Ajali ya Bus Hungaria Yauwa Mahujaji 12 Kutoka Poland, 10 Wamejeruhiwa
Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.
Bus lililokuwa limebeba mahujai 59 wa mji wa Podkarpazia nchini Poland waliokuwa wanarejea kutoka katika hija ya maisha ya kiroho kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Medjugorje yaani “Bikira Maria Mama wa Amani” huko Bosnia-Erzegovina, Dominika tarehe 16 Agosti 2026 limepinduka na hivyo kusababisha watu 12 kupoteza maisha na wengine 10 kupata majeraha makubwa. Ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia tarehe 16 Agosti 2026 kwenye barabara kuu ya M3, karibu na mji wa Mezőkeresztes, takriban kilomita 140 Mashariki mwa mji mkuu wa Hungaria, Budapest. Uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha ajali hiyo. Kwa mujibu wa taarifa za awali, basi hilo lililokuwa na watu 59 lilitoka nje ya barabara na kuingia mtaroni kisha kupinduka. Inawezekana dereva alisinzia akiwa anaendesha.
Baba Mtakatifu Leo XIV amepokea taarifa hizi kwa majonzi na masikitiko makubwa. Katika salam zake za rambirambi zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Adam Szal wa Jimbo kuu la Przemyśl na Askofu Jan Wątroba wa Jimbo la Rzeszó, Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kiroho kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na ajali hii mbaya na ya kusikitisha. Na anapenda kuwakabidhi marehemu wote kwa huruma na rehema za Mwenyezi Mungu na anamwomba Mwenyezi Mungu awajalie faraja, amani na kitulizo familia zote zilizokumbwa na ajali hii.
Hatimaye, Baba Mtakatifu Leo XIV amewakabidhi wote waliopatwa na ajali hii chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Częstochowa. Mwishoni Baba Mtakatifu Leo XIV amewapatia baraka zake za kitume ikiwa ni ishara ya ukaribu wa kibaba na tumaini la Kikristo katika maisha na uzima wa milele. Mabaraza ya Maaskofu wa Poland na Hungaria pia yametoa rambirambi zao na kuahidi sala kwa ajili ya wale wote waliofikwa na ajali hii mbaya.
