Tafuta

Jimbo Katoliki la Bagamoyo limezinduliwa rasmi tarehe 4 Mei 2025 kisha Askofu Stefano Lameck Musomba OSA kusimikwa rasmi kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo Jimbo Katoliki la Bagamoyo limezinduliwa rasmi tarehe 4 Mei 2025 kisha Askofu Stefano Lameck Musomba OSA kusimikwa rasmi kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo  (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Askofu Stephano Musomba, OSA., Jimbo Katoliki la Bagamoyo! Kumekucha!

Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Bagamoyo ni la Moyo Safi wa Bikira Maria na kwamba, Jimbo Katoliki la Bagamoyo limezinduliwa rasmi tarehe 4 Mei 2025 kisha Askofu Stefano Lameck Musomba OSA kusimikwa rasmi kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo. Maadhimisho hayo yalifanyika katika Viwanja vya Bagamoyo ambapo Askofu mkuu Angelo Accattino, Balozi wa Vatican nchini Tanzania alisoma hati maalumu kutoka kwa Hayati Papa Francisko

Na Sarah Pelaji, - Vatican.

Mnamo tarehe 7 Machi 2025, Hayati Baba Mtakatifu Francisko aliunda Jimbo Katoliki la Bagamoyo, kwa kuligawa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na Jimbo la Morogoro na kumteua Askofu Stephano Lameck Musomba, OSA, kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo. Kabla ya uteuzi huu, Askofu Stephano Lameck Musomba, OSA alikuwa ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Bagamoyo ni la Moyo Safi wa Bikira Maria na kwamba, Jimbo Katoliki la Bagamoyo limezinduliwa rasmi tarehe 4 Mei 2025 kisha Askofu Stefano Lameck Musomba OSA kusimikwa rasmi kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo. Maadhimisho hayo yalifanyika katika Viwanja vya Bagamoyo ambapo Askofu mkuu Angelo Accattino, Balozi wa Vatican nchini Tanzania alisoma hati maalumu kutoka kwa Hayati Baba Mtakatifu Francisko ya kutambulisha rasmi uteuzi wa jimbo jipya la Bagamoyo na ya uteuzi wa Askofu Msomba kuwa Askofu wa Jimbo jipya Katoliki Bagamoyo ili kuhalalisha uzinduzi wa jimbo na askofu wa jimbo hilo jipya.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC   (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi, OFMCap., wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam, ndiye aliyeongoza madhehebu ya kumsimika Askofu Musomba katika kiti cha Kiaskofu cha Jimbo Katoliki Bagamoyo. Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S., wa Jimbo Katoliki Morogoro, katika mahubiri yake, amemshukuru Hayati Baba Mtakatifu Francisko kukubali kuipa Bagamoyo hadhi ya kuwa na kiti cha kiaskofu ikiwa ni sehemu ya kihistoria ya imani ya Kanisa Katoliki Afrika Mashariki. Amesema jukumu ambalo Jimbo Jipya Katoliki Bagamoyo linapewa ni kuendelea kuwavua watu yaani kuwatoka katika wimbi la dhambi na kuwakomboa ili watoke kwenye vifungo vya dhambi wapate uhuru wa kumpenda Mungu wao na kuishi kwa furaha. Amemsihi Askofu Musomba kunedelea kuwa mwalimu bora wa imani, maadili na utu wema. Awe jasiri wa kukemea maovu na kulinda umoja wa Kanisa kama ilivyo kauli mbiu yake ‘Ili wawe na umoja.’

Askofu mkuu Angelo Accattino Balozi wa Vatican Nchini Tanzania.
Askofu mkuu Angelo Accattino Balozi wa Vatican Nchini Tanzania.   (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Askofu mkuu Angelo Accattino, Balozi wa Vatican nchini Tanzania amefurahi kuona historia ya Bagamoyo ya kuwakomboa wanadamu kutoka katika vifungo vya utumwa wa kimwili na kiroho inajirudia tena. Kama mlango wa Imani, Bagamoyo ilikuwa Vicarieti mnamo 11 Mei 1906 lakini ikatoweka mnamo 25 Machi 1953 baada ya kuundwa Jimbo Katoliki Bagamoyo. Amesema ni furaha kuona mamlaka ya zamani yamerudi katika kipindi ambacho Kanisa linaadhimisha Jubilei kuu ya Mwaka 2025 ya Ukristo. Analipongeza Jimbo kuu Dar es Salaam na Jimbo Katoliki Morogoro si tu kwa kushiriki mchakato wa kuunda jimbo hilo jipya bali kwa kukubali kutoa sehemu ya Parokia na Mapadre wao ili kuunda Jimbo jipya la Morogoro. Enzi za wamisionari Bagamoyo palikuwa ni sehemu ya biashara ya utumwa ambapo utu na heshima ya mwanadamu ulivunjwa lakini wamisionari waliwakomboa watumwa na kuwapa uhuru wa kuishi kwa furaha na kuwafundisha imani. Amesema ni kazi sasa ya Jimbo la Bagamoyo ambalo ni sehemu maarufu ya hija kudumisha ari na moyo wa kimisionari wa kutoa uhuru kwa wengine. Amelitaka jimbo la Bagamoyo kukuza Imani Katoliki kwa kufundisha dini, kusali na Askofu mahalia sasa aweke sera na mpango mkakati ya kuliendeleza jimbo hilo. ‘Usiogope kwakuwa Mungu yu Pamoja nawe.’

Makamu wa Rais Dr Philip Mpango amehudhuria
Makamu wa Rais Dr Philip Mpango amehudhuria   (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Baada ya kuzinduliwa kwa Jimbo Katoliki la Bagamoyo, linalifanya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuwa na majimbo Katoliki 36 kiashiria cha kuonesha ukomavu wa imani na matunda ya uinjilishaji wa kina nchini Tanzania yaliyoanzishwa na wamisionari kupitia mlango wa imani Bagamoyo. Kwa sasa Kanisa Katoliki Tanzania lina majimbo 36 yanayoongozwa na Maaskofu 41 na Maaskofu wastaafu wako 11. Baraza la Maaskofu Tanzania ni la tatu kwa ukubwa Barani Afrika. Maadhimisho hayo yametokea wakati Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania likiwa limepatwa na “sintofahamu” baada ya Katibu mkuu wa TEC Padri Charles Kitima kuvamiwa na kujeruhiwa na watu wasiojulikana ambapo TEC ilionya kwa ukali tukio hilo. Makamu wa Rais TEC Askofu Eusebius Nzigilwa alisema kushambuliwa kwa Padri Kitima katika makazi ya Baraza hilo ni zaidi ya kumshambulia mtu mmoja. Tukio hilo si la kawaida kwani linagusa utu wa mtu, heshima ya taasisi na sifa ya Taifa la Tanzania. Huu haukuwa wizi wa mali bali ni jaribio la kupoka uhai, uhuru na haki ya kuishi kwa dhamiri na imani.

Waamini wakishiriki katika uzinduzi wa Jimbo la Bagamoyo
Waamini wakishiriki katika uzinduzi wa Jimbo la Bagamoyo   (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Askofu Stefano Musomba OSA wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo kwa upande wake, amewashukuru walezi, walimu, Shirika lake la Mtakatifu Augustino, OSA kwa malezi na ushirikiano hadi kufikia Daraja Takatifu ya Uaskofu. Amelishukuru Jimbo kuu Katoliki la Dar es Salaam hususani Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi, OFMCap. kwa kumlea katika Urika wa Maaskofu, kwa mang’amuzi ya utume. Amemshukuru Mwadhama Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwa malezi, ushauri na kumpokea kama Baba mara zote katika kipindi chote alipolihudumia jimbo hilo. Amelishukuru Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC kwa ushirikiano na Vatican kwa kumwamini kwamba anaweza kuliongoza Jimbo jipya la Bagamoyo. Amewashukuru waamini wa Bagamoyo kwa kumpokea huku akitaka wadumishe umoja baina yao.

Chama Cha Utoto Mtakatifu Jimbo Katoliki la Bagamoyo
Chama Cha Utoto Mtakatifu Jimbo Katoliki la Bagamoyo   (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Makamu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Philip Mpango ambaye katika hotuba yake amelaani vikali na kukemea tukio hilo la kushambuliwa na kuumizwa kwa Katibu mkuu wa TEC Padri Charles Kitima pamoja na matukio mengine kama hayo ya uvunjifu wa sheria na amani. Amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani imeviagiza vyombo vya dola kuwatafuta, kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria wahusika wa tukio hilo. Amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu wakati wote wa: Maandalizi, kampeni, uchaguzi mkuu pamoja na kutangazwa kwa matokeo. Amesema ni vema kuepuka kauli za kichochezi, uzushi na upotoshaji kupitia mitandao ya kijamii na njia nyingine za mawasiliano kwa misingi ya tofauti ya itikadi za kisiasa, kidini, kabila au rangi. Vilevile Makamu wa Rais amewaasa vijana kutokubali kutumiwa na wanasiasa wenye uchu wa mali na wa madaraka waliotayari kuwatumia kuchochea vurugu wakati wa uchaguzi kwa manufaa yao wenyewe.

Askofu Musomba akisalimiana na watawa
Askofu Musomba akisalimiana na watawa   (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Amewasisitiza watendaji serikalini kutenda haki katika utekelzaji wa majukumu waliyokabidhiwa. Amesema ni muhimu kuliombea taifa la Tanzania kwa Mwenyezi Mungu ili liwe na amani na utulivu hususani mwaka huu 2025 linapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Amesema kuwa, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi wa dini na taasisi zake ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kuhudumia vyema umma wa watanzania. Serikali inathamini mchango mkubwa wa Kanisa Katoliki na madhehebu mengine ya dini katika kuimarisha upatikanaji wa huduma mbali mbali za jamii husani afya na elimu. Ameeleza kuwa, uamuzi wa Hayati Baba Mtakatifu Francisko kuunda Jimbo Jipya Katoliki Bagamoyo si tu umeipa Bagamoyo hadhi lakini pia umesogeza huduma za kichungaji kwa waamini na utaongeza kasi ya uinjilishaji wa kina. Makamu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Philip Mpango amewapongeza wanajimbo la Bagamoyo kwa kupata jimbo na mchungaji mkuu. Bagamoyo imekuwa ndiyo mlango wa kuingia imani ya Kikristo nchini Tanzania na maeneo mengine ya Afrika Mashariki na kati.

Umoja na mshikamano katika ujenzi wa Kanisa
Umoja na mshikamano katika ujenzi wa Kanisa   (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Jimbo Katoliki la Bagamoyo chini ya Askofu Stefano Musomba OSA linaundwa na Dekania tano ambazo ni: TEGETA inayoundwa na Parokia ya Boko, Bahari Beachi, Ununio, Mbweni Teta, Yohane Mwinjili (Kibaoni), Yohane Mbatizaji (Teule) na Dekano wake ni Padre Emmanueli Makusalo, C.PP.S. DEKANIA MIVUMONI inaundwa na Parokia ya: Mivumoni, Wazo, Madale, Mbopo, Nyakasangwe, pamoja na Toma Mtume. Dekano wake ni Padre Joseph Rwena. DEKANIA YA BUNJU inaundwa na Parokia ya: Bunju, Rafaeli, Francis Mpiji, Kinondo, Kerege, Kiharaka pamoja na Parokia teule ya Zinga na Dekano wake ni Padre Edwin Dino. DEKANIA YA BAGAMOYO inaundwa na Parokia ya: Moyo Safi wa Bikira Maria, Epifania, Kiwangwa, Mandela, Lugoba na Makurunge. Dekano ni Padre Eliasi Petro. DEKANIA CHALINZE inaundwa na Parokia ya: Chalinze, Mdaula, NgeleNgele pamoja na Parokia ya Bwani. Dekano wake ni Padre Patrick Kung'aro. ya Askofu Stefano Musomba OSA amewataka Madekano kujikita katika kukuza na kudumisha uwazi na uwajibikaji katika kutekeleza nyajibu zao.

Jimbo la Bagamoyo
08 Mei 2025, 14:47