Uwasilishaji wa Jubilei ya Wasanii:Sanaa inahuisha tumaini!
Vatican News
Ni mkutano wa kimataifa wa kweli ambao unawaleta pamoja zaidi ya wajumbe elfu saba, kutoka mataifa zaidi ya 60 katika mabara matano. Ndivyo basi, Kardinali Tolentino de Mendonca, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu, aliwasilisha Jumatano tarehe 12 Februari 2025 katika Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Vatican Matukio mbalimbali ya Jubilei ya Ulimwengu wa Wasanii na Wanamichezo itakayoadhimishwa mjini Roma kuanzia tarehe 15 hadi 18 Februari 2025. Kwa njia hiyo Kardinali alieleza kuwa “Changamoto madhubuti ni kuunda fursa za ubunifu zinazoruhusu kila mtu, na kila mmoja, kufufua matumaini,
De Mendonça: Matumaini sio nyongeza
Matumaini ni uzoefu wa kimataifa wa kianthropolojia, ambao hugusa moyo wa kila utamaduni, na ambao unatoa uwezekano wote wa mazungumzo," Kardinali alisisitiza. Katika Hati ya kutangaza Jubilei (Bolla di indizione Spes non confundit), Papa Francisko alieleza kuwa, “Mwaka Mtakatifu 2025 uwe fursa kwa ajili ya kuhuisha tumaini, matukio ya Jubilei hii lazima yatusaidie kuiweka katikati ya nafasi ya umma kama mada kuu ya kiutamaduni, kama nyenzo muhimu na yenye nguvu ya pamoja ambayo lazima tuwekeze zaidi na zaidi. Kwa hivyo, ni hitaji la msingi na sio nyongeza tu. Ni lazima tujiulize jinsi urithi wa kiutamaduni wa dini unavyoweza kuwa msambazaji hai wa matumaini kwa vizazi vipya na jinsi sanaa ya kisasa inaweza kutoa tumaini.”
Saini katika Makumbusho ya Vatican
Katika siku za Jubilei hii, washiriki wataalikwa kupita katika Mlango Mtakatifu jioni ya Dominika tarehe 16 Februari 2025 na kwa ratiba tajiri ya mipango ambayo itafunguliwa Jumamosi tarehe 15 Februari, kwa kushiriki katika Mkutano wa Jubilei ya Papa na mkutano wa kimataifa ukiongozwa na mada: “Kushiriki matumaini kwa Urithi wa eneo la Kiutamaduni.” Tukio hili likiwa limeandaliwa kwa ushirikiano na Makumbusho ya Vatican, litawaleta pamoja wakuu wa baadhi ya taasisi maarufu za kisanii na makumbusho duniani ambao watachunguza lugha na mikakati mipya ya kuthaminisha na kusambaza urithi wa kidini na kisanii. Mazungumzo yao yatapelekea kutiwa saini kwa Ilani ya kielimu juu ya uwasilishaji wa kanuni za kiutamaduni za dini, bila kwayo, Kardinali de Mendonça alisisitiza kuwa “utamaduni unabaki kuwa duni usioweza kurekebishwa.”
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa Jumba la Makumbusho ya Vatican, Profesa Barbara Jatta alieleza kuwa: “Tulitaka sana Jubilei hii iwe ya kujitolea sio tu kwa wasanii bali pia kwa wale wanaofanya kazi katika ulimwengu wa sanaa ambao jukumu lao ni muhimu katika usambazaji wa kanuni za kidini, mila, imani na sanaa yenyewe. Makumbusho ya Vatican yanatambua thamani ya wale wote ambao, kwa kueneza na kufundisha, wanahifadhi na kusambaza urithi huu na Jubilei hii ni ishara ya shukrani.”
Kwa mara ya kwanza Papa atatembelea Cinecittà
Tukio la kilele la Jubilei ya Wasanii na wanamichezo litakuwa Jumatatu tarehe 17 Februari 2025, wakati ambapo Papa Francisko anatarajia kutembelea studio za filamu(Cinecittà)jijini Roma: kwa mara ya kwanza kama Papa. Katika roho ya Jubilei, Papa Francisko atakutana na wajumbe wa wasanii na wahusika wakuu kutoka katika ulimwengu wa utamaduni, lakini pia wafanyakazi wa Cinecittà na familia zao, kwa jumla ya watu mia saba. Pia wanatarajiwa watengenezaji filamu wa kimataifa kama vile Tornatore, Burton, Ferrara, Bellocchio, na waigizaji kama vile Monica Bellucci, Pierfrancesco Favino, Toni Servillo na Sergio Castellitto. Chaguo la Papa la kukutana na wale wanaotajirisha macho na roho ya kila mmoja wetu kwa kazi zao za kisanii na talanta yao linawakilisha utambuzi mkubwa wa thamani ya sanaa ya saba na mchango unaotolewa kwa jamii na wahusika wakuu wa ulimwengu wa utamaduni,” alisema Naibu Waziri wa Utamaduni wa Jamhuri ya Italia, Lucia Borgonzoni.