Tafuta

Askofu Mkuu Novatus Rugambwa alikutana na Papa Leo XIV wakati wa Mkutano na Mabalozi wa Vatican tarehe 10 Juni 2025. Askofu Mkuu Novatus Rugambwa alikutana na Papa Leo XIV wakati wa Mkutano na Mabalozi wa Vatican tarehe 10 Juni 2025. 

Askofu Mkuu Novatus Rugambwa,ameaga dunia

Ni taarifa iliyotolewa na Askofu Mwijige wa Jimbo la Bukoba,Tanzania.Askofu Mkuu Novatus Rugambwa aliyekuwa Balozi wa zamani,New Zealand na mwakilishi wa Kitume kwenye visiwa vya Bahari ya Pacific aliaga dunia Septemba 16 katika Hospitali jijini Roma.Alizaliwa tarehe 8 Oktoba 1957,katika Jimbo Katoliki la Bukoba.Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi,akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 6 Julai 1986.Akajiunga na utume wa kidiplomasia mjini Vatican tarehe 1 Julai 1991.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Jimbo Katoliki la Bukoba  nchini Tanzania,  Jumatano tarehe 17 Septemba 2025, na Mwashamu Askofu Jovitus Francis Mwijage, wa Jimbo hilo  aliwaelekea Wahashamu Maaskofu, Waheshimiwa Mapadre, Watawa na Waamini wote kuwa:  “Tumsifu Yesu Kristo, ninasikitika kutangaza kifo cha Mpendwa wetu Mhashamu Askofu Mkuu Novatus Rugambwa aliyeitwa na Mungu jana jioni  tarehe 16 Septemba 2025, wakati akipatiwa matibabu huko Roma nchini Italia.” Askofu Mwijage aliongeza: “Pole sana” na kwamba, “tuzidi kuiombea roho yake ipate pumziko la Milele.”  Wakati huo huo, anabainisha kwamba “Mipango ya Mazishi itaendelea kuratibiwa.” Na Kumwombea : “Raha ya Milele umpe Ee Bwana, na Mwanga wa Milele umwangazie. Apumzike kwa Amani," Amina.

Kanisa Katoliki la Tanzania na Ulimwengu ni kote, linaomboleza kwa ajili ya mtumishi wake Askofu Mkuu Novatus Rugambwa aliyezaliwa tarehe 8 Oktoba 1957, Katika Jimbo Katoliki la Bukoba nchini Tanzania. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre mikononi mwa Hayati Askofu Nestorius Timanywa kunako tarehe 6 Julai 1986. Akajiunga na utume wa kidiplomasia mjini Vatican hapo tarehe 1 Julai 1991. Baada ya kufanya kazi mbali mbali katika Balozi za Vatican, kunako tarehe 28 Juni 2007,  Baba Mtakatifu  Benedikto wa XVI akamteuwa kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum. Ilipofika tarehe 6 Februari 2010, Baba Mtakatifu Benedikto XVI, akamteua kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Angola, Sao Tome na Principe na kuwekwa wakfu kuwa Askofu Mkuu na Kardinali Tarcisio Bertone, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Vatican kwa wakati ule hapo tarehe 18 Machi 2010.

Na tarehe 5 Machi 2015 akateuliwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Honduras. Tarehe 29 Machi 2019, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Balozi wa Vatican huko New Zealand na mwakilishi wa Kitume kwenye visiwa vya Bahari ya Pacific. Na kunako  tarehe 30 Machi 2021, Baba Mtakatifu Francisko alimwongezea tena majukumu kwa kumteua kuwa ni Balozi mpya wa Vatican kwenye Jamhuri ya Microsia, iliyoko Magharibi mwa Bahari ya Pacific. akiendelea kuwa ni Balozi wa Vatican kwenye Visiwa vya Marshall, Kiribati, Nauru na Tonga, na Balozi wa Vatican nchini New Zealand, Fiji, na  Palau.


Hata hivyo hivi karibuni, wakati tayari anaumwa  Askofu Mkuu Rugambwa aliweza kushiriki Mkutano kunako tarehe 10 Juni 2025 na Baba Mtakatifu Leo XIV, alipokutana na Mabalozi wote wa Vatican wanaomwakilisha Baba Mtakatifu Ulimwenguni kote. Raha ya Milele Umpe Ee Bwana na Mwanga wa Milele Umwangazie apumzike kwa amani, Amina.

Kifo cha Askofu Mkuu Rugambwa

Mazishi

Kwa taarifa, zaidi kutoka Jimboni Bukoba, Mwili wa marehemu utasafirishwa tarehe 26 Septemba 2025 kwenda Dar Es Salaam , Tanzania,  na baadaye kusafirishwa kwenda Bukoba, mahali ambap atazikwa tarehe 29 Septemba 2025 katika Kanisa Kuu Katoliki la Bukoba Tanzania.

Misa ya kuaga Marehemu mjini Vatican inafanyika leo tarehe 25 Septemba 2025 katika Basilika ya Mtakatifu Petro mjini Vatican.

 

Imesasishwa Alhamisi 25 Septemba 2025 saa 1.29 asubuhi saa za Ulaya.

17 Septemba 2025, 10:28