Papa Leo XIV:"Mwaka wa kiliturujia una thamani katika maisha ya kila mwamini"
Na Angella Rwezaula – Vatican.
“Mwaka wa kiliturujia lazima ueleweke kama uhalisia wa kudumu wa kazi ya wokovu ambayo Kristo anaitimiza katika historia. Kupitia mzunguko huu wa kidunia, Kanisa linabaki katika uhusiano na tendo la ukombozi la Bwana, ili waamini wote wajazwe neema yake.” Haya yamo katika Mzunguko wa Katekesi unaojikita na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Usomaji Mpya wa Nyaraka zake, ambapo Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 12 Agosti 2026, akiwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, kwa waamini na mahujaji waliofika mjini Vatican aliendelea na Sura ya V ya Katiba ya Mtaguso ya Sacrosanctum Concilium (SC) kuhusu mada ya “mwaka wa kiturujia kwamba ni ya “thamani katika maisha ya kila mwamini.” Awali ya yote ni muhimu kukumbuka kwamba namna hii ya kulezea mzungukoo wa siku kuu za kikristo kama “mwaka wa kiliturujia,” ilienea lugha ya kikanisa, shukrani kwa kazi ya Mtumishi wa Mungu, Abati Prosper Guéranger (1805-1875).
Mwaka wa Kiliturujia ni Kristo mwenyewe
Katika Waraka wa Mediator Dei, Papa Pio XII anathibitisha kuwa huu siyo uwakilishi baridi na usio na uhalisia wa ukweli ambao ni wa zamani au kumbukumbu rahisi ya ukweli kutoka nyakati zingine. Mwaka wa kiliturujia, badala yake, ni Kristo mwenyewe, ambaye anaishi daima katika Kanisa lake na ambaye anaendeleza njia ya huruma kubwa iliyoanzishwa naye […] katika maisha haya ya kibinadamu […], kwa lengo la kuziunganisha roho za wanadamu na mafumbo yake na kuzifanya ziishi kwa ajili yao; mafumbo ambayo yapo na yanatenda kazi kila wakati. Kwa hivyo, mwaka wa kiliturujia lazima ueleweke kama uhalisia wa kudumu wa kazi ya wokovu ambayo Kristo anaitimiza katika historia. Kupitia mzunguko huu wa kidunia, Kanisa linabaki katika uhusiano na tendo la ukombozi la Bwana, ili waamini wote wajazwe neema yake. ( SC, 102), Papa Leo XIV alisisitiza.
Uhusiano wa Kristo unaweza kuonekana
Kukutana na Yesu, aliyekufa na kufufuka kwa ajili yetu, ndilo lengo ambalo Kanisa hufuata kila wakati, likiweka sherehe ya tukio la Pasaka katikati ya kila wakati. Kwa sababu hiyo, Papa Leo XIV alibanisha kwamba “Mababa wa Mtaguso waliiona Dominika "siku ya kwanza ya siku kuu," kuwa "msingi na kiini cha mwaka wa kiliturujia" (taz. SC, 106). Katika lugha kadhaa za kisasa, jina lake linathibitisha kuwa "dies Domini," "Siku ya Bwana." Hata katika lugha zile ambapo marejeo ya "siku ya jua" (Dominika, Sonntag) yameshinda, uhusiano na Kristo inaweza kuonekana: Yeye ndiye "jua la haki" la kweli linalomwangazia kila mtu!
Mtakatifu Yohane Paulo II, katika Barua yake ya Kitume Dies Domini (31 Mei 1998), anafundisha kwamba Dominika ni siku ya Bwana, siku ya Kanisa, siku ya mwanadamu na, hatimaye, "siku ya siku": “Kwa kuwa Dominika ni Pasaka ya kila Juma,ambpo siku ambayo Kristo alifufuka kutoka katika wafu inakumbukwa na kuwekwa sasa, pia ni siku inayofunua maana ya wakati. […] Ikitiririka kutoka Ufufuko, inapita katika wakati wa kibinadamu, miezi, miaka, karne, kama mshale unaoelekea unaopita ndani yake, ukiwaelekeza kuelekea lengo la kuja kwa mara ya pili kwa Kristo. Dominika inaashiria siku ya mwisho, ile ya Parousia (namba 75), ambapo sote tutafufuliwa.
Ili kutakasa Dominila lazima kuadhimisha Misa
Baba Mtakatifu Leo XIV aliendelea kusema kuwa "Ili kutakasa Dominika, ni muhimu kuadhimisha Misa. Kusikiliza Neno na kushiriki katika Mwili wa Kristo kunahusisha, kulingana na Mababa wa Mtaguso, kusanyiko la waamini (taz. SC, 106), yaani, kusanyiko la sherehe la waamini. Katika kusanyiko hili, jumuiya ya Kikristo inaonesha ushirika wake na Bwana na inashuhudia kuwa ni mali ya Kristo na uaminifu wake kwa Kanisa. Kusanyiko hili haliwezi kubadilishwa na uwepo wa kidijitali tu, wala haliwezi kupunguzwa kuwa kusanyiko lisilo na shughuli. Mkutano wa kiliturujia unatekelezwa kwa ushiriki hai wa kaka na dada, walioitwa pamoja "kumshukuru Mungu aliyewazaa 'kwa njia ya ufufuko wa Kristo kutoka katika wafu, kwa tumaini lililo hai' (1 Pet 1:3).
Ombi la Papa kushiriki ibada ya misa Takatifu
Katika suala hilo “ninawasihi kila mtu kutafuta hali bora ili kuhakikisha kwamba hata wale ambao hawawezi kuwa na muda wa mapumziko kazini siku za Dominika wanaweza kushiriki katika Misa Takatifu.” Papa alikazia kuwa “ mwaka wa kiliturujia, unaoadhimishwa na Dominika una historia ya kuvutia, iliyounganishwa na imani na ibada ya Kanisa. Tangu karne ya pili BK, kiukweli, sherehe ya Pasaka ya kila Juma imeunganishwa na ile ya Pasaka ya kila mwaka, "sherehe kuu" (SC, 102), iliyoongezwa katika "kipindi cha furaha zaidi" cha siku hamsini, ikifikia kilele katika Pentekoste, na kuandaliwa na Kipindi cha Toba cha Kwaresima (taz. SC, 109). Maendeleo yaliyofuata ya mzunguko wa Noeli, yaliyotokana na mzunguko wa Pasaka, yametuwezesha kuishi tena mafumbo la Neno la Mungu Kufanyika Mwili, kuzaliwa kwake, na kudhihirishwa kwake katika ulimwengu.
Vipindi kwa heshima ya Bikira Maria
Kanisa pia limeingiza katika vipindi mbalimbali heshima ya Bikira Maria, "iliyounganishwa bila kuvunjika na kazi ya Mwanae ya kuokoa"(SC, 103), na "ukumbusho wa mashahidi na watakatifu wengine ambao [...] mbinguni wanaimba sifa kamili kwa Mungu na kutuombea" (SC, 104).
Mwaka wa kiliturujia unaunda kanuni yenye msukumo wa matendo ya kichungaji
Kwa hivyo mwaka wa Kiliturujia unaonesha tena katika umbo la sakramenti, ufundishaji wa historia ya wokovu, ukiwaongoza waamini kutoka katika matarajio ya Masiha hadi utimilifu wa Fumbo la Pasaka na matarajio ya Utukufu ujao. Ndani yake, Kanisa linaadhimisha ukweli wa Wokovu wa Fumbo la Kristo, likiwaruhusu waamini kushiriki kwa undani zaidi. Kwa kuhitimisha Papa Leo XIV alisema: “Kwa sababu hiyo, mwaka wa kiliturujia unaunda kanuni yenye msukumo na mfumo muhimu kwa ajili ya matendo yote ya kichungaji.”
Nyaraka za Mtaguso wa II wa Vatican
Ikumbukwe kuna Nyaraka Kuu 4 za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican: “Dei verbum” kuhusu, “Ufunuo wa Kimungu”; “Sacrosanctum concilium” kuhusu, “ Liturujia”; “Lumen gentium” kuhusu Fumbo la Kanisa” pamoja na “Gaudium et spes” kuhusu “Kanisa katika ulimwengu mamboleo.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.
