Tafuta

Jubilei ya Miaka 25 ya maisha, wito, utume na zawadi ya Daraja Takatifu, Padre Paul Innocent Maria Kaigalura, O. Carm., tarehe 15 Septemba 2024, kwenye Madhabahu ya Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Napoli, Italia Jubilei ya Miaka 25 ya maisha, wito, utume na zawadi ya Daraja Takatifu, Padre Paul Innocent Maria Kaigalura, O. Carm., tarehe 15 Septemba 2024, kwenye Madhabahu ya Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Napoli, Italia 

Padre Paul Innocent Maria Kaigalura, Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre!

Ni katika muktadha wa Jubilei ya Miaka 25 ya maisha, wito, utume na zawadi ya Daraja Takatifu, Padre Paul Innocent Maria Kaigalura, O. Carm., tarehe 15 Septemba 2024, kwenye Madhabahu ya Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Napoli, Italia, amemwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya maisha na wito wa Kipadre. Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na Askofu Filippo Iannone, O. Carm., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Sheria za Kanisa ! Wito wa Upadre!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Jubilei ni wakati uliokubalika wa kumwangalia Kristo Yesu, ili kutafakari kwa kina na mapana changamoto anayotoa kwa Wakleri wake katika mchakato wa kumwilishwa huruma na upendo wa Mungu katika sera na mikakati yao ya shughuli za kichungaji. Ni muda wa kufanya toba na kuomba msamaha; kusifu, kushukuru na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya maisha na wito wa Kipadre, bila kusahau wema na ukarimu anaoendelea kuwatendea Watumishi wa Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma kwa waja wake. Yote haya yanadhihirisha wema na huruma ya Mungu kwa Wakleri wake hata kama wakati mwingine wanaelemewa na udhaifu wao wa kibinadamu, lakini bado Mwenyezi Mungu anaendelea kubaki kuwa mwema na mwaminifu kwa ahadi zake. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja takatifu ya Upadre ni muda uliokubalika wa kupyaisha maisha na utume wao, tayari kunukia ile harufu ya Kondoo wao, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia ukuu, wema, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, ili kweli Wakleri waweze kuwa na ari na nguvu mpya, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake.

Padre Paulo Innocent Maria Kaigalura Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre
Padre Paulo Innocent Maria Kaigalura Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre

Ni katika muktadha wa Jubilei ya Miaka 25 ya maisha, wito, utume na zawadi ya Daraja Takatifu, Padre Paul Innocent Maria Kaigalura, O. Carm., tarehe 15 Septemba 2024, kwenye Madhabahu ya Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Napoli, Italia, amemwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya maisha na wito wa Kipadre. Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na Askofu Filippo Iannone, O. Carm., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Sheria za Kanisa “Dicasterium De Legum Textibus.” Katika mahubiri yake, alikazia umuhimu wa waamini kumfahamu fika Kristo Yesu, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu, tayari kumkiri na kuanza kumfuasa kwa sadaka ya maisha na uaminifu kwa upendo wake usiokuwa na kifani. Hii ni changamoto ya kumwilisha imani katika matendo adili na matakatifu, kama ilivyokuwa sadaka ya Kristo Yesu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Katika kipindi cha miaka 25 Padre Paul Innocent Maria Kaigalura, Mkarmeli, O. Carm., amejitahidi kuiishi, kuhifadhi na kuwashirikisha wengine imani yake kwa Kristo Yesu. Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu aliyewaita na hatimaye, akawachagua Mitume kumi na wawili, akawatuma kushiriki maisha na utume wake, hata Padre Paul ameitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na kwamba, Kristo Yesu ni zawadi kubwa ya Baba kutoka mbinguni, changamoto na mwaliko kwa Mapadre kubaki katika maisha, utume na upendo wao kwa Kristo Yesu, kwani bila Kristo Yesu, hakuna linaloweza kufanyika.

Mama Modesta Kaigalura ameshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu
Mama Modesta Kaigalura ameshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu

Padre anateuliwa miongoni mwa watu wa Mungu ili kuzaa matunda kwa njia ya ushuhuda wa maisha, huku wakitambua kwamba, zawadi, maisha na utume wa Kipadre umehifadhiwa katika hazina ya udongo. Kumbe, Padre anapaswa kufuata njia ya Kristo, kutafakari, kujifunza na kumwilisha Neno la Mungu chemchemi ya furaha ya maisha, kielelezo makini cha imani thabiti na yenye nguvu. Imani inaboreshwa kwa njia ya: Maisha ya sala binafsi na zile za kijumuiya; Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa sanjari na kuendelea kujikita katika ujenzi wa upendo na ushirika na Kristo Yesu. Changamoto kubwa kwa Mapadre kwa wakati huu ni kushiriki kikamilifu katika kujenga na kudumisha upendo na ushirika na Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake na hivyo kuendelea kuwa ni mashuhuda waaminifu wa upendo na ushirika wa Kipadre. Miaka 25 ya maisha na wito wa Kipadre ni kipindi ambacho kimesheheni furaha, machungu na mafanikio ya kuzima kiu na njaa ya watu kukutana na Mwenyezi Mungu. Ibada ya Misa Takatifu imehudhuriwa na Mama Modesta Kaigalura pamoja familia yake, akabahatika kuwa ni kati ya waamini waliopeleka mapaji Altareni. Mama Modesta anasema, wanatoka Parokia ya Buyango, Kigango cha Kabashana, hiki ni Kijiji maarufu sana Jimbo Katoliki la Bukoba, lakini kwa miaka mingi wameishi Parokia ya Mtakatifu Francisko Xsaveri, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Jubilei ya Miaka 25 yenye changamoto, magumu na furaha ya Daraja Takatifu
Jubilei ya Miaka 25 yenye changamoto, magumu na furaha ya Daraja Takatifu

Mama Modesta anasema, Padre Paul Innocent Maria Kaigalura, O. Carm., alizaliwa tarehe 18 Februari 1970 kwenye Hospitali ya Ocean Road, enzi hizo. Baada ya malezi na majiundo yake ya maisha ya kitawa, tarehe 10 Septemba 1995 akaweka nadhiri zake za kwanza na zile za daima akaweka tarehe 9 Desemba 1998 na hatimaye, tarehe 12 Septemba 1999 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kumbe, ni Mtoto wake anayemfahamu fika. Tangu mwanzo kabisa mwa maisha yake alionesha upendo mkubwa kwa Kanisa na masomo. Alikuwa ni Mtumishi wa Altare, na baadaye akawa ni mwalimu wa watumishi wa Altare. Tangu utotoni, Padre Paul Innocent Maria Kaigalura, O. Carm., alikuwa “shapu shapu” hadi leo hii hajabadilika sana. Mama Modesta anapenda kumshukuru Mungu kwa kumwezesha mtoto wake Paul kuwa Padre kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani zake. Wito kwa wazazi na walezi waendelee kuwatia shime watoto wao wanaoonesha nia na karama za kumtumikia Mungu, kama Mapadre na Watawa wasiwakatishe tamaa bali wawatie moyo. Ikumbukwe kwamba, miito inapata chimbuko lake kutoka katika Kanisa na kupapaliliwa katika Jumuiya ndogondogo za Kikristo, changamoto na mwaliko wa kukuza na kudumisha imani, matumaini na mapendo ndani ya familia na katika Jumuiya ndogondogo za Kikristo, ili Kanisa liweze kupata watenda kazi waaminifu na watakatifu.

Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa
Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa

Padre Paul Innocent Maria Kaigalura, O. Carm., katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, katika maisha na wito wake kama Padre amekumbana na changamoto nyingi na hizo zimekuwa ni fursa ya kukua na kukomaa katika maisha ya Kijumuiya, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu na Kristo Yesu. Neno la Mungu daima limekuwa ni taa na mwongozo wa maisha yake; Maisha ya sala kwa kujikabidhi na kujiaminisha mbele ya Mungu pamoja na maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa ibada na uchaji; kwa unyenyekevu na uvumilivu na tafakari ya kina pasi na haraka ya maisha! Sherehe ya Jubilei ya Miaka 25 ya Maisha na Wito wa Padre Paul Innocent Maria Kaigalura, O. Carm., yalifana sana, hasa kuona umati mkubwa watu wa Mungu wakitokwa na machozi ya furaha kwa hatua hii kubwa ya maisha na wito wake wa Kipadre. Ila tu, Sherehe haikunoga saaaana kutokana na Kikapu cha Senene, Matoke na Rubisi kushindwa kuwasili kwa wakati! Lakini ya Mungu mengi yote tisa kumi ni Sherehe hizi zitakapokamilishwa Jimboni Bukoba!

Jubilei Padre Paulo
18 September 2024, 13:24