Kardinali Júlio Duarte Langa Shuhuda wa Imani, Unyenyekevu na Huduma!
Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika salam zake za rambirambi alizomwandikia Askofu mkuu mstaafu Francisco Chimoio, O.F.M. Cap. wa Jimbo kuu la Maputo na Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Xai-Xai, nchini Msumbiji, kufuatia kifo cha Kardinali Julio Duarte Langa, Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Xai-Xai “Shai-Shai” anasema, anapenda kuonesha ukaribu wake katika maisha ya kiroho kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji, kwa familia ya Marehemu Kardinali Júlio Duarte Langa, kwa Jimbo Katoliki la Xai-Xai na kwa nchi nzima ya Msumbiji, inayoomboleza kwa kumpoteza mchungaji wake mashuhuri, aliyekuwa mwaminifu kwa Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu; akajifunza kutoka kwake sanaa ya ujenzi wa ujirani mwema katika maisha na utume wake wa kuchunga roho za waamini. Ni kiongozi aliyejisadaka bila ya kujibakiza, huku akijitoa kwa unyenyekevu, moyo wa bidii, na ustahimilivu kwa kundi ambalo alikabidhiwa na Mama Kanisa.
Ni kiongozi ambaye katika maisha na utume wake, hakuruhusu kukata wala kukatishwa tamaa na changamoto mbalimbali zilizojitokeza bali aliona ndani yake maeneo yenye kiu ya Habari Njema ya Wokovu na hasa ilipohitajika kutangaza na kushuhudia Injili ya amani na upatanisho kwa ajili ya sasa na kwa wakati ujao wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu miongoni mwa watu wote wa Msumbiji. Baba Mtakatifu Leo XIV alisema, katika kipindi hiki cha majonzi na huzuni kubwa, lakini zaidi sana, ni muda wa imani na matumaini katika ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele, ni kipindi cha kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa maisha marefu aliyomkirimia Kardinali Júlio Duarte Langa, Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Xai-Xai, kwa neema ya Daraja Takatifu ya Upadre kwa Miaka 69, Miaka 49 kama Askofu na Miaka 11 kama Kardinali katika huduma kwa watu wa Mungu nchini Msumbiji na kwa Kanisa zima.
Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba, Balozi wa Vatican nchini Msumbiji akiongoza Ibada ya Misa Takatifu na baada ya kusoma ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa watu wa Mungu nchini Msumbiji waliokuwa wamekusanyika kwenye Ibada ya Mazishi ya Kardinali Júlio Duarte Langa, Jumamosi tarehe 8 Agosti 2026 kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes huko Xonguene: “Shongwene” na mahubiri kutolewa na Askofu Lúcio Andrice Muandula, amesema Kanisa na jamii katika ujumla wake inawahitaji watu kama Kardinali Júlio Duarte Langa, kwani alikuwa ni chombo na shuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, alikuwa ni mtu mnyenyekevu asiyependa makuu na akabaki mwaminifu kutekeleza mapenzi ya Mungu mpaka dakika ya mwisho ya uhai wake hapa duniani. Kwake madaraka, kilikuwa ni kielelezo cha huduma kwa watu wa Mungu. Ni mtu aliyeridhika na maisha yake na wala hakuona utajiri ni kitu cha kufungamana sana nacho na wala hakupenda sifa za walimwengu. Ni katika muktadha huu, Hayati Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 14 Februari 2015 akamteuwa kuwa Kardinali, kwa sababu aliguswa sana na ushuhuda wa maisha yake, wema na unyenyekevu, akajisadaka katika majiundo ya watu wa Mungu, ili kuwaweka tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Alijitahidi kumwilisha katika maisha na utume wake, tunu msingi za Kiinjili, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu ndani na nje ya Msumbiji kutekeleza dhamana na majukumu yao katika ukweli, utakatifu, uaminifu, ukaribu kwa watu wa Mungu na unyenyekevu. Ni matumaini ya Askofu Mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba, Balozi wa Vatican nchini Msumbiji kwamba, amana, utajiri na urithi mkubwa wa maisha ya kiroho na kiutu aliouacha Kardinali Júlio Duarte Langa utaendelezwa na watu wa Mungu ndani na nje ya Msumbiji.
Itakumbukwa kwamba, Kardinali Júlio Duarte Langa, Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Xai-Xai, Msumbiji, alizaliwa tarehe 27 Oktoba 1927. Baada ya malezi na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 9 Juni 1957 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Lourenço Marques, Msumbiji. Tarehe 31 Mei 1976 akateuliwa na Mtakatifu Paulo VI kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Xai-Xai, Msumbiji na kuchagua kauli mbiu yake ya Kiaskofu kuwa ni “In finem dilexit eos” Yaani “Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo.” Yn 13:1. Kwa muda wa miaka 28 wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Msumbiji, akawaongoza, akawafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimboni Xai-Xai, hadi pale, tarehe 4 Oktoba 1992 Mkataba wa amani uliotiwa saini mjini Roma, Italia, na kujulikama kama Mkataba Mkuu wa Amani wa Msumbiji (General Peace Accords au Acordo Geral de Paz) ulimaliza vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu kwa takribani miaka 16 kati ya Serikali ya FRELIMO na waasi wa RENAMO. Tarehe 12 Julai 2004 Mtakatifu Yohane Paulo II akaridhia ombi lake la kutaka kung’atuka kutoka madarakani. Tarehe 14 Februari 2015 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Kardinali na ilipogota tarehe 3 Agosti 2026 akaitupa mkono dunia, akiwa na umri wa miaka 98 tangu alipozaliwa.
