanza au kupyaisha maisha ya kiroho. Katika safari hii mpya, mtu anaweza kutambua kwamba Mungu, kama asemavyo Mtakatifu Augustino, “ni Mama kwa sababu anajali, kwa sababu analisha, kwa sababu ananyonyesha, kwa sababu analinda” (Ufafanuzi wa Zaburi ya 27, II, 18). Hii ni hali ya kutambua inayomsaidia mwanadamu kutoona aibu kwa udhaifu unaojitokeza, na pia kuelewa kwamba siku zote wanahitajiana na wanahitaji uangalifu na utunzaji. Kwa Mungu, ambaye huwakaribia na ambaye binadamu anajifunza kumtambua katika upole wake, sasa anaweza kumgeukia kwa imani ya mtoto katika sala. Kamwe si kuchelewa mno kuanza kumgeukia Mwenyezi Mungu. Hilo linaweza kuwa zawadi kuu kwa kila mtu.
Hayati Baba Mtakatifu Francisko anawataja wazee kama watu wapya kwa kuwa idadi ya watu wenye umri mkubwa haijawahi kuwa kubwa hivi katika historia ya mwanadamu. Kwa hiyo, ni muhimu zaidi kuliko wakati wowote kutafakari pamoja na wazee, yaani “watu wapya,” kuhusu wito wao wakati udhaifu ambao ni mwenza wa mwanadamu tangu kuzaliwa pale unapoonekana kutawala. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaambia wazee kwamba, “wasiogope udhaifu wanao ubeba ndani mwao, kwani huu ni uwezo mpya ambao huangazia hatua nyingine za maisha. Hakika, binadamu anapokiri udhaifu wake, mioyo yao hufunguka kusaidiana na kumwomba Mwenyezi Mungu anayeweza kutoa kile ambacho nguvu yoyote ya kibinadamu haiwezi kuhakikisha: upatanisho wa kina wa mioyo na, pamoja na hayo, amani ya kweli.” Hivi ndivyo binadamu wanaweza kuishi uzee wao kama Wakristo: wakiwa “wadhaifu” lakini wakati huo huo “wanaitwa.” Kwa kweli, binadamu anaweza kuzaliwa upya katika uzee (taz. Yn 3:4-6) na kutangaza, pamoja na Nabii Isaya: “Kwa kutubu na kutulia mtaokolewa; katika utulivu na tumaini itakuwa nguvu yenu” (Isa 30:15). Nguvu hii inaweza kuwa mwaliko wa kutotumia njia za kiburi na mamlaka ili kuhakikisha kuishi pamoja kwa wanadamu, bali kutumia njia za upatanisho na amani ya kweli. Katika wakati huu, ambao umeathiriwa sana na vurugu za vita na machafuko ya kijamii, watu wengi wanajiuliza ni aina gani ya ulimwengu ambao wajukuu zao watakulia ndani yake. Baba Mtakatifu Leo XIV anawasihi wazee kuungana pamoja naye katika sala ya dhati ili amani iweze kutawala duniani kote. Anawashukuru kwa kumuunga mkono katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro hasa wanaposali Rozari Takatifu Rozari muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; maisha na utume wa Kristo Yesu kwa njia ya Bikira Maria. Baba Mtakatifu Leo XIV kutoka ndani kabisa ya “sakafu” ya moyo wake anapenda kuwarejeshea tena shukrani na kuwaachia sala hii: “Bwana na atufanye upya daima katika imani, tumaini na upendo Yeye ambaye hatusahau kamwe!
