Tafuta

Picha ya Papa  Leo XIV wakati wa kutembelea Lampedusa akipitia mfano wa lango la kuingia Ulaya na Familia moja ya wakimbizi,Julai 4,2026. Picha ya Papa Leo XIV wakati wa kutembelea Lampedusa akipitia mfano wa lango la kuingia Ulaya na Familia moja ya wakimbizi,Julai 4,2026.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV:Watoto ndio kundi lililo hatarini zaidi katika harakati za uhamiaji duniani

Katika ujumbe wake wa Siku ya 112 ya Wahamiaji na Wakimbizi Duniani,Papa Leo XIV anatoa wito wa kuzuia kutengwa na kukataliwa,kuunda nafasi ili utambulisho wa kiutamaduni wa kila mtu uheshimiwe na kuzuia hatari ya itikadi kali."Kwa njia nyingi sana,hadhi za wahamiaji zinakanyagwa.Mateso ya watoto wahamiaji hayaishii kwenye kuhamishwa,wengi wameshuhudia vitendo vya ukatili visivyoelezeka na wametengwa na familia zao kwa muda mrefu."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika Ujumbe wa Papa ulitolewa tarehe 14 Agosti 2026 na Ofisi ya Vyombo vya Habari ya vya Kiti Kitakatifu katika fursa ya kuelekea Siku ya 112 ya Wahamiaji na Wakimbizi Duniani, ambayo Mama  Kanisa ataiadhimisha mnamo Septemba 27, Baba Mtakatifu  Leo XIV, amebainisha kuwa, “Kilio cha watoto waliohamishwa kinamfikia Mungu leo.”  Katika kilele cha siku hii kinaakisiwa na kauli mbiu: "Hata mmoja tu wa watoto hawa," kutoka Injili ya Mtakatifu Mathayo 18,10).

Watoto ndiyo kundi lililo hatarini katika harakati za kimataifa za uhamiaji

Baba Mtakatifu Leo XIV katika Ujumbe wake anaanza kwa kusisitiza kuwa hata kichwa cha ujumbe unavutia  umakini wetu kwa watoto wadogo wanaohusika moja kwa moja katika uzoefu wa uhamiaji na kukimbia, kwa utunzaji unaowastahili, na kwa ahadi ya Bwana kwamba "Yeyote akimpokea mtoto mmoja namna hii kwa jina langu anipokea Mimi"(Mk 9:37). Baba Mtakatifu alikumbusha kwamba watoto wadogo ndio kundi lililo hatarini zaidi katika harakati za kimataifa za uhamiaji. “ Mateso ya watoto wahamiaji hayaishii kwenye uhamisho wao.” Alikumbuka “watoto wadogo sana ambao wamepoteza wazazi, kaka, dada na marafiki, na ambao wameshuhudia vitendo vya vurugu visivyoelezeka; wengine ambao wametengwa na familia zao kwa muda mrefu; na watoto wadogo, hata kama wanafanya safari pamoja na wazazi wao, wakiwa katika hali mbaya na ya kutisha.”

Watoto wakabiliwa na matatizo ya biashara haramu na unyonyaji

Papa Leo XIV anakazia kusema kuwa, "hatuwezi kusahau hali mbaya ya wale waliotenganishwa na wazazi wao kwa sababu ya kurudishwa makwao." Katika hilo Papa anasikitishwa na  vifo vingi katika njia za uhamiaji; biashara haramu na unyonyaji; kuajiri watoto wadogo kwa ajili ya matumizi katika migogoro ya silaha; unyanyasaji wa kijinsia; ndoa za kulazimishwa; na ukatili walioupata au kushuhudia wakati wa safari zao. Heshima yao, inakanyagwa kwa njia nyingi."

Tunaitwa kufanya matendo ya kibinadamu

Baba Mtakatifu pamoja na hayo yote anatoa shukrani “kwa watu wengi, familia, taasisi za kiraia, na Jumuiya za Kanisa ambazo huchagua kutogeuza kisogo, badala yake hutoa mshikamano. Papa vile vile alielezea juu ya suala la idadi au takwimu. “Injili, inatualika kuwa tusihesabu hata mmoja. Kila mtoto, kila mwanadamu, ana heshima isiyo na kikomo." Mbele ya kila mtoto mhamiaji, tumeitwa kufanya kitendo cha ubinadamu na imani, kwani tunaweza kumkaribisha na kukutana na Bwana."

Umuhimu wa kuingilia kati nchi za asili,kuondoa sababu za kukimbia

Kwa kusikikitka zaidi Papa anabainisha kwamba, watoto wahamiaji hupuuzwa kwa urahisi zaidi, kwa sababu hawana watu wazima wenye uwezo wa kuwalinda na kuwasaidia. Kwa sababu hiyo ni muhimu kuingilia kati katika nchi zao za asili ili kuondoa sababu zinazowalazimisha kukimbia, huku wakitoa ulinzi na kuwakaribisha katika nchi za usafiri na unakoenda. Papa alikazia kuwa “Kilio cha watoto waliohamishwa kinamfikia Mungu leo, kama vile kilio kilichosikika katika Kitabu cha Kutoka, na kwamba  hatuwezi kubaki bila kujali, wala hatuwezi kuzoea mateso kama hayo.

Kulinda haki za msingi

“Katika maisha yetu binafsi, tunapaswa kufungua macho na mioyo yetu kwa kusikiliza kwa kina historia, hofu na ndoto, kushinda mgawanyiko huo unaompunguza mwanadamu kwa takwimu ambayo haituhusu moja kwa moja.” Papa ametoa mwaliko "kutambua hadhi ya kila mtoto, hata kabla ya kuzingatia hali ya kuwa mhamiaji, na kulinda haki zake za msingi: haki ya maisha, elimu na kiwango cha maisha kinachowezesha maendeleo kamili ya kimwili, kiakili, kiroho, kimaadili na kijamii."

Tubadilishe ukaribishaji dhahania hadi uzoefu thabiti wa kichungaji

“Katika maisha ya Kanisa, tumeitwa kubadilisha ukaribishaji kutoka dhana dhahania hadi mazoezi thabiti ya kichungaji.” Baba Mtakatifu alisema “hatuwezi kukabidhi kazi hii tu kwa taasisi au vyama vilivyopewa karama fulani. Mbele ya nyuso halisi zinazotukabili katika maisha ya kila siku, "jumuiya nzima ya Kikristo inaitwa kuwaona watoto hawa kama wana na binti zake, na kushiriki katika historia halisi ya kila mmoja wao,"Baba Mtakatifu alihimiza.

Jumuiya za Kikristo, zinapaswa kuhimizwa kukuza ujumuishaji wa wakimbizi na wahamiaji na kuwathamini kama wanachama kamili wa familia ya kikanisa. Hata mmoja tu wa watoto hawa, ndani ya upeo wa dini tofauti anatukumbusha kwamba udhaifu wa vijana haujui mipaka ya kidini na unatuunganisha katika jukumu la pamoja la kibinadamu na kiroho." Papa alisisitiza kwamba hii inakuwa msingi mzuri wa mazungumzo halisi ya kidini, ambapo waumini, wakitegemea hisia zao za kupita kiasi, wanashirikiana katika kuunganisha mitandao ya ulinzi.

“Jumuiya za imani, zimeitwa kuunda nafasi ambapo kila mvulana na kila msichana anaheshimiwa na kuthaminiwa katika utambulisho wake wa kiutamaduni, na hivyo kuzuia hatari ya misimamo mikali na vikundi vyenye msimamo mkali. Hata mmoja tu wa watoto hawa, katika muktadha wa taasisi za kiraia, anatuita kuthibitisha kanuni ya maslahi bora ya mtoto. Papa alitoa  wito kwa taasisi za umma na za kibinafsi, ambazo zinalazimika kutanguliza ulinzi na utu wa kila mtoto na kijana kwamba “Hii inahitaji kupitishwa kwa vyombo vya kisheria vya ulinzi, kukuza umoja wa familia, na kuzuia kiwewe kinachosababishwa na kutengana.

Mabadiliko ya haraka ya mtazamo yanahitajika

Katika lengo la mjadala lazima libadilike kutoka katika usimamizi tu wa uhamiaji hadi ulinzi kamili na wa haraka wa haki za binadamu, kupitisha jibu lililoratibiwa, la kuunga mkono na lenye ufanisi, lenye uwezo wa kuhakikisha ulinzi, kukaribishwa na fursa za kweli za kuunganishwa kwa wale wanaohama.

Baba Mtakatifu Leo XIV alihitimisha na sala kwa kuwakabidhi watoto wahamiaji na wakimbizi kwa ulinzi wa Mama Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu na mtoto Yesu waliopata kimbilio huko Misri: “Tunawakabidhi watoto wahamiaji na wakimbizi chini ya ulinzi wa Mama wa Maria Mtakatifu sana ambaye, pamoja na Mtakatifu Yosefu na mtoto Yesu, walipitia ukatili wa vurugu za Herode na mkasa wa uhamishoni Misri (taz. Mt 2:13-15). Aasindikize nyayo zao na kuzisaidia Jumuiya zetu kuwa ishara hai na za kuaminika za Injili.

Ujumbe wa Papa Leo XIV wa Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.

 

14 Agosti 2026, 16:10