Papa Leo XIV Majadiliano ya Kiekumene Na Waluteri wa Norway: Ushuhuda wa Pamoja
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa katika maisha na utume wake anaendelea kukazia: Uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma, kwani uekumene wa damu na ule wa utakatifu wa maisha ni mambo msingi yanayoshuhudiwa na Wakristo sehemu mbalimbali za dunia katika umoja, udugu na upendo kama kikolezo cha ujenzi wa Ufalme wa Mungu na wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Uekumene wa damu unajikita katika: Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo. Lakini, ikumbukwe kwamba, damu ya mashuhuda hawa wa imani ni chachu ya Ukristo. Uekumene wa maisha ya kiroho na utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu wa kibinadamu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile watahamasisha na kutekeleza umoja wa Wakristo na udugu wa kibinadamu kati yao. Uekumene wa huduma unatekelezwa kwa njia ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na maisha ya kitume.
Ni katika muktadha wa Majadiliano ya Kiekumene, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 26 Agosti 2026 amekutana na kuzungumza na Maaskofu kadhaa wa Kanisa la Kiluteri kutoka nchini Norway waliomtembelea mjini Vatican. Baba Mtakatifu ameonesha furaha yake kubwa na kwamba, katika hija yao ya maisha ya kiroho mjini Roma, wamepata nafasi kutembelea maeneo matakatifu yanayohusiana na Wakristo wa mwanzo sanjari na mashuhuda wa imani na kwamba, ushuhuda wao wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake unabaki kuwa ni chemchemi ya kudumu ya msukumo unaowahimiza Wakristo katika Ulimwengu mamboleo kusadaka maisha yao kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao. Baba Mtakatifu Leo XIV amewaambia Maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri kutoka Norway kwamba, kwa sasa watu wa Mungu wanapitia changamoto nyingi na misukosuko mikubwa; kuna ongezeko la uhasama kati ya watu, jambo linaloloshuhudiwa si tu katika migogoro na kinzani za Kimataifa, bali pia katika nchi mbalimbali, hali inayojionesha wazi kupitia hali ya chuki ambayo mara nyingi hutawala mijadala ya kisiasa na kijamii.
Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, “Kwa kuzingatia hali yetu ya kibinadamu iliyoanguka dhambini, ni rahisi sana kuwa na mtazamo wa uhasama dhidi ya wale tunaotofautiana nao. Hivyo basi, kunahitajika juhudi za makusudi ili kutafuta njia madhubuti za upatanisho na ujenzi wa udugu wa binadam Katika muktadha huu, Kristo Yesu anawaoesha njia nyingine, akifunua kuwa wema na upendo vina nguvu ya kuondoa uhasama na kuleta amani.”Kwa hiyo, Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru Maaskofu hawa kutoka Norway kwa uwepo na nia yao ya pamoja ya kutafuta njia za kujenga umoja na ushirikiano. Hakika, hata matendo madogo madogo yanaweza kuwapatia msukumo na kuwaongoza katika njia ya upatanisho. Baba Mtakatifu amewakumbushia Maaskofu hawa ile Sala ya Kristo Yesu, ya kuombea umoja miongoni mwa wafuasi wake akisema: “Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi.” Yn 17:23. Baba Mtakatifu amewataka Maaskofu hawa kujikita katika Sakramenti ya Ubatizo sanjari na Utume wao wa pamoja wa kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, wazidi kukua pamoja katika huduma ya kukuza haki na amani Ulimwenguni, kwa kutazama mifano hai ya Watakatifu kama vile: Olaf na Mtakatifu Sunniva. Walijiweka wakfu kwa Mungu na jirani, wakasaidia kuwaunganisha watu na kutoa ushuhuda wa kudumu kuhusu nguvu ya upendo inayoleta mabadiliko.
Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru tena Maaskofu kutoka Norway kwa ujio na ukarimu wao, na hatimaye, ameomba baraka za Mwenyezi mungu, ili ziwashukie na kukaa nao katika wema na hekima yake isiyokuwa na kikomo, awasaidie kuishi zaidi na zaidi kama ndugu wa kweli na hivyo kutangaza na kutoa ushuhuda wa pamoja kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa walimwengu.
