Tafuta

Papa kwa Watawa:Upendo ni dawa dhidi ya utandawazi wa kutojali

Katika ujumbe wa video kwa Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Wakuu wa Mashirika ya kitawa wa Marekani(LCWR),Papa Leo XIV anakumbusha kwamba Kanisa linahitaji wanaume na wanawake waliowekwa wakfu kwa sababu ya uchangamfu wao na ushuhuda wao wa maisha yanayomhusu Yesu na wanaweza kuchangia katika kuamsha Ulimwengu.Papa alishukuru kwa michango ya kudumu ya Taasisi zao katika nyanja za uinjilishaji,elimu na matunzo kwa maskini na waliotengwa.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kanisa linahitaji wanaume na wanawake watawa na utofauti na utajiri wote wa aina za utakaso na huduma wanazowakilisha, kwa sababu kwa nguvu zao na ushuhuda wa maisha yanayomlenga Yesu, wanaweza kusaidia kuuamsha ulimwengu. Kwa hivyo, pamoja, tutaweza kukabiliana na utandawazi wa kutojali na kutokuwa na uwezo na tiba ya upendo na huruma ya Kristo. Kwa maneno hayo, Baba Mtakatifu Leo XIV ananukuu Hotuba ya washiriki wa Jubilei ya Watawa  iliyofanyika tarehe 10 Oktoba 2025 akiwaelekea kwa njia ya video, kwa lugha ya kiingereza  Watawa waliokusanyika huko Orlando kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa Baraza la Wakuu wa Mashirika Makuu nchini Marekani(Lcwr-Leadership Conference of Women Religious) katika fursa ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwao.

Katika ujumbe wake Papa anawasalimia wote na kuwatakia heri wanaume na wanawake wa makanisa mbalimbali nchini Marekani wanaoshiriki katika hafla ya mkutano huo kwa mwaka huu.  “Ijapokuwa mnatoka katika jumuiya zenye historia na utume tofauti, ni muhimu kukumbuka haja ya kukuza umoja katika Taasisi zenu na kati ya kila mmoja wenu, na pia katika Kanisa kwa ujumla," Papa alisema na kuongeza: "Wakristo wote wameitwa kuwa wajenzi wa Ushirika wa Kristo, ambao unafanyika katika Kanisa la Sinodi ambamo kila mtu anashirikiana katika utume sawa kulingana na karama na huduma yake (Taz.Hotuba ya Papa katika Ufunguzi wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Makardinali, 26 Juni 2026).

Watawa wanaitwa kuwa wataalamu wa Sinodi

Kwa  namna ya  pekee, Papa Leo XIV anabainisha kwamba: “washiriki wa maisha ya kitawa wanaitwa kuwa wataalamu wa Sinodi kwa sababu ya fursa za kuifanya kazi inayotolewa na maisha ya jumuiya, na pia kwa jinsi ya Mashirika yenu yalivyopangwa (Taz. Mkutano na Washiriki katika Jubilei Watawa, Oktoba 10, 2025). Kwa maana hiyo Papa anasema, “nilifurahi kusikia  kwamba taratibu za Mkutano Mkuu zitajumuisha njia ya sinodi ya kusikiliza, kujadili, na utambuzi, kwa uwazi na nia ya kuelewa kile ambacho wengine wanasema.”

Matumaini ya Papa kwa mazungumzo ya kidugu kwa mstakabali wa huduma

 “Ninatumaini kwamba, kupitia muundo huu wa mazungumzo ya kidugu na ya kupokea, mtaweza kutambua kile ambacho Roho Mtakatifu anasema (Ufu 2:7) kuhusu sasa na mustakabali wa maisha yaliyowekwa wakfu katika mataifa mnayohudumia.” Hasa, kupitia karama nyingi zilizotolewa na Roho Mtakatifu katika historia yote, wanawake na wanaume waliowekwa wakfu wamesaidia kufanya utume na fumbo la Kanisa kuonekana katika ulimwengu wetu (taz. Mtakatifu Yohane Paulo II, Wosia wa Kitume Baada ya Sinodi Vita Consecrata, n. 1)." Papa Leo katika hilo amewapongeza kwamba: "Katika suala hilo, ninatoa shukrani kwa michango endelevu ya Taasisi zenu katika nyanja za uinjilishaji, elimu, na kuwatunza maskini na waliotengwa, kwa kutaja machache tu."

"Karama Nyingi, Roho mmoja, Wito mmoja"

Mnapotafakari mada yenu,“ Many Charisms, One Spirit, One Call”,  yaani Karama Nyingi, Roho mmoja, Wito mmoja, ninasali  kwamba mtakumbuka, kwa njia ya pekee, karama maalum ambazo Mungu amewakabidhi waanzilishi wa kike na kiume wa jumuiya zenu husika.” Papa Leo XIV alisisitiza kwamba “ Kanisa linawahitaji ninyi na utofauti wote na utajiri wa aina za utakaso na huduma mnazowakilisha, kwani kwa nguvu zenu na ushuhuda wenu wa maisha yanayomlenga Yesu, mnaweza kusaidia kuamsha ulimwengu (tazama Kukutana na washiriki katika Jubilei ya Watawa, Oktoba 10, 2025). Kwa hivyo, pamoja, mtaweza kukabiliana na utandawazi wa kutojali na kutokuwa na nguvu kwa tiba ya upendo na huruma ya Kristo."

Viapo vya umaskini, usafi wa moyo na utii huleta furaha,amani na utimilifu

Baba Mtakatifu anakazia kuwa, “ili kukuza ustawi halisi wa maisha yaliyowekwa wakfu, kufanya kazi ili kukuza miito ya kitawa ni muhimu sana. Kama wengi wetu tulivyopitia kibinafsi, wito wa Kristo wa kumfuata kwa moyo usiogawanyika kupitia viapo vya umaskini, usafi wa moyo, na utii huleta furaha, amani, na utimilifu.” Leo, licha ya kuongezeka kwa udini duniani, pia kuna njaa inayoongezeka ya Mungu. Hakika, kama nilivyoona hivi karibuni wakati wa ziara yangu ya Kitume kwenda Hispania, "vijana na watu wazima wanagundua upya imani ya Kikristo, labda baada ya kipindi maishani mwao ambacho walikuwa wamejitenga na Mungu" (Mkesha wa Maombi, Juni 9, 2026).

Kwa njia hiyo, Papa Leo XIV alisema kwamba "ni katika mwingiliano wenu na vijana, katika kujaribu kutafuta njia za kushirikiana nao, njia yenu ya maisha na kuwasaidia kusikia sauti ya Bwana, anayezungumza nasi kwa kina cha mioyo yetu." Papa ameomba "Watieni moyo kuwa na ujasiri wa kumjibu Yesu, ambaye ukarimu wake hauwezi kupitwa, ili wao pia waweze kushiriki furaha inayotokana na kufuata wito wake." Kwa hisia hizo Papa Leo XIV alibainisha “ninawatakia mkutano wenye matunda na kuwahakikishia ukaribu wangu wa kiroho. Ninakabidhi kazi ya Mkutano mkuu  kwa ulinzi wa mama wa Maria, Mama wa Kanisa, ili aweze kuwaombea nyote na kwa Jumuiya mnazowakilisha. Na Mungu Mwenyezi awabariki, Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Amina.”

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.

 

 

12 Agosti 2026, 16:42