Sekretarieti kuu ya Sinodi yapongeza kuchaguliwa kwa Papa Leo XIV!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Sekreteriti Kuu ya Sinodi ilituma Barua kwa Papa Mpya Papa Leo XIV ili kumpongeza kuchaguliwa kwake. Katika barua hiyo inaanza kubainisha kuwa: Baba Mtakatifu uliyebarikiwa sana, kwa shukrani nyingi, Sekretarieti Kuu ya Sinodi inatoa shukrani kwa Bwana kwa ajili uchaguzi wako kwa uongozi wa Kanisa. Kwako wewe, ambaye pia unaongoza Sekretarieti hii, tunakuonesha tangu wakati huu furaha yetu ya kutembea pamoja, kuunga mkono huduma yako kwa ushirika kati ya Makanisa yote. Sinodi ni safari ya kikanisa inayoongozwa na Roho Mtakatifu, zawadi ya Bwana Mfufuka anayetusaidia kukua kama Kanisa la kimisionari, likiendelea kuongoka kwa kusikiliza Injili kwa makini.
Barua hiyo inaendelea kusema kuwa “kwa kupendelewa na Baba Mtakatifu Francisko,sinodi inawahusisha Watu wote wa Mungu katika mchakato wa pamoja, ambapo kila mtu anachangia katika kutambua hatua za kuchukua, kadiri ya karama, miito na huduma anazopokea. Baada ya kuanza mwaka 2021 na awamu ya kusikiliza watu wa Mungu, mchakato wa sinodi sasa ulikamilisha awamu ya utambuzi wa Wachungaji na Mkutano Mkuu wa XVI wa Sinodi ya Maaskofu na kwa idhini ya Hati ya Mwisho na Baba Mtakatifu Francisko.” Maelekezo yaliyomo katika Hati hiyo “tayari sasa yanaweza kutekelezwa katika Makanisa ya mahalia pamoja na vikundi vya Makanisa, kwa kuzingatia miktadha tofauti, kile ambacho tayari kimefanyika, na kile kinachosalia kufanywa ili mtindo unaofaa kwa Kanisa la Sinodi ya kimisionari uweze kujifunza na kuendelezwa vyema zaidi daima” (Maelezo Yanayoambatana Nayo).
Wakati huo huo, vikundi vya mafunzo vinafanya kazi kuwasilisha mapendekezo kwako Baba Mtakatifu kwa nia ya kufanya maamuzi yanayohusisha Kanisa zima. Na kwa sasa kwa kuwa safari inaendelea chini ya uongozi wako Baba Mtakatifu, tunatazamia kwa ujasiri maelekezo Utakayoonyesha, ili kusaidia Kanisa kukua kama jumuiya iliyo makini kusikiliza, karibu na kila mtu, yenye uwezo wa mahusiano ya kweli na ya kukaribisha—nyumba na familia ya Mungu iliyo wazi kwa wote: Kanisa la sinodi ya kimisionari. Sekretarieti Kuu ya Sinodi bado inapatikana kikamilifu ili kutoa huduma yake kwa moyo wa ushirikiano na utii. Barua hiyo inahitimishwa kuwa" Kwa upendo wa kimwana na katika maombi." Waliotia saini ni Kardinali Mario Card. Grech Katibu Mkuu wa Wa Sekretarieti ya Sinodi, Monsinyo Luis Marín de San Martín, O.S.A. Katibu wake, na Sr. Nathalie Becquart, X.M.C.J. Katibu Msaidizi.