Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV katika Nia zake kwa Mwezi Agosti 2026 anawaalika waamini kuungana pamoja naye kusali kwa ajili ya kukoleza mchakato wa uinjilishaji mijini Baba Mtakatifu Leo XIV katika Nia zake kwa Mwezi Agosti 2026 anawaalika waamini kuungana pamoja naye kusali kwa ajili ya kukoleza mchakato wa uinjilishaji mijini  (AFP or licensors)

Nia za Baba Mtakatifu Leo XIV Kwa Mwezi Agosti 2026: Uinjilishaji Mijini

Papa Leo XIV katika Nia zake kwa Mwezi Agosti 2026 zinazosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Mawasiliano Jamii, anawaalika waamini kuungana pamoja naye kusali kwa ajili ya kukoleza mchakato wa uinjilishaji mijini kwani katika miji mikubwa ambayo mara nyingi watu hujulikana kwa hali ya kutojulikana, huku wakielemewa na upweke hasi, Kanisa liweze kupata njia mpya za kutangaza na kushuhudia Injili!

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mataguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa kimsingi ni Sakramenti ya wokovu, linatumwa kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu, kama sehemu ya utii wa agizo lililotolewa na Kristo Yesu mwenyewe kwa wafuasi wake. Dhamana hii kwa mara ya kwanza ilitekelezwa na Mitume, waliofuata nyayo za Kristo Yesu, wakahubiri Neno la uzima na kuanzisha Makanisa. Waandamizi wa Mitume wanao wajibu msingi wa kuhakikisha kwamba, Neno la Mungu linaendelea kutukuzwa, huku Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika kweli na uzima; utakatifu na neema; haki, mapendo na amani ukitangazwa na kusimikwa duniani kote! Amri ya kimisionari ya Kristo Yesu ina chanzo na kilele chake katika upendo wa milele unaopata chimbuko lake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kwa tabia yake, Kanisa linalosafiri hapa duniani ni la kimisionari, kwani linachota chanzo chake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili kuwawezesha watu kushiriki katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Uinjilishaji ni kielelezo cha mapendo ya Mwenyezi Mungu kwa binadamu. Kutangaza na kushuhudia Injili ni dhamana na utume ambao Kristo Yesu amewakabidhi Mitume wake. Huu ni utume wa kwanza unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa kila mtu na kwa ulimwengu mzima. Utume huu unatekelezwa kikamilifu na Mama Kanisa anapotangaza na kushuhudia Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini kwa binadamu wote: kiroho na kimwili. Upendeleo wa pekee ni kwa maskini, wagonjwa na wadhaifu ndani ya jamii. Katika muktadha huu, Kanisa linapaswa kujikita katika: Toba na wongofu wa kimisionari na kichungaji kwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Kanisa lijitambulishe na kueleweka kuwa ni Fumbo la Ushirika unaomwilishwa katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari.

Papa anaomba upendo unaoweza kushinda haraka za mijini
Papa anaomba upendo unaoweza kushinda haraka za mijini   (ANSA)

Ni katika muktadha wa utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu, Baba Mtakatifu Leo XIV katika Nia zake kwa Mwezi Agosti 2026 zinazosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Mawasiliano Jamii, anawaalika waamini kuungana pamoja naye kusali kwa ajili ya kukoleza mchakato wa uinjilishaji mijini kwani katika miji mikubwa ambayo mara nyingi watu hujulikana kwa hali ya kutojulikana, huku wakielemewa na upweke hasi, Kanisa liweze kupata njia mpya za kutangaza na kushuhudia Injili, kwa kujikita katika njia bunifu za kujenga jumuiya. Baba Mtakatifu anamwomba Kristo Yesu, Mchungaji mwema anayetembea katika mitaa na viwanja vya miji, anayeingia katika majengo marefu na vitongoji vya kawaida, huku akiandamana na mamilioni ya watu wanaotafuta maana ya maisha katikati ya kelele na haraka nyingi. Moyo wa majiji una mwanga na vivuli vyake; una kelele na upweke wake, awawezeshe waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wake mijini, wawe ni wamisionari jasiri na wenye kipaji cha ugunduzi, wanaotangaza na kushuhudia kwa mtindo wa maisha yao upendo unaovuka mipaka ya haraka, kelele na hali ya kutotambulikana mijini. Majiji yameitwa kuwa ni mahali pa uhuru na fursa, lakini yanaweza pia kuwa ni mahali pa watu kutojulikana na hatimaye kutengwa.

Papa Leo XIV anawataka waamini wawe ni mashuhuda wa uinjilishaji
Papa Leo XIV anawataka waamini wawe ni mashuhuda wa uinjilishaji   (ANSA)

Ndiyo maana Baba Mtakatifu Leo XIV anamwomba Kristo Yesu awawezeshe waamini kuwa na mtazamo mpya unaoweza kugundua katikati ya maisha ya jiji ardhi yenye rutuba ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Anamwomba Kristo Yesu awakirimie imani ya ubunifu na ya kina inayomwilishwa katika matendo adili na ya upendo. Awajalie waamini kuwa ni Kanisa linatoka nje, lenye uwezo wa kuwafikia wote wanaosukumizwa pembezoni mwa miji, ili liweze kuwafariji wapweke na hatimaye, kupanda mbegu za udugu na uhusiano badala ya hali ya kutojali na kugeuziana kisogo. Jumuiya za mijini ziwe ni nyumba wazi zinazokaribisha, mahali ambapo tumaini linashirikishwa na wote wanapata fursa ya kuonekana na hivyo kuiwezesha furaha ya Injili kuchanua na kung’aa katika maisha ya waamini walio wengi. Mwishoni, Baba Mtakatifu anamwomba Kristo Yesu awafanye waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wake mijini, wamisionari jasiri na wabunifu wanaotangaza na kushuhudia upendo wa Mungu kwa njia ya maisha yao adili na matakatifu. Huu ni upendo anasema, Baba Mtakatifu Leo XIV wenye uwezo wa kushinda haraka, kelele na hali ya kutojulikana mijini.

Upendo ushinde haraka, kelele na hali ya kutokujulikana
Upendo ushinde haraka, kelele na hali ya kutokujulikana   (AFP or licensors)

Takwimu zinaonesha kwamba, takribani asilimia 45% ya idadi ya watu ulimwenguni kote wanaishi mijini na hivyo kuifanya miji kuwa ni eneo maalum la uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ongezeko la idadi ya watu wanaozaliwa kila siku, limeibua changamoto za kijamii na kijumuiya, kiasi kwamba, vitongoji vingi havijulikani na hatimaye kunaibuka ofisi na maeneo ya biashara ambayo yanatumika kama maficho na mahali pa upweke hasi na matokeo yake ni watu wa mijini kuzama sana katika matumizi ya mitandao ya kijamii. Watu wanajenga na kudumisha uhusiano wa juu juu ambao kimsingi hauna mizizi, watu wanashindwa kujenga hata ujirani mwema, ingawa wanaishi katika ghorofa moja, kiasi kwamba, hakuna nafasi ya watu kukutana na “kujamiiana.” Ndiyo maana Padre Frédéric Fornos SJ., Mkurugenzi wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, utume ambao umeenea katika nchi 98 duniani na unashirikiana kwa karibu sana na Chama cha Kitume cha Vijana wa Ekaristi anasema, Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufanya tafakari ya kina, itakayowawezesha kufanya toba, wongofu na mabadiliko ya ndani yanayopata chimbuko lake katika moyo wa sala na kwamba, kwa nguvu na uweza wa Roho Mtakatifu, anaweza kuwajalia waamini mwanga wa jinsi ya kujenga miji inayosimikwa katika haki, ukarimu na ujirani mwema. Mtindo huu wa uinjilishaji unaiwezesha Injili isiyoonekana, iweze kuonekana, kutangazwa na kushuhudiwa. Hii ni sehemu ya mchakato wa kupandikiza mbegu ya imani, uwapo angavu na endelevu wa Kristo Yesu kwa Neno, Sakramenti na Huduma makini inayosimikwa katika huruma na upendo, ili yote haya yaweze kuonekana wazi wazi na walimwengu.

Nia za Papa Mwezi Agosti 2026
02 Agosti 2026, 15:32