Kumbukizi ya Miaka 81 Tangu Hiroshima na Nagasaki Ilipuliwe Kwa Mabomu ya Nyuklia
Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.
Mtakatifu Yohane Paulo II wakati wa hija yake ya Kitume nchini Japan kunako mwaka 1981 aliwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema: kufunga na kusali, kufanya toba na wongofu wa ndani kwa ajili ya kuombea amani huko Hiroshima na Nagasaki nchini Japan. Hii ni miji inayotikiswa sana kutokana na madhara makubwa ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Utu, heshima na haki msingi za binadamu zilisiginwa. Mwanadamu akaonja ukatili wa silaha za nyuklia, mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita zaidi katika mchakato wa ujenzi wa: Majadiliano katika ukweli na haki; amani na maridhiano duniani. Ilikuwa ni tarehe 6 Agosti 1945 bomu la kwanza la atomiki liliporushwa mjini Hiroshima na kupelekea vifo vya watu kati ya 70, 000 hadi 80, 000 na hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 1945 watu waliofariki dunia walikuwa ni 140, 000 na tarehe 9 Agosti 1945 mji wa Nagasaki ukalipuliwa kwa bomu la atomiki na kupelekea vifo vya watu 150, 000 hadi 246, 000 na kwamba, huu ni mwaka wa 81 tangu mabomu hayo ya atomiki yaliporushwa nchini Japan. Kardinali Isao Tarcisio Kikuch, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Japan, CBCJ, anasema, mashambulizi haya yalisababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, watu wengi walifariki dunia, walijeruhiwa na kupata ulemavu wa kudumu; kulikuwepo na uharibifu mkubwa wa mazingira na miundo mbinu na kwamba, huu ni muda wa kuombea amani ili iweze kutamalaki ulimwenguni kote. Tangu wakati wa hija ya Kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II, familia ya Mungu nchini Japan kuanzia tarehe 6 hadi 15 Agosti ya kila mwaka imekuwa ikisali kwa ajili ya kuombea amani duniani. Huu ni muda muafaka wa kusali na kutafakari kuhusu Injili ya amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Majadiliano katika ukweli na uwazi, yasaidie kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV katika Maadhimisho ya Siku ya 59 ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi, Januari 2026 ulinogeshwa na kauli mbiu: "Amani iwe nanyi nyote: Kuelekea amani "Isiyo na Silaha na inayopokonya Silaha. Ikumbukwe kwamba, "Kauli mbiu inayonogesha Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV katika Maadhimisho ya Siku ya 60 Kuombea Amani Duniani kwa mwaka 2027 ni “Disarming Technology, Serving Peace. Politics as Preventive Responsibility.” Yaani “Legeza Teknolojia, Imarisha Amani. Siasa Kama Wajibu wa Kinga.” Itakumbukwa kwamba, tarehe 20 Septemba 2017 Vatican iliridhia Mkataba wa Kimataifa unaopiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za nyuklia. Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Japan, CBCJ, kwa ajili ya Siku 10 za kuombea Amani Duniani, kuanzia tarehe 6-15 Agosti 2026 unanogeshwa na kauli mbiu: "Guided by the hibakusha-inspired Spirit of Hiroshima, let us work together in heartfelt unity to change the world.” Yaani “Tukiongozwa na Roho ya Hiroshima iliyochochewa na waathirika wa mabomu ya atomiki (hibakusha), na tufanye kazi pamoja kwa umoja wa dhati ili kuibadilisha dunia.” Baraza la Maaskofu Katoliki Japan, kwa nyakati mbalimbali limekuwa likitoa ujumbe kwa ajili ya kumbukumbu ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Maaskofu wanasema, leo hii bado kuna vita, kinzani na migogoro mbalimbali. Kuna wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Kuna vita baridi inayoendelea kati ya China na Marekani, Marekani na Iran hali inayodhohofisha mahusiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni. Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linawahamasisha wadau katika mgogoro huu, kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Tarehe 22 Januari 2021, Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW, ulioridhiwa na Mataifa zaidi ya 50 ulianza kutumika rasmi. Huu ni Mkataba wa Kimataifa unaopiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za nyuklia. Hii inatokana na ukweli kwamba, matumizi ya silaha hizi hayana macho wala pazia, na hayawezi kuchagua wala kubagua! Katika kipindi kifupi tu, matumizi ya silaha hizi yanaweza kusababisha maafa makubwa na yatakayodumu kwa muda mrefu kwa binadamu na mazingira yake. Wachambuzi wa masuala ya mikataba ya Kimataifa wanakiri kwamba, Mkataba huu ni dhaifu sana kwani bado kuna idadi kubwa ya Mataifa hayajaridhia, changamoto na mwaliko kwa nchi ambazo bado hazijaridhia kufanya hivyo haraka iwezekanavyo, kwani silaha za maangamizi zinatishia usalama na amani duniani. Myanmar, Afghanstan na maeneo mengine duniani, bado kuna uvunjwaji wa haki msingi za binadamu na kwamba, amani inaonekana kana kwamba, iko mbali. Utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kudumishwa, badala ya kusingizia usalama wa Taifa na ustawi wa nchi husika.
Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Japan Mwezi Novemba 2019, alikazia umuhimu wa kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani. Aliwataka vijana wa kizazi kipya kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutafuta na kudumisha amani. Rasilimali fedha inayotumika kwa ajili ya kutengeneza, kuboresha na kuhifadhi na hatimaye, kuuza silaha za maangamizi, nyuma yake kuna kilio cha watoto na familia nyingi duniani. Watu wanatamani amani ya kudumu ili kuondokana na vitisho vya silaha za maangamizi na kwamba, hii ni changamoto inayowahusisha watu wote; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kuaminiana na wala si katika tabia ya kupimana nguvu. Kuna haja ya kudhibiti biashara ya silaha kimataifa na maendeleo makubwa ya teknolojia kuhusu masuala ya kijeshi. Hii ni dharura inayohitaji kushughulikiwa na viongozi wote wa Jumuiya ya Kimataifa.
Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” unagusia kwa namna ya pekee kuhusu: magonjwa jamii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Msamaria mwema anawekwa mbele ya walimwengu kama ni mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini. Baba Mtakatifu anakazia maisha ya kiroho, mshikamano wa kidugu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, utawala bora, ushirikiano na mshikamano katika kukabiliana na changamoto mamboleo ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee. Baba Mtakatifu anagusia kuhusu siasa safi kwa ajili ya huduma kwa jamii, maendeleo, ustawi na mafao ya wengi; utu, haki msingi za binadamu na umuhimu wa kufanya mageuzi makubwa kwenye Umoja wa Mataifa ili kweli uweze kuwa ni “familia ya Mataifa.” Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linakaza kusema, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Ni katika kulinda na kudumisha uhai wa kila kiumbe, hapo amani inaweza kuundwa na kudumishwa kikamilifu!
Baba Mtakatifu Francisko anasema, dunia bila kuwa na silaha za kinyuklia inawezekana kabisa na ni muhimu sana na kwamba, silaha hizi za maangamizi kamwe haziwezi kuwasaidia viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na uhakika wa usalama wa raia na mali zao kitaifa na kimataifa. Kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu madhara yake katika maisha ya watu sanjari na mazingira; kwa kuondoa hofu, mazingira ya kutoaminiana, chuki na uhasama vinavyozungumza “dhana ya silaha za nyuklia.” Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linasema amani ni safari ya matumaini, mwaliko kwa wananchi wa Japana kuendelea kuwajibika kulinda na kudumisha amani, umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu unaofumbata majadiliano katika ukweli na uwazi. Maaskofu wanawataka watu wa Mungu nchini Japan kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya amani, ili amani ya Kristo iamue miyoni mwao. Umefika wakati wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini kutoka sehemu mbalimbali za dunia, kwa kujenga na kuimarisha utamaduni wa majadiliano; toba na wongofu wa ndani, ili utamaduni wa uhai, upatanisho na udugu viweze kutawala katika akili na nyoyo za watu.
Ifuatayo ni Sala ya Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa ajili ya kuombea amani duniani: "Ee Bwana unifanye kuwa chombo cha amani. Palipo chuki nieneze upendo. Palipo na mashaka pawe na imani. Palipo na tumaini pawe na matumaini. Palipo na giza pawe na mwanga. Palipo na huzuni pawe na furaha. Ee Bwana Mungu, unijalie; Nisitafute kufarijiwa bali kufariji Nisitafute kupendwa bali kupenda. Kwani ni katika kutoa ndipo tunapopokea Ni kwa kusamehe ndipo tunaposamehewa. Na ni kwa kufa ndipo tunazaliwa katika uzima wa milele, AMINA". Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu: kutubu, kuongoka na kujiaminisha mbele ya Mungu ili aweze kuwageuza kuwa ni vyombo vya amanbi, upendo na mshikamano wa kweli na hivyo kutorudia tena kwenye makosa ya kihistoria.
