Cardinal Koch ampongeza Askofu Mkuu Mteule Sarah Mullally wa Canterbury
Vatican News
Mfalme Charles III wa Uingereza aliidhinisha uteuzi wa Mheshimiwa Bi Sarah Mullally, kuwa Askofu wa London, kama Askofu Mkuu wa 106 wa Kianglikani wa Canterbury. Askofu Mkuu Mteule anakuwa mwanamke wa kwanza kushikilia ofisi hiyo, huku kuanza kwake utume wake kufanyika mnamo Machi 2026 katika Kanisa Kuu la Canterbury nchini Uingereza.
Katika barua aliyomwandikia Askofu Mullally, Kardinali Kurt Koch, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Kikristo alitoa pongezi zake na kueleza uungaji mkono wa Kanisa Katoliki kwa huduma yake mpya. Kardinali Koch aliandika: “Baada ya kufahamu kuteuliwa kwako… ninakuandikia kukupongeza kwa kuteuliwa kwako na kukutakia heri njema za Kanisa Katoliki unapojitayarisha kufanya huduma hii muhimu katika Kanisa lako. Ninaomba kwamba Bwana akubariki kwa karama unazohitaji kwa ajili ya huduma ngumu sana ambayo umeitiwa sasa, kukuwezesha kuwa chombo cha ushirika na umoja kwa waamini ambao utatumikia miongoni mwao."
Kardinali Koch aidha aliakisi mazungumzo ya kitaalimungu ya muda mrefu kati ya Usharika wa Kianglikani na Kanisa Katoliki, akibainisha kwamba yamekuza maelewano na upendo kwa karibu miaka sitini. Alikumbuka joto la mahusiano kati ya jumuiya hizo mbili, hasa baada ya kifo cha Papa Francisko mapema mwaka huu, na akaelezea matumaini kwamba ukaribu huu utaendelea: "Ni matumaini yangu makubwa kwamba ukaribu huo unaweza kuendelea katika miaka ijayo tunapoendelea kutembea pamoja njiani. Nikiwa na hakikisho la maombi yangu kwa ajili yako na familia yako," alisema.
Kardinali Kurt Koch,Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Kikristo.
Askofu Mullally
Askofu Mullally anamrithi Askofu Mkuu Justin Welby, ambaye alijiuzulu karibu mwaka mmoja uliopita. Amehudumu kama Askofu wa London tangu 2018, na kuwa mwanamke wa kwanza katika jukumu hilo, na hapo awali aliwahi kuwa Askofu katika Usharika wa Exeter. Kabla ya kuwekwa wakfu mwaka wa 2001, alikuwa Afisa Mkuu wa Muuguzi wa Uingereza, ambaye ndiye kijana mdogo zaidi aliyepata kuteuliwa kufanya kazi hiyo akiwa na umri wa miaka 37. Ameeleza kuwa uuguzi ni “fursa ya kuonesha upendo wa Mungu.”
Tume ya Uteuzi ya Canterbury ilimchagua Askofu Mullally kufuatia mchakato wa mashauriano ya umma na utambuzi wa maombi ulioanza Februari 2025. Tume hiyo ilijumuisha wawakilishi kutoka Kanisa la Kianglikani, Usharika wa Kianglikani wa kimataifa, na Usharika wa Canterbury. Akitafakari kuhusu kuteuliwa kwake, Askofu Mkuu Mullally alisema anatumaini kulitia moyo Kanisa “kuendelea kukua katika imani katika Injili, kuzungumzia upendo tunaoupata kwa Yesu Kristo na kwa ajili yake kuunda matendo yetu,” na tunatazamia kushiriki “safari hii ya imani na mamilioni ya watu wanaomtumikia Mungu na jumuiya zao katika Parokia zote nchini na katika Usharika wa Kianglikani wa kimataifa.”
Asante sana kusoma makala yetu. Kama unataka kujisasisha, unaweza kujiandikisha kwa makala zetu za kila siku hapa: Just click here.