Hayati Kardinali Langa: Chombo Cha Huduma, Amani na Majadiliano
Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema amepokea kwa majonzi na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Kardinali Júlio Duarte Langa, Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Xai-Xai, “Shai-Shai” nchini Msumbiji kilichotokea Jumatatu tarehe 3 Agosti 2026 huko Maputo, akiwa na umri wa miaka 98 tangu alipozaliwa, akabahatika kulitumikia Kanisa kama Padre kwa miaka 69 na Miaka 49 kama Askofu akiwa na dhamana ya: Kuongoza, Kutakatifuza na Kuwafundisha watu wa Mungu na Miaka 11 kama Kardinali. Baba Mtakatifu Leo XIV katika salam zake za rambirambi alizomwandikia Askofu mkuu mstaafu Francisco Chimoio, O.F.M. Cap. wa Jimbo kuu la Maputo na Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Xai-Xai, nchini Msumbiji, anasema, anapenda kuonesha ukaribu wake katika maisha ya kiroho kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji, kwa familia ya Marehemu Kardinali Júlio Duarte Langa, kwa Jimbo Katoli Katoliki la Xai-Xai na kwa nchi nzima ya Msumbiji, inayoomboleza kwa kumpoteza mchungaji wake mashuhuri, aliyekuwa mwaminifu kwa Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu; akajifunza kutoka kwake sanaa ya ujenzi wa ujirani mwema katika maisha na utume wake wa kuchunga roho za waamini.
Ni kiongozi aliyejisadaka bila ya kujibakiza, huku akijitoa kwa unyenyekevu, moyo wa bidii, na ustahimilivu kwa kundi ambalo alikabidhiwa na Mama Kanisa. Ni kiongozi ambaye katika maisha na utume wake, hakuruhusu kukata wala kukatishwa tamaa na changamoto mbalimbali zilizojitokeza bali aliona ndani yake maeneo yenye kiu ya Habari Njema ya Wokovu na hasa ilipohitajika kutangaza na kushuhudia Injili ya amani na upatanisho kwa ajili ya sasa na kwa wakati ujao wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu miongoni mwa watu wote wa Msumbiji. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, katika kipindi hiki cha majonzi na huzuni kubwa, lakini zaidi sana, ni muda wa imani na matumaini katika ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele, ni kipindi cha kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa maisha marefu aliyomkirimia Kardinali Júlio Duarte Langa, Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Xai-Xai, kwa neema ya Daraja Takatifu ya Upadre kwa Miaka 69, Miaka 49 kama Askofu na Miaka 11 kama Kardinali katika huduma kwa watu wa Mungu nchini Msumbiji na kwa Kanisa zima. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa baraka zake za kitume kwa wote wanaoshiriki katika Ibada ya Mazishi ya Kardinali Júlio Duarte Langa, Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Xai-Xai, Jumamosi tarehe 8 Agosti 2026 kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes huko Xonguene: “Shongwene.”
Itakumbukwa kwamba, Kardinali Júlio Duarte Langa, Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Xai-Xai, Msumbiji, alizaliwa tarehe 27 Oktoba 1927. Baada ya malezi na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 9 Juni 1957 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Lourenço Marques, Msumbiji. Tarehe 31 Mei 1976 akateuliwa na Mtakatifu Paulo VI kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Xai-Xai, Msumbiji na kuchagua kauli mbiu yake ya Kiaskofu kuwa ni “In finem dilexit eos” Yaani “Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo.” Yn 13:1. Kwa muda wa miaka 28 wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Msumbiji, akawaongoza, akawafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimboni Xai-Xai, hadi pale, tarehe 4 Oktoba 1992 Mkataba wa amani uliotiwa saini mjini Roma, Italia, na kujulikama kama Mkataba Mkuu wa Amani wa Msumbiji (General Peace Accords au Acordo Geral de Paz) ulimaliza vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu kwa takribani miaka 16 kati ya Serikali ya FRELIMO na waasi wa RENAMO. Tarehe 12 Julai 2004 Mtakatifu Yohane Paulo II akaridhia ombi lake la kutaka kung’atuka kutoka madarakani. Tarehe 14 Februari 2015 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Kardinali na ilipogota tarehe 3 Agosti 2026 akaitupa mkono dunia, akiwa na umri wa miaka 98 tangu alipozaliwa.
