Jubilei ya Makatekista:Septemba 26-28 ni mahujaji kutoka nchi 115!
Vatican News
Makatekista kutoka sehemu mbalimbali dunia wamekusanyika mjini Roma kuadhimisha Jubilei ya Makatekista kuanzia tarehe 26 hadi 28 Septemba 2025. Zaidi ya mahujaji elfu ishirini kutoka nchi 115 wamewasili jijini Roma kutoka: Italia, Hispania, Ureno, Ufaransa, Poland, Ukraine, Marekani, Argentina, Brazili, Paraguai, Mexico, Peru, Colombia, Ufilipino, India, na Australia na kwingineko. Matukio ya Jubilei yamejitolea kwa wale ambao kila siku wanashiriki katika katekesi, wakifundisha imani kwa watu wa rika na matabaka yote ya maisha. Hawa wanawakilisha ofisi za kijimbo na kitaifa za katekesi na Mabaraza ya Maaskofu ya nchi zao.
Jubilei ilianza siku ya Ijumaa asubuhi tarehe 26 Septemba 2025 na makatekista wakianza hija zao kupitia Mlango Mtakatifu wa Basilika ya Mtakatifu Petro. Baadaye katika siku hiyo Mkesha wa Sala ulifanyika ndani ya Kanisa Kuu, ukiongozwa na Askofu Mkuu Rino Fisichella, Msimamizi wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji. Katika sehemu ya pili ya Liturujia ya Neno, inayozingatia kifungu cha wanafunzi kwenye barabara ya kwenda Emau(Lk 24:13-33a), makatekista watatu kutoka Italia, Msumbiji, na Mexico walishiriki historia zao za kibinafsi za huduma katika jumuiya zao mahalia.
Jumamosi tarehe 27 Septemba Makatekista walishiriki Katekesi ya Jubilei katika Uwanja wa Mtakatifu Petro pamoja na Papa Leo XIV, ambaye aliwasalimia. Mchana saa 10:00 makatekista walikuwa na mkusanyika katika makanisa mbalimbali katikati mwa Roma kwa ajili ya katekesi katika vikundi vya lugha pamoja na maaskofu wao. Lugha zilizokuwa zimepangwa ni: Kiitaliano, Kiingereza, Kireno, Kihispania, Kifaransa na Kipoland.
Jubilei hiyo itafikia kilele Dominika tarehe 28 Septemba kwa Misa katika Uwanja wa Mtakatifu Petro itakayoongozwa na Papa Leo saa 4:00 asubuhi, masaa ya Ulaya ambapo atawatuma makatekista wapya 39. Wagombea wa huduma ya walei ya Katekista, ambao kila mmoja atapokea msalaba kutoka kwa Papa kama ishara ya wito wao maalum, wanatoka Italia, Hispania, Uingereza, Ureno, Brazil, Mexico, India, Korea ya Kusini, Timor ya Mashariki, Falme za Kiarabu, Ufilipino, Marekani, Msumbiji, Brazil, Peru na Jamhuri ya Dominika.
Mkesha katika Basilika ya Mtakatifu Petro
“Katekesi ni safari, njia, mpango unaotekelezwa siku baada ya siku,” alisisitiza hayo Askofu Mkuu Rino Fisichella, Mwenyekiti wa Baraza la Uinjilishaji, alipokuwa akiongoza Mkesha wa Sala ya Jubilei ya Makatekista katika Kanisa Kuu la Vatican Ijumaa, tarehe 26 Septemba. Askofu Mkuu alisema kuwa Kristo Mfufuka ndiye Kitovu cha Historia na Moyo wa Imani na kwa njia hiyo alitoa tadkaritatu maalum wakati wa mahubiri yake mbele ya waamini elfu ishirini kutoka nchi 115. Kwanza, alisema, “katekesi lazima isimikwe juu ya Kristo Mfufuka, kitovu cha historia na moyo wa imani, kwa kuwa fumbo la wokovu wake ni fumbo la historia yetu. Kwa hiyo, msisitizo ulikuwa kwamba katekesi lazima ifanyike pamoja na Kristo, kwa sababu Yeye anatusindikiza, Yeye hukutana nasi. Mara nyingi-alibainisha-tunazungumza juu ya Kristo, lakini hatuishi kwa ajili yake Yeye, na katekesi, hata ingawa ni nzuri, inabaki tupu ikiwa Bwana hatembei nasi."
Hatimaye, mshereheshaji alihimiza kuchanganya mafundisho ya katekesi na utajiri wa kisakramenti, kwa kutazama mfano wa wanafunzi wa Emau, ambao walimtambua Yesu katika kuumega mkate na kisha waliona uharaka wa kurudi Yerusalemu na kutangaza Ufufuko wake. Hii inaonesha kwamba katekesi ni tukio la jumuiya, si tukio la mtu binafsi. Kila katekista kamwe hayuko peke yake, bali huleta jumuiya ya Kikristo pamoja nao. Kwa hiyo, kitia-moyo cha kumalizia cha kuwa mashahidi wa tumaini kubwa zaidi linalotuonesha wakati ujao utakaojengwa."