Tafuta

Kauli mbiu: “Mwitikio unaozingatia imani dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya na utumbukizaji wa vijana katika uhalifu: Majadiliano kutoka Amerika ya Kusini na Carribean kwenda Ulimwenguni kote.” Kauli mbiu: “Mwitikio unaozingatia imani dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya na utumbukizaji wa vijana katika uhalifu: Majadiliano kutoka Amerika ya Kusini na Carribean kwenda Ulimwenguni kote.”   (@VATICAN MEDIA)

Papa Leo XIV Familia Kitovu Cha Mapambano Dhidi ya Matumizi Haramu Dawa za Kulevya!

Papa Leo XIV: Lengo ni kutafakari, kwa mtazamo wa imani, kuhusu tatizo la dawa za kulevya na athari zake kwa vijana wa kizazi kipya kwani uraibu ni jambo tata linaloanika wazi kushindwa kwa ulimwengu uliopoteza utu. Mateso ya vijana yanahitaji majibu ya kina: hatua za kuzuia zinazohusisha jamii, huduma za kitaalamu za kitabibu, haki yenye kuzingatia utu na heshima ya binadamu, sanjari na kuwa na uongozi wa karibu katika utekelezaji wa shughuli za kichungaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini kwa kushirikiana na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean CELAM, Mpango wa CELAM wa Huduma ya Kichungaji kwa ajili ya Kusaidia na Kuzuia Uraibu (PLAPA), na Tume ya Amerika ya Kusini Kwa Ajili ya  Kudhibiti Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya (CICAD) ambayo ni chombo cha ushauri na usaidizi cha Shirika la Mataifa ya Amerika (OAS) kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 27 Agosti 2026 imekuwa ikikutana mjini Vatican kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Mwitikio unaozingatia imani dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya na utumbukizaji wa vijana katika uhalifu: Majadiliano kutoka Amerika ya Kusini na Carribean kwenda Ulimwenguni kote.” Biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo kama vile kazi za suluba kwa watoto wadogo, biashara ya ngono, biashara haramu ya viungo vya binadamu; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Mambo haya yanapaswa kutambuliwa kama yalivyo na viongozi wote wa kidini, wanasiasa, viongozi wa kijamii na watunga sheria wa kitaifa na kimataifa! waathirika wakuu wa janga la biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni vijana wa kizazi kipya wanaopoteza dira, mwelekeo na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Kumbe, huu umekuwa ni muda muafaka wa kufanya upembuzi yakinifu juu ya madhara ya matumizi haramu ya dawa za kulevya huko Amerika ya Kusini na Caribbean. Wajumbe wa Mkutano huu, Alhamisi tarehe 27 Agosti 2026 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican.

Familia ziwezeshe kupambana na matumizi haramu dawa za kulevya
Familia ziwezeshe kupambana na matumizi haramu dawa za kulevya   (@VATICAN MEDIA)

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake amewashukuru na kuwapongeza wale wote wanaoendelea kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwasindikiza vijana, kuzuia matumizi haramu ya dawa za kulevya, kusaidia kupona na kujumuika tena katika jamii, wakiwa wametoka Asia, Afrika, Ulaya, na Amerika na kwamba, uwepo wao unawakumbusha waamini kwamba, mateso na matumaini havina mipaka.Dhumuni kubwa lililowakusanya pamoja ni kutafakari, kwa mtazamo wa imani, kuhusu tatizo la dawa za kulevya na athari zake kwa vijana wa kizazi kipya kwani uraibu ni jambo tata linaloanika wazi kushindwa kwa ulimwengu uliopoteza utu. Mateso ya vijana yanahitaji majibu ya kina: hatua za kuzuia zinazohusisha jamii, huduma za kitaalamu za kitabibu, haki yenye kuzingatia utu na heshima ya binadamu, sanjari na kuwa na uongozi wa karibu katika utekelezaji wa shughuli za kichungaji. Mchango wao anasema Baba Mtakatifu Leo XIV lazima uzingatie huduma, uwepo, na ujenzi mpya wa mshikamano wa kijamii. Hii ndiyo maana madaraja manne yamekutana ili kushirikiana na kushikamana katika mkutano huu, yakiwakilisha njia mbalimbali za ushirikiano katika kukabiliana na tatizo na changamoto ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Daraja la kwanza linaunganisha Kanisa na mashirika ya kimataifa, kwani hakuna anayeweza kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya peke yake. Katika muktadha huu, ni muhimu kutaja ushirikiano unaoendelea kati ya Shirika la Mataifa ya Amerika (OAS); Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean CELAM; hawa wanaratibu mafunzo kwa mashirika ya kijamii yenye misingi ya imani na kujenga mitandao ya kutoa mwongozo na usaidizi; juhudi ambazo zimewezesha CELAM kuandaa Mwongozo wa Huduma ya Kichungaji ya Amerika ya Kusini kuhusu Usaidizi na Kinga dhidi ya Uraibu.

Papa Leo XIV akipokea Kitabu kutoka kwa washiriki
Papa Leo XIV akipokea Kitabu kutoka kwa washiriki   (@VATICAN MEDIA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Daraja la pili linaunganisha sayansi na imani. Kanisa haliingilii suala la matumizi haramu ya dawa za kulevya kwa lengo la kushindana au kuchukua nafasi ya sayansi ya neva (neuroscience), saikiatria, au afya ya jamii; badala yake, linajaribu kutoa mwanga kuhusu suala hilo kupitia tunu msingi za Injili, likijikita katika uelewa mpana na kamili wa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Daraja la tatu lipo ndani ya Kanisa lenyewe katika safari yake kupitia Mabara mbalimbali. Watu kutoka Amerika, Asia, Afrika, na Ulaya wamekusanyika hapa ili kushirikishana huzuni, matumaini, na ari yao ya shughuli za kichungaji. Daraja la nne ni la Majadiliano ya kiekumene. Kupitia matendo halisi ya Injili ya upendo kwa wanaoteseka, Kanisa Katoliki na jumuiya nyingine za Kikristo hugundua lugha yenye nguvu na ya pamoja inayobubujika kutoka katika imani; lugha inayowawezesha kuandamana na vijana wa kizazi kipya na hivyo kuwakumbatia katika mahitaji yao msingi na ndoto zao. Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake, ametoa kipaumbele cha kwanza kwa familia ambayo kwa kadiri ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Hapa ni mahali pa kulea, kutunza na kujiandaa kwa siku za mbeleni. Rej LG, 11. Hakuna kinga bora dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya kuliko familia imara na madhubuti.

Papa Leo XIV amewapatia baraka zake za kitume
Papa Leo XIV amewapatia baraka zake za kitume   (@VATICAN MEDIA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasikitika kusema kwamba, “Leo, tunashuhudia maumivu ya familia nyingi zilizomeguka na kusambaratika, iiwe ni kwa sababu ya matumizi haramu ya dawa za kulevya, vurugu, mtoto kujiingiza katika uhalifu, umaskini wa mali, maadili na utu mwema, au ukosefu wa fursa unaowasukuma watu wengi pembezoni mwa jamii. Mtakatifu Yohane Paulo II alituomba tulifanye Kanisa kuwa "nyumba na shule ya ushirika. Rej. Barua ya Kitume “Novo Millennio Ineunte”, 43. Na Baba Mtakatifu Francisko alitukumbusha kuwa Yesu anataka "tuguse taabu za za binadamu, tuguse miili ya watu wengine wanaoteseka.” Rej. Evangelii gaudium, 270. Hii inabainisha kwamba kiini hasa cha utume wanaoutekeleza: ni ule wa Kanisa kuwa familia, familia inayowakumbatia hasa wale wanaoteseka. Hatimaye, Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha hotuba yake kwa kuonesha matamanio yake halali ya kulitaka Kanisa liwe familia kwa wale wote wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii kama yule Msamaria mwema kwa mtu anayengukia mikononi mwa wanyang’anyi waliomtenda vibaya na kumwacha karibu ya kufa, watu wasipite  bila kujali wana kuguswa na mahangaiko ya wengine; Waamini wajenge Kanisa linalosimama, linalokaribia, linaloguswa na kuonesha huruma, linalopaka mafuta ya upendo na divai ya huruma yale majeraha; Kanisa linalolisha, na kuwa makazi ya watu waliovunjika na kupondeka moyo.

Papa Leo XIV Dawa za Kulevya

 

 

27 Agosti 2026, 15:27