Hija ya Kichungaji ya Papa Leo XIV Assisi: Ibada ya Misa Na Mahojiano Na Vijana
Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.
Katika Maadhimisho wa Sikukuu ya Kung’ara Bwana, Alhamisi tarehe 6 Agosti 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV amefanya hija ya kichungaji, Mjini Assisi kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Malkia wa Malaika “Basilica Papale di Santa Maria Degli Angeli in Porziuncola,” ili: Kukutana na vijana; akajibu maswali yao ya ndani; akaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Vijana wa Kifranciskani wenye umri kati ya miaka 18 hadi 33. Itakumbukwa kwamba, Mkutano huu ulizinduliwa tarehe 3 Agosti 2026 na unafikia kilele chake kwenye Sikukuu ya Kung’ara Bwana, tarehe 6 Agosti 2026. Tukio hili ni sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipofariki dunia na unapania kuwasaidia vijana wa kizazi kipya kugundua amana na utajiri wa Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa njia ya mikutano, sala na kusherehea uzuri na utakatifu wa maisha. Mkutano huu unanogeshwa na kauli mbiu “Go! Franciscan Youth Meeting.” Hii imekuwa ni fursa kwa vijana kutafakari udugu wa kibinadamu na changamoto zake; safari ya ukuaji wa mtu binafsi na kwamba, vijana wameonesha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Sikukuu ya Kung’ara sura Bwana wetu Yesu Kristo ni tukio ambalo linaelezwa na Injili tatu: Marko, Mathayo na Luka na linaadhimishwa tarehe 6 Agosti ya kila mwaka. Kristo Yesu akiwa ameambatana na Mitume wake: Petro, Yakobo na Yohane akapanda nao mlimami kusali. Akiwa anasali sura yake ikageuka, ikang’ara na mavazi yake yakawa meupe wanatokea Musa na Eliya. Hawa ni watu muhimu sana katika historia ya Wayahudi. Musa ndiye anayewakilisha Torati, yaani Sheria na Taratibu zinazoongoza maisha yote ya Wayahudi. Eliya yeye anawakilisha Manabii. Zaidi ya hapo uwepo wa pamoja Musa na Eliya, yaani Torati na Manabii, katika lugha ya kibiblia maana yake ni ufunuo wa Maandiko Matakatifu. Torati na Manabii ni neno lililotumika kumaanisha Maandiko Matakatifu katika Agano la Kale. Mwisho wa tukio hilo ni kwamba linashuka wingu na ndani ya wingu hilo inasikika sauti ikisema: “Huyu ni mwanangu mpendwa msikieni Yeye.” Wingu na sauti hii ni ile ile iliyosikika siku ya Ubatizo wa Yesu mtoni Yordani. Wingu ni alama ya uwepo wa Mungu kumbe, sauti hiyo inayosikika inaonekana moja kwa moja kuwa ni ushuhuda wa sauti ya Mungu: “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye.” Mk 9:7: Haya pia ni maandalizi ya ufunuo wa Siku ya Mwisho, atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake amesema, Mji wa Assisi ni mahali ambapo palifanyika mageuzi ya maisha ya watakatifu Francisko wa Assisi na Clara, wakasikiliza mwaliko wa Kristo Yesu na hatimaye, wakamfuasa, huu ni mwaliko kwa waamini kujenga utamaduni wa kusikiliza, kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu, ili hatimaye, kufuata nyayo za Kristo Yesu, kwa kushinda kishawishi cha kukata na kukatishwa tamaa; kuondoa hofu na wasiwasi kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu. Wafuasi wa Kristo Yesu wanaitwa kujadiliana naye mintarafu historia yake, tayari kuanza kuandika ukurasa mpya wa historia ya maisha yao. Kristo Yesu alipokuwa anasali, sura yake iligeuka na kwamba, vijana wa kizazi kipya katika mkutano huu, wamepata fursa ya wao kukutana, kuzungumza na kushirikishana tajiriba ya maisha, changamoto na mwaliko wa kumsikiliza Kristo Yesu na kufanya maamuzi ya busara mintarafu tasaufi ya Kifranciskani ambayo ndani mwake wao wanachota amana na utajiri mkubwa, tayari kujenga na kudumisha uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu, majirani zao pamoja na viumbe wote.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, “kila kizazi hurithi jukumu la kuunda wakati wake: kuliruhusu historia kukomaa na kuwa hali ambapo utu wa kila mtu unalindwa, haki inahimizwa, na udugu unawezekana. Hata hivyo, kila zama hukabiliwa na hatari ya kujenga ulimwengu usio na utu na uliojaa ukosefu wa haki zaidi. Popote ambapo wanadamu wako katika hatari ya kupoteza sura yao halisi, sisi Wakristo huinua macho yetu kwa Mungu aliyefanyika mwili, tukijua kwamba “ni katika fumbo la Neno aliyefanyika mwili pekee ndipo fumbo la mwanadamu hupata mwanga wa kweli.” Utu huu mtukufu ndani ya Yesu Kristo unakuwa Njia, Kweli, na Uzima, ukifungua njia kwa kila mmoja wetu kukua kuelekea utimilifu.” Rej. Waraka wa kwanza wa Kitume wa Baba Mtakatifu Leo XIV: “Magnifica humanitas” yaani: “Utu wa kupendeza" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde” N, 1.
Hata baada ya kutimia takribani miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Francisko wa Assisi, bado Mji wa Assisi unaendelea kuwa ni kitovu cha mababadiliko, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Clara aliyetaka kufuata nyayo za Mtakatifu Francisko, akijitahhidi kuishi kama mwanamke akiwa huru kama walivyokuwa wafuasi wa Mtakatifu Francisko, huo ukawa ni mwanzo wa nguvu ya Kikristo iliyotenda kazi ndani mwao. Vijana wa kizazi kipya wanajitahidi kuwatafuta watakatifu wapya, mwaliko kwa vijana hawa ni kuthubu kuamini katika Injili, ili waweze kuwa binadamu huru, kwa kuambata na kukumbatia ufukara wa Kiinjili, tayari kutumwa sehemu mbalimbali za dunia kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, tayari kugusa Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu kwa watu wanaoteseka kwa matatizo na changamoto mbalimbali za maisha na hivyo kuingia kwenye uhalisia wa maisha ya watu na hivyo kujua nguvu ya upole. Rej. Evangelii gaudium, 270. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika vijana wa kizazi kipya kuachana na utamaduni wa “kujimwambafai”, kwa kubomoa kuta za utengano, kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya kifamilia na tamaduni njema. Ni mwaliko wa kuondokana na hofu na woga usiokuwa na msingi, ghasia na matumizi ya nguvu, tayari kujenga utamaduni unaothamini wengine na kuwahudumia; kwa kujikita katika utamaduni wa upendo, ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo na wajenzi wa haki na amani; kwa kukumbatia na kuambata Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kujenga na kudumisha utu wa binadamu katika masomo, taaluma, kazi, urafiki wa kijamii, upendo na katika maisha ya sala.
Ee Bwana unifanye kuwa chombo cha amani. Baba Mtakatifu Leo XIV mwishoni mwa mahubiri yake, amewakabidhi vijana wa kizazi kipya amana na utajiri unaobubujika kutoka kwenye Sala ya Mtakatifu Francisko wa Assisi ili wakatende hivyo hivyo katika maeneo yao:
Palipo chuki nieneze upendo
Palipo na mashaka pawe na imani.
Palipo na tumaini pawe na matumaini.
Palipo na giza pawe na mwanga.
Palipo na huzuni pawe na furaha.
Ee Bwana Mungu, unijalie;
Nisitafute kufarijiwa bali kufariji
Nisitafute kupendwa bali kupenda.
Kwani ni katika kutoa ndipo tunapopokea
Ni kwa kusamehe ndipo tunaposamehewa.
Na ni kwa kufa ndipo tunazaliwa katika uzima wa milele.
Baba Mtakatifu Leo XIV anawatuma vijana wa kizazi kipya kutenda yafuatayo:
Bwana, nijaalie nisitafute sana
kufarijiwa bali kufariji,
kueleweka bali kuelewa,
kupendwa bali kupenda.
Maana kwa kutoa ndipo tunapopokea,
kwa kujisahau ndipo tunapojigundua,
kwa kusamehe ndipo tunaposamehewa,
kwa kufa ndipo tunapofufukia uzima wa milele.
Baba Mtakatifu Leo XIV amewaambia vijana kwamba, maadhimisho haya mjini Assisi yanabaki na kuhifadhiwa katika kumbukumbu za maisha yao wanaporejea tena katika maeneo yao. Kumbukumbu hii iwe ni kama vile kushuka kwa Mtakatifu Petro, Yakobo, na Yohane kutoka Mlimani juu wakati wa kung’ara kwa Kristo Yesu, tayari kukabiliana na changamoto za nyakati zijazo, tayari kujitoa kwa Kristo Yesu bila ya kujibakiza na kwamba, Kristo Yesu ana waamini, anawategemea na anaendelea kubaki pamoja nao katika hija ya maisha yao.
Kijana Francesco Varone, kwa niaba ya vijana wenzake wote kutoka sehemu mbalimbali za Bara la Ulaya, amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Leo XIV, katika nafsi ya Khalifa wa Mtakatifu Petro anayetembea na watu wa mungu katika hija ya maisha yao, huku wakishirikishana magumu ya maisha, changamoto sanjari na Injili ya matumaini na upendo. Katika mkutano huu, vijana wamemjifunza kwa dhati Mtakatifu Francisko wa Assisi na kwamba, yote aliyotenda yalikuwa ni majibu kwa upendo wa Mungu. Vijana wanasema, wanahitaji mashuhuda wa kweli, wenye uwezo wa kuwaelekeza kwa Krksto Yesu kupitia maisha yao kwa njia ya ushuhuda mwenye mvuto na mashiko. Baba Mtakatifu amewatia moyo ili kamwe wasiogope kuchagua yaliyo mema na kuyafuata, waendelee kuamini kwamba, Injili bado ina uwezo wa kuleta toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.
Vijana wanaendelea kusema, “Baba Mtakatifu, kauli mbiu inayofafanua maisha na utume wako imegusa sana mioyo yetu katika siku hizi za hivi karibuni: katika Yeye mmoja, sisi ni wamoja. Sisi vijana tunafahamu vyema changamoto ya utengano na hofu ya upweke hasi katika maisha. Unatukumbusha kuwa umoja wetu hautokani na mambo tunayofanana, bali unatokana na Nafsi moja: Yesu Kristo. Ndani Yake, hakuna aliye mgeni; hakuna anayetengwa. Kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi, hii ndiyo ilikuwa kiini cha ujenzi wa udugu wa kibinadamu: kuhisi kuwa ndugu wa kweli si kwa bahati mbaya, bali kwa sababu sisi ni watoto wa Baba mmoja. Hili ndilo wanalolibeba kutoka Assisi: hapa, tumeshuhudia wenyewe kuwa Kristo Yesu anatufungamanisha pamoja na kwamba hatuko peke yetu. Kukusanyika karibu na Khalifa wa Mtakatifu Petro kumetufanya tulielewe hili waziwazi.” Vijana wameahidi kuendelea kusali na kumwombea Baba Mtakatifu Leo XIV katika maisha na utume wake, ili aweze kuliongoza Kanisa kwa hekima, busara na upendo mkuu na wanamwomba, kamwe asiwasahau katika sala na sadaka yake, ili wale wanaokosa ujasiri wa kumchagua Kristo Yesu katika maisha yao, waweze kuitambua sauti yake katika kelele za Ulimwengu, ili kweli maisha yao, yawe ni kielelezo cha sadaka ya maisha inayotolewa kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu Leo XIV aendelee kuwa ni mwanga angavu wa imani, matumaini na mapendo.
Baba Mtakatifu Leo XIV alipowasili, mjini Assisi amefanya mahojiano ya maswali na majibu na vijana watatu. Kwanza kabisa wamemmwomba Baba Mtakatifu Leo XIV kuwapatia ushauri wa mambo yale wanayopaswa kufanya ili kweli waendelee kuwa ni wafuasi wamisionari amini wa Kristo Yesu, tayari kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini, furaha na wanyofu wa moyo. Baba Mtakatifu amewataka vijana kuwa ni wanyenyekevu wa moyo, wajitahidi kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu; wakuze imani yao kwa Kristo Yesu na kuishuhudia; wawe ni watu wa majadiliano katika ukweli na uwazi; wakite maisha yao katika majadiliano ya kidini na kiekumene; wajenzi wa haki, amani na upatanisho. Kama mashuhuda wa Kristo Yesu wajiepushe na utamaduni wa “kujimwambafai”, wabomoe kuta za kufikirika na maamuzi mbele; wajitahidi kujenga utamaduni wa upendo unaokita mizizi yake katika ukarimu; mambo ambayo si rahisi sana kutekelezwa, lakini ni chemchemi ya furaha ya kweli, amani na utulivu. Wawe ni vyombo vya Injili ya huruma na upendo; watu wasiokuwa na makelele wanaopenda kujenga na kudumisha Jumuiya ya waamini na kwamba, ushuhuda wa ufukara wa Kiinjili una nguvu zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Vijana wamemuuliza Baba Mtakatifu Leo XIV mambo msingi aliyokumbana nayo katika safari yake ya wito. Anasema, Mama Kanisa anawaalika vijana kufuata miito yao kikamilifu, hata wakati mwingine kwa kufanya maamuzi magumu, lakini yenye ujasiri na yanayoleta mageuzi makubwa katika maisha ya binadamu. Jambo la msingi ni kukita maisha yao katika fadhila ya upendo, kuwa na imani pamoja na kujiaminisha kwa Mungu. Vijana wajifunze kujifahamu, kufanya mang’amuzi na maamuzi na hatimaye, kuweza kumjibi kwa uaminifu Kristo Yesu anayewaita katika miito mbali mbali ndani ya Kanisa, na kwamba, wanapaswa kujitahidi kuwa waaminifu, ili waweze kupata utimilifu wa maisha. Rej. Yn 10: 10. Haya ndiyo yaliyomkuta katika safari ya maisha ya wito wake, hadi kupata wito maalum wa kuwa ni Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mwenyezi Mungu ameweka msingi wa maisha na wito wa kila mtu, changamoto na mwaliko wa kuendelea kusikiliza na kuitikia wito huu kila siku ya maisha, kwani kila wito ni safari ya ukombozi na uponyaji na kwamba, Kristo Yesu anawaita kila siku, anaangaza utu wao na kuwafanya waheshimu pia utu wa jirani zao.
Vijana wanasema, leo hii ni vigumu sana kuweza kuliamini Kanisa kuwa ni Mama na Mwalimu, kutokana na matatizo na changamoto zake; madonda yake, lakini daima yuko tayari kuwapokea watoto wake na kuwaonesha upendo. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mtakatifu Francisko wa Assisi, alisikiliza kwa makini na kulitafakari Fumbo la Msalaba kwa kina, akaona kashfa zilizoliandama Kanisa. Kristo Yesu katika Injili aliwateuwa wafuasi wake wachache, akawaita kuwa ni Mitume wake na ndani ya Kanisa waamini wanajikuta wakiwa ni ndugu wamoja, lakini bado linaelemewa na ubinadamu wake, lakini Kristo Yesu anakazia ujenzi wa umoja na udugu na kwamba, kwa yule anayetaka kuwa ni mkubwa atambue kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma. Neno la Mungu, Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni kielelezo cha Kanisa la Kristo Yesu linalotaka kuhudumia, kuwapokea watoto wake na kuwahudumia kwa upendo kwa kuwajalia maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Mungu na hivyo kuwawezesha kuwa watu huru zaidi. Mtakatifu Francisko wa Assisi aliitwa ili kulikarabati Kanisa la Kristo, lililokuwa linabomoka. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kila mwamini ndani ya Kanisa anao wajibu na dhamana; wito na karama zake; mambo yote haya yanapaswa kuwekwa kwa pamoja kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa. Ni Mama anayempeleka Kristo Yesu kwa waamini wake na kuendelea kubaki pamoja nao, ili kama waamini waendelee kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Mfufuka katika maisha na historia yao.
