Tafuta

2023.10.13  Kardinali Ambongo, Askofu Mkuu wa Kinshasa ameongoza misa takatifu katika kanisa Kuu la Mtakatifu petro mjini Vatican kwa washiriki wa Sinodi. 2023.10.13 Kardinali Ambongo, Askofu Mkuu wa Kinshasa ameongoza misa takatifu katika kanisa Kuu la Mtakatifu petro mjini Vatican kwa washiriki wa Sinodi.  (Vatican Media)

Kard.Ambongo,Unabii wa Yoeli unafanana na uzoefu wa Sinodi tunayofanya sasa

Tukiwa tunatoka katika mabara yote na kuunganishwa katika familia moja,katika uzuri huu wa umoja katika utofauti wa kiutamaduni,tunaalikwa pia kulia na kuomboleza mbele ya madhabahu haya,kwenye kaburi la Mtakatifu Petro,kwa sababu ya udhaifu wetu kama Kanisa.Amesema hayo katika mahubiri Kardinali Ambongo.

Na Angella Rwezaula, Vatican

Ijumaa tarehe13 Oktoba 2023, washiriki wa Sinodi wameshirik Ibada ya Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, kwa kuongozwa na Kardinali Fridolin Ambongo, Askofu Mkuu wa Kinshasa, DRC. Katika mahubiri yake kwa kuongozwa na masomo ya  siku na muktadha wa Sinodi inayoendelea, ameanza na kifungu cha Zaburi, kisemacho ,"Kwa moyo wangu wote, Bwana, nataka kukusifu na kuziimba kazi zako zote za ajabu" (Zaburi 9). Zaburi ya kiitikio ya leo inatualika kumshukuru Mungu; na tunazo sababu nyingi za kumshukuru Mungu. Moja ya sababu bila shaka ni neema ya njia hii ya sinodi, ambayo tunasafiri kama Kanisa, tukiongozwa na Roho Mtakatifu.

Washriki wa Sinodi katika Misa kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro
Washriki wa Sinodi katika Misa kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro

Sinodi hii ya kisinodi ni Pentekoste mpya, ambayo kwa hakika italifanya upya Kanisa katika ushirika wa washiriki wake na katika ushiriki hai wa wote katika maisha na utume wa Kanisa. Ndiyo, Kanisa lilihitaji wakati huu wa neema na utambuzi, wakati wa kutazama nyuma kwenye njia ambayo tumesafiri, pamoja na utukufu wake na kushindwa kwake, ili kujifunza kutoka kwayo kuwa mwanzo mpya. Katika somo la kwanza, nabii Yoeli anawaalika makuhani, wahudumu wa madhabahu, kulia na kuomboleza kwa sababu matoleo na majitoleo ya kinywaji yametoweka katika nyumba ya Mungu. Anawashauri mapadre kuwaleta pamoja wazee ili kujifunza na kutafuta pamoja njia mpya za kujionesha mbele za Mungu.

Waliotumikia Misa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Peto 13 Oktoba 2023 ni waseminari wa Urbaniana
Waliotumikia Misa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Peto 13 Oktoba 2023 ni waseminari wa Urbaniana

Unabii huu wa Yoeli unalingana kwa kiasi fulani na uzoefu wa sinodi ambao tunapitia siku hizi hapa Roma. Tukiwa tunatoka katika mabara yote, na kuunganishwa katika familia moja, katika uzuri huu wa umoja katika utofauti wa kiutamaduni, tunaalikwa pia kulia na kuomboleza mbele ya madhabahu haya, kwenye kaburi la Mtakatifu Petro, kwa sababu ya udhaifu wetu kama Kanisa. Hakika, kama chombo  chetu kitendea kazi kinatukumbusha: “Uso wa Kanisa leo una dalili za machafuko makubwa ya imani na uaminifu. Katika mazingira mengi, migogoro inayohusishwa na unyanyasaji wa kijinsia, matumizi mabaya ya mamlaka, matumizi mabaya ya dhamiri na unyanyasaji wa kiuchumi, na mengine (IL,23), shuhuda za kupingana ambazo zilihatarisha kuwatenga watu kutoka kwa Kanisa. Kardinali Ambongo amesema , tuko hapa kulia na kumwomba Mungu atusamehe dhambi zetu. Lakini njia bora ya kulia ni ujasiri wa kuchukua njia ya toba na wongofu, ambayo inafungua njia za upatanisho, uponyaji na haki (IL, 23).

Misa takatifu kwa washiriki wa Sinodi
Misa takatifu kwa washiriki wa Sinodi

Kardinali akitazama Injili amesema,- Injili ya leo inahusu mapambano ya Yesu dhidi ya shetani. Inatukumbusha kwamba shetani bado yuko na anafanya kazi katika ulimwengu wetu. Nguvu zake ziko hasa katika mkakati wa kusahaulika na kuonekana katika aina za kuvutia zaidi na za kutia moyo. Akijua mawindo yake vizuri, shetani anazindua mashambulizi yake kutoka kwa ukweli nyeti zaidi. Kama Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita alivyosema, "Mwovu daima anataka kuharibu kazi ya Mungu kwa kupanda utengano ndani ya moyo wa mwanadamu, kati ya mwili na roho, kati ya mtu binafsi na Mungu, katika mahusiano ya kibinafsi, kijamii na kimataifa. Mwovu hupanda fitina. Kwa njia hiyo Kardinali amesema kwamba, ikiwa tutakuwa na ujasiri wa kutazama ukweli wetu wa sasa kama Kanisa, haitakuwa vigumu kuona ni kwa kiwango gani yule Mwovu anafanya kazi na kuathiri namna yetu ya kuwa na kutenda.

Ibada ya Misa 13 Oktoba 2023 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro
Ibada ya Misa 13 Oktoba 2023 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro

Kardinali Ambo amesisitiza kuwa Yule Mwovu anayetaka kuona tumegawanyika, anaweza hata kututumia baadhi yetu kwa ajili yake. Ndiyo maana ni lazima tupigane na yule Mwovu kwa ujasiri, tukitumia hasa silaha za sinodi, zinazohitaji umoja, kutembea pamoja, utambuzi katika sala, kusikilizana na yale ambayo Roho anatuambia. Tumeitwa kupigana na adui huyu mwenye nguvu na silaha yenye nguvu sawa tuliyo nayo, ambayo ni Roho Mtakatifu, mhusika mkuu wa njia hii mpya ya kuwa Kanisa - Kanisa la sinodi. Ekaristi tunayoitoa hapa kwenye kaburi la Petro itufungue ili kumsikiliza Roho Mtakatifu. Lisogeze Kanisa la Sinodi kutoka kwenye ndoto hadi uhalisia, kutoka kwa maneno hadi maisha halisi ambapo tutaweza kutembea pamoja katika ushirika, ushiriki na utume.

Mahubiri ya Kardinali Ambongo 13 Oktoba 2023
13 October 2023, 09:44