Tafuta

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle anasema, watu wa Mungu nchini DRC., wanaitwa na kualikwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu ili kuyatakatifuza malimwengu. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle anasema, watu wa Mungu nchini DRC., wanaitwa na kualikwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu ili kuyatakatifuza malimwengu.  (Foto dalla pagina FB di UCS-Goma)

Kardinali Luis Tagle: Ujumbe kwa Watu wa Mungu Goma, DRC

Katika mahubiri yake amewasilisha salam na matashi mema ya Baba Mtakatifu Francisko kwa watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Goma; amegusia maisha na utume wa Mtakatifu Anthony wa Padua na mwishoni amewataka watu wa Mungu Goma kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu ili kuyatakatifuza malimwengu kwa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Amewasilisha pia salam za Baba Mtakatifu Francisko anayewakumbuka kwa sala na sadaka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya 40 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC kuanzia tarehe 31 Januari 2023 hadi tarehe 3 Februari 2023 ilinogeshwa na kauli mbiu “Wote wapatanishwe katika Yesu Kristo.” Baba Mtakatifu alikuwa ametia nia ya kutembelea mji wa Goma, ili kushuhudia mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu katika eneo hili, lakini haikuwezekana kutokana na sababu za ulinzi na usalama. Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alimteuwa Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu kuwa mwakilishi wake maalum katika Maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa, kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 11 Juni 2023, huko Lubumbashi, nchini DRC., sanjari na maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu, “Corpus Christi.” Mahubiri yake yalinogeshwa na kauli mbiu “Ekaristi Takatifu na Familia”; amejikita zaidi katika umuhimu wa chakula jangwani; matamanio halali ya binadamu; Kristo Yesu ni chakula kilichoshuka kutoka mbinguni; Ekaristi Takatifu na maisha ya kifamilia, kumbukumbu hai na endelevu katika tunu msingi za maisha ya kifamilia. Jumanne tarehe 13 Juni 2023 katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mtakatifu Anthony wa Padua, Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Parokia ya Bibi Yetu wa Mlima Karmeli, Jimbo Katoliki la Goma, nchini DRC. Katika mahubiri yake amewasilisha salam na matashi mema ya Baba Mtakatifu Francisko kwa watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Goma; amegusia maisha na utume wa Mtakatifu Anthony wa Padua na mwishoni amewataka watu wa Mungu Goma kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu.

Watu wa Mungu wanaitwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu
Watu wa Mungu wanaitwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu

Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Anthony wa Padua alizaliwa tarehe 15 Agosti 1195 huko Lisbon nchini Ureno. Katika umri wa ujana wake, alijisadaka sana kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Mtakatifu Anthony wa Padua alikuwa ni mtu wa sala na tafakari ya kina katika maisha yake, kiasi cha kuwavuta watu wengi kufanya toba na wongofu wa ndani. Alifariki dunia tarehe 13 Juni 1231, akiwa na umri wa miaka 35 tu, matendo makuu ya Mungu. Papa Gregori wa IX, hapo tarehe 30 Mei 1232, akiwa mjini Spoleto, Italia akamtangaza kuwa Mtakatifu. Tarehe 16 Januari 1246 Papa Pio XII akamtangaza kuwa Mwalimu wa Kanisa “Doctor Evangelicus” yaani “Mwalimu wa Injili”. Hii ni kutokana na amana na utajiri uliokuwa unabubujika kutoka katika mahubiri yake yaliyokuwa yanapata chimbuko lake katika Injili. Ibada kwa Mtakatifu Antony wa Padua imeenea sehemu nyingi za dunia. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle anasema, watu wa Mungu nchini DRC., wanaitwa na kualikwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu, ili kukoleza ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Chumvi hufanya kazi ya kutakasa, kuhifadhi vitu visioze na inasaidia kukoleza ladha ya chakula. Watu wengi eneo la Goma, kimsingi maisha yao hayana ladha.

Ushuhuda wa imani katika matendo adili na manyoofu
Ushuhuda wa imani katika matendo adili na manyoofu

Lakini Kristo Yesu anawaalika watu wa Mungu nchini DRC kukoleza maisha yao kwa ladha inayo bubujika kutoka kwa Kristo Yesu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Kwa njia ya huruma, upendo, unyenyekevu na huduma kwa njia ya Kristo Yesu, watu wengi zaidi watapata na kuonja maana mpya ya maisha; kwani watu wote wa Mungu wanaitwa na kuhimizwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu mjini Goma. Katika mchakato huu, kinachoangaliwa ni “huduma kwa watu wengine.” Hii ndiyo chumvi na nuru ya unyenyekevu, chemchemi ya imani, matumaini na mapendo! Kwa wananchi wa Goma wanapitia hali tete ya maisha, kiasi cha kushindwa kufahamu ni wapi pa kukimbilia. Hii inatokana na ukweli kwamba, wale watu waliopaswa kuwa ni chumvi na nuru wamekengeuka! Ikumbukwe kwamba, Kristo Yesu ndiye nuru ya Mataifa, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa ni mashuhuda amini wa maisha na utume wa Kanisa; kwa njia ya faraja, ukarimu na mapendo thabiti na kwa njia hii, matumaini yanaweza kuchanua miongoni mwa watu wa DRC. Kristo Yesu ataendelea kuwa ni chumvi na mwanga wa Mataifa; changamoto na mwaliko wa kushikamana na Kristo Yesu ili kuyatakatifuza malimwengu, kwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha haki, amani, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kristo Yesu chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu, asaidie kukoleza moyo wa uponyaji, sadaka na majitoleo kwa ajili ya wale waliojeruhiwa. Kama nuru ya ulimwengu, waamini wanapaswa kusimama kidete katika misingi ya ukweli, msamaha na upatanisho wa Kitaifa; ili kukoleza na kudumisha amani kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.

Kardinali Tagle Goma

14 June 2023, 16:00