Tafuta

Nembo ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kimataifa huko Quito nchini Equador kuanzia 8 hadi 15 Septemba 2024. Nembo ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kimataifa huko Quito nchini Equador kuanzia 8 hadi 15 Septemba 2024. 

Rais wa Kamati ya Kipapa ya Makongamano ya Ekaristi Kimataifa yuko Ecuador

Mambo yameanza kutimua vumbi na jasho katika maandalizi ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa,litakalofanyika kuanzia 8 hadi 15 Septemba 2024 huko Quito,Ecuador.Ni katika muktadha huo ambapo Rais wa Kamati ya Kipapa ya maandalizi amefika jijini humo kwa mara ya tatu katika maandalizi haya miezi mitano kabla ya tukio hilo muhimu.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kwa hamasa kubwa na utamu unaomtambulisha, Padre Corrado Maggioni, Rais wa Kamati ya Kipapa ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu ya Kimataifa, aliwasili  mnamo tarehe 4 Aprili 2024  katika mji mkuu wa Ecuador akitokea Roma. Mwakilishi huyo wa Vatican aliwasili kwa madhumuni ya kuwasindikiza  na kuhimiza shirika la  maandalizi ya Kongamano la 53 Kimataifa la Ekaristi (IEC 2024,) lililopangwa kufanyika jijini  Quito kuanzia tarehe 8 hadi 15  Septemba 2024. Katika siku zake za kwanza katika Equador, alitembelea vituo vya Kongamano la 53 la Ekaristi na Curia ya Mji Mkuu wa Quito. Alifanya mkutano na Askofu Mkuu Alfredo José Espinoza Mateus, wa Jimbo Kuu Katoliki la  Quito, na rais wa Kamati mahalia ya IEC 2024.

Na  kauli mbiu itakayaoongoza Kongamano hilo ni: “Fraternidad para sanar el mundo”, yaani: “Udugu kwa ajili ya kuponesha ulimwengu ambayo inatokana na neno la Kiinjili lisemalo: “Ninyi nyote ni ndugu” (Mt 23,8). Ishara hiyo  inakumbusha uzoefu wa sasa wa kisinodi wa Kanisa, ambalo linaalika kugeuka kuwa mahali  pa udugu wa ujumuishi, na uwepo wa kushirikisha na ukarimu wa kina.

https://www.vaticannews.va/sw/vatican-city/news/2023-05/kongamano-la-ekaristi-takatifu-huko-quito-equador.html

Msamaha wa kuponya moyo

Kutoka katika Tovuti iliyoandaliwa kwa ajili ya tukio hili la Quito 2024 inabainishwa kuwa “ Katika mahojiano yaliyofanyika kwa ajili ya kipindi cha “Udugu wa Kuponya Ulimwengu”, Padre Maggioni alieleza furaha yake ya kuwa nchini Ecuador, nchi iliyowekwa wakfu kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu miaka 150 iliyopita,  na ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko aliichagua kuwa makao makuu ya Kongamano la 53 la Ekaristi. Kadhalika, aliakisi juu ya thamani ya msamaha ili kuponya moyo wa mwanadamu, kuepusha huzuni na kutangaza habari njema ya Injili kwa furaha.”

Akimzungumzia  Mama Maria, mama wa Kanisa, alitaja kuwa uwepo wake ni wa msingi katika Kongamano kwani ndiyo Tabernakulo ya kwanza ya Kristo, inayoongoza watoto wake kwenye Ekaristi. Yeye ndiye mama anayetualika kuishi umoja, upendo na udugu. Hata hivyo Padre Corrado atashiriki Ibada ya Ekaristi Takatifu ya kuabdhimisha miaka 150  tangu  kuwekwa wakfu kwa Ecuador kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, inayotarajiwa kufanyika tarehe 10 Aprili 2024 saa 6:00 mchana  katika Basilika ya Nadhiri ya Kitaifa, ambapo uwepo wa mamlaka ya kitaifa unatarajiwa pia.

Ziara ya tatu kwa Ecuador

Ni kwa mara ya tatu kwa rais wa Kamati ya Kipapa ya Makongamano ya Ekaristi ya Kimataifa kutembelea nchini Equador, ya kwanza ilikuwa mwezi Novemba 2022; ya pili mnamo Septemba 2023, kuhusu Mkutano Mkuu wa Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu la Kimataifa, ambapo wajumbe kutoka Mabaraza ya Maaskofu wa nchi mbalimbali duniani walishiriki. Ikiwa ni miezi mitano imebaki ya  mkutano mkuu wa Kanisa, basi Kongamano hilo linaandiliwa vizuri na Kamati mahalia ya Kongamano la  Ekaristi Takatifu la kimataifa(IEC 2024.)

Padre Maggioni alizaliwa mjini Bergamo-Italia, akapewa daraja la Upadre wa Wamissionari wa Shirika la Maria, ana daktari wa Liturujia kutoka Taasisi ya Kipapa ya Liturujia ya Mtakatifu Anselm, Roma. Amehudumu mjini Vatican kwa miaka 34. Mnamo mwaka 2014, Baba Mtakatifu Francisko alimteua kuwa Katibu Msaidizi wa  Baraza la Kipapa na  Ibada na Nidhamu ya Sakramenti na mwaka 2021 akamteua kuongoza Kamati ya Kipapa ya Makongamano ya Kimataifa ya Ekaristi, akichukua nafasi ya Askofu Piero Marini, ambaye amekuwa mwenyekiti wake tangu mwaka 2007. Kwa habari nyingine zaidi unaweza kutembea tovuti iliytayarishwa kwa ajili ya tukio hili:https://www.iec2024.ec/en/presidente-comite-visita-ecuador/.

Wimbo wa Kongamano la Ekaristi Takatifu huko Quito, Equador

Ikumbukwe tarehe 10 mei 2023  katika Makao makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Equador waliwakilisha Nembo na Wimbo Rasimi wa Kongamano hilo. Katika Nembo hiyo unaonekana Msalaba, Moyo, Ekaristi na mji Mkuu wa Nchi hiyo. Kwa habari zaidi zinazohusiana na tukio hilo zinaweza zinapatikana katika mtandao wa Kamati ya Maandalizi:(www.iec2024.ec) na Tume ya Kipapa kwa ajili ya Makongamano ya Ekaristi Kimataifa: (www.congressieucaristici.va).

Kongamano la Ekaristi Takatifu Kimataifa huko Ecuadoro 8-15 Septemba 2024

 

06 April 2024, 12:02