Ujumbe wa Sikukuu ya Vesak/Hanamatsuri 2025: Mazungumzo ya Ukombozi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Tangu Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipozindua mchakato wa majadiliano ya kidini katika Tamko lao la “Nostra aetate” yaani “Nyakati Zetu”, kumekuwepo na mafanikio makubwa yanayofumbata amana na utajiri wa maisha ya kiroho; uelewa na udugu wa kibinadamu unaopania kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya waamini wa dini mbalimbali duniani. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa Katoliki halikatai yoyote yaliyo kweli na matakatifu katika dini mbali mbali zisizo za kikristo. Lenyewe laheshimu kwa sifa timamu namna zile za kutenda na kuishi, sheria zile na mafundisho yale ambayo, ingawa mara nyingi yanatofautiana na yale ambayo lenyewe laamini na kufundisha, hata hivyo, mara nyingine, yanarudisha nuru ya mshale wa ule Ukweli wenye kumwangazia kila mtu. Kanisa linaendelea kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, njia, ukweli na uzima. Rej. Yn. 14:6. Ndani ya Kristo Yesu kuna utimilifu wa utauwa, na ambamo Mwenyezi Mungu alivipatanisha vitu vyote na nafasi yake.
Adui mkubwa wa mchakato wa majadiliano ya kidini ni woga na wasiwasi usiokuwa na msingi, mambo yanayochangia watu wa dini mbalimbali kushindwa kufahamiana na hatimaye kuishi kwa amani, umoja na udugu wa kibinadamu kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na hivyo tofauti zao za kidini si sababu msingi ya malumbano na kinzani zisizo na tija wala mashiko kwa watu. Katika mchakato wa majadiliano ya kidini, Mababa wa Mataguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanaendelea kuhimiza umuhimu wa waamini wa dini mbalimbali kufahamiana na kushirikiana. Majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa Katoliki ili kujenga na kudumisha amani, upendo na mshikamano kati ya watu na wala si kwa bahati mbaya kwamba, Kanisa katika sera, mikakati na vipaumbele vyake katika mchakato wa uinjilishaji linaendelea kukazia majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali duniani.
Sikukuu ya "Vesak", ni siku ya mwezi uliokamilika na huadhimishwa mwezi wa Mei, kila mwaka. Ni siku takatifu zaidi kwa mamilioni ya Wabuddha ulimwenguni kote. Na ilikuwa ni katika Siku ya Vesak milenia mbili na nusu zilizopita, mwaka wa 623 Kabla ya Kristo (KK), ambapo Gautama Buddha alizaliwa. Ni katika muktadha wa siku hii Buddha pia alipata upako na ni katika maadhimisho ya Sikukuu hii, Gautama Buddha alipofariki dunia, akiwa na umri wa miaka 80 tangu alipozaliwa. Kumbe hii ni fursa ya kuwa karibu na watu wanaoteseka, ili kuwapatia faraja, amani na furaha kwa njia ya huduma inayojikita katika huruma. Ni katika muktadha wa Sikukuu ya Vesak kwa mwaka 2025 inanogeshwa na kauli mbiu: “Wabuddha na Wakristo katika Mazungumzo ya Ukombozi kwa Wakati Wetu,” Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini linasema, Mama Kanisa anafanya kumbukizi ya miaka 60 ya Tamko la “Nostra aetate” yaani “Nyakati Zetu” sanjari na maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Kipindi cha Jubilei ni muda muafaka wa neema, upatanisho na upyaisho wa maisha ya kiroho. Hiki ni kipindi cha kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema: “Katika ubuddha, kulingana na madhehebu yake mbalimbali, hukirika kule kutoweza kwa asili kwa ulimwengu huu geugeu, na kufundishwa njia ambayo watu, wakiifuata kwa moyo wa ibada na imani, wanaweza kujipatia hali ya afua kamili au kuifikia ile hali ya mwangaza mkuu, ama kwa njia ya juhudi zao wenyewe, au kwa msaada unaotoka juu.” Nostra aetate, 2.
Njia ya Kibuddha ya ukombozi inahusisha kuvuka ujinga, tamaa, na mateso kupitia ufahamu, mwenendo wa maadili mema, na nidhamu ya akili. Safari ya kuelekea Nibbana - uhuru wa mwisho kutoka kwa mzunguko wa kuzaliwa, kifo, na kuzaliwa upya, inaonesha nguvu ya mabadiliko ya hekima na huruma. Shauku hii ya ukombozi wa kweli inapata mwamko wake wa kina katika harakati za waamini pamoja na ukweli sanjari na utimilifu wa maisha, na inapatana na mafundisho ya mila za watu. Buddha alifundisha kwamba, "Yeye ambaye hana tamaa na kushikamana, ni mkamilifu katika kufunua maana ya kweli ya Mafundisho, na anajua mpangilio wa Maandiko matakatifu katika mlolongo sahihi, yeye kwa hakika ndiye mbebaji wa mwili wake wa mwisho. Hakika anaitwa mwenye hekima nyingi, mtu mkuu" ( Dhammapada, Sura ya 24, V. 352). Kwa Kristo Yesu, ujuzi wa Kweli ni ukombozi: "Mtaifahamu kweli, na hiyo kweli itawaweka huru" Yn 8:32.
Katika nyakati hizi ambamo kumegubikwa na mipasuko, kinzani na mateso; kuna haja kwa waamini kujikita katika majadiliano yanayomwilishwa katika matendo kwa ajili ya: haki, amani, utu na heshima ya binadamu wote. Kwa hakika dini zina mchango mkubwa kwa kutoa majibu kuhusu vitendawili vigumu vya hali ya wanadamu, ambayo hadi sasa vinafadhaisha sana nyoyo ya watu. Rej. Nostra aetate, 1. Kumbe, kuna umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, kwa kushirikishana amana na utajiri wa maisha ya kiroho, ili kukabiliana na changamoto mamboleo na hivyo kuendelea kujenga udugu wa kibinadamu, umoja na mapendo kati ya watu wa Mataifa. Waamini wa dini mbalimbali waendelee kujikita katika yale mambo yanayowaunganisha, kuthamini tofauti msingi pamoja na kuendelea kutajirishana kutoka na utofauti wao. Huu ni mwaliko wa kukumbatia utamaduni wa majadiliano, ushirikiano na mshikamano. Baraza la Kipapa la Majadiano ya Kidini linahitimisha ujumbe wake kwa maadhimisho ya Sikukuu ya Vesak kwa Mwaka 2025.