Papa Leo XIV,vijana Iraq:Gundueni moyo wa Kristo&msiogope kujenga maisha yenu juu yake
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kwa ajili ya vijana waliokusanyika huko Ankawa, katika Jimbo Kuu la Upatriaki wa Erbil, nchini Iraq katika Mkutano wao wa kila mwaka kuanzia tarehe 8 hadi 11 Julai 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV aliwatumia ujumbe wake kwa njia ya video akiwahimiza kuwa "wamisionari wa matumani na nuru ya Kristo katika nchi inayoendelea kushuhudia matokeo ya vita na ukosefu wa utulivu." Kwa njia hiyo Papa akiwaelekea vijana hao, wanaoongozwa kauli mbiu ya mwaka 2026: “Utume," alionesha furaha yake kwa washiriki wote kwamba “Mmetoka sehemu mbalimbali za Iraq kukusanyika katika mazingira ya imani na ushirika, na ninaomba kwamba itakuwa fursa kwenu nyote kukua katika urafiki na Yesu na kati yenu. Ujana ni wakati wa maisha unaooneshwa na hamu ya kufanya mambo makubwa na kuleta mabadiliko duniani. Katika suala hilo, ninafurahi kujua kwamba mada iliyochaguliwa kwa mkutano wenu mwaka huu ni utume. Kanisa lina utume muhimu wa kutumikia ulimwengu kwa kushiriki nuru ya Kristo (taz. Yh 8:12) na kuwaleta wanaume na wanawake katika ushirika na Mungu. Mnashiriki katika utume huu, na ninawategemea ninyi kusaidia kuunda Kanisa na ulimwengu katika miaka ijayo. Kama nilivyosema hapo awali, vijana si kwamba ni mustakabali wa Kanisa tu, bali pia ni wa sasa.”
"Siyo rahisi kuwa mwanga wa Ulimwengu"
Papa Leo XIV aliendelea kusema kuwa “Si rahisi kila wakati kuwa nuru duniani (taz. Mt 5:13). Hakika, kwa sasa, mmeitwa kuangaza nuru hii katika hali ambayo mara nyingi imekuwa ikioneshwa na vita na ukosefu wa utulivu. Bwana ameweka imani kubwa kwenu katika kuwapatia utume huu, na mimi pia nina imani kubwa kwenu nyote. Lazima muwe nuru ya Kristo katikati ya giza ambalo wakati mwingine linaweza kuonekana kuwa kubwa. Msiogope! Na msifikiri kwamba mko peke yenu katika utume huu,” Papa Leo XIV anawahakikisha ukaribu wake: “Mimi niko pamoja nanyi; Kanisa liko pamoja nanyi. Wekeni imani yenu kwa Yesu; msikilize kwa maombi na kupitia mwongozo wa wengine, na mruhusu awaongoze.”
"Mungu yuko pamoja nasi ingawa hatuwezi kumwona"
Baba Mtakatifu aliwapatia njia tatu za kufuata kwamba “Nuru ni muhimu kwa maisha kwa njia kadhaa, na ningependa kutaja tatu ambazo zinaweza kuwasaidia katika utume huu. Kwanza, nuru ni muhimu kwa kuona, ambayo inatukumbusha zawadi ya imani. Imani katika Mungu si njia ya kukabiliana na magumu ya maisha. Badala yake, ni kutambua uhalisia na kuishi katika ukweli, kujifunza kuona ulimwengu, wengine na sisi wenyewe kama Mungu anavyotuona. Inahitaji kusafiri maishani huku mioyo yetu na macho yetu yakitazama nchi yetu ya kweli (taz. Waeb 11:14), tukijua kwamba Mungu yuko pamoja nasi ingawa hatuwezi kumwona. Jinsi mnavyoishi lazima pia mshuhudie imani yenu, ili wengine waweze kuona ndani yenu ukweli na maana ambayo wao pia wanatamani, na hivyo kushiriki katika nuru ile ile.”
"Gundueni moyo wa Kristo na msiogope kujenga maisha yenu juu yake"
Papa aliendelea kufafanua kuwa mantiki ya pili ya nuru ni kwamba, "nuru hutoa joto, ambalo linaashiria upendo. Ili kuwa nuru kwa ulimwengu, lazima kwanza tushiriki katika nuru na maisha ya Kristo. Ili kushiriki katika utume, lazima kwanza tugundue uhusiano hai na Mungu. Lazima tumjue. Kwa kujifungulia upendo wa Mungu unaobadilisha, tunapokea neema muhimu ili kumfuata Yesu na kukumbatia maisha anayotuita tuyaongoze. Hii ndiyo maana ni muhimu sana kutumia muda kila siku katika maombi, na kumkaribia Mungu kupitia sakramenti, hasa Kitubio na Ekaristi,” Kwa kuongeza ushauri Baba Mtakatifu alisema “ Ishini mioyo yenu katika msingi imara wa upendo wa Mungu kwenu; gundueni moyo wa Kristo, na msiogope kujenga maisha yenu juu yake (taz. 1 Yh 4:16). Kwa kufanya hivyo, si kwamba mtapata utimilifu mnaoutamani tu, bali pia mtaweza kushiriki joto la upendo wa Mungu na nguvu ya upatanisho wa neema yake na wale walio karibu nanyi.”
"Fadhila ya tumaini hututia moyo kutazama mbinguni"
Ushauri wa Tatu, wa Papa Leo XIV alisema “hatimaye, nuru ni muhimu kwa ukuaji na maisha mapya, na ni taswira ya tumaini. Mkiwa na mizizi katika upendo, mmeitwa hasa kuwa wapatanishi, kuwaunganisha wale walio karibu nanyi, na kuwatia wengine tumaini la mustakabali unaooneshwa na amani ya kudumu. Huenda msiweze kudhibiti hali yenu au changamoto mtakazoombwa kukabiliana nazo, lakini mnaweza kuchagua kuruhusu amani ya Kristo itawale mioyoni mwenu (taz. Kol 3:15). Fadhila ya tumaini hututia moyo kutazama mbinguni. Hii haimaanishi kusahau kuhusu ulimwengu, bali kuwa na ujasiri wa kushiriki nao amani na uzima unaotoka kwa Kristo, ambaye nuru yake inamulika Yerusalemu Mpya (taz. Ufu 21:23).
"Msitilie shaka wema wa Mungu"
“Wapendwa vijana, msitilie shaka wema wa Mungu, na msiogope mpango alio nao Bwana kwa kila mmoja wenu maishani,” Papa aliwasihi. Kwa kufafanua alisema “Nabii Yeremia pia alikabiliwa na nyakati ngumu, na anashuhudia kwamba mipango ya Bwana ni “kwa ajili ya ustawi wenu na si kwa ajili ya madhara, kuwapa mustakabali wenye matumaini” (Yer 29:11). Nikiwakabidhi kila mmoja wenu ulinzi na mwongozo wa Mama Maria, Mama wa Kanisa, ninaomba kwamba katika siku hizi za ufufuko wa kiroho, mpate kugundua ndani yake mfano halisi wa maisha yaliyotolewa kikamilifu kwa neema ya Mungu.” Baba Mtakatifu Leo XIV anahitimisha ujumbe huo kwa kuwabariki: “Na Mwenyezi Mungu awabariki nyote, Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu. Amina.”
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.
