Kard.Koovakad:Dini zina nafasi ya pekee katika kukuza amani
Vatican News.
Kardinali George Jacob Koovakad, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Maendeleo Fungamani ya Binadamu, Ijumaa tarehe 3 Oktoba 2025 alihutubia mkutano wa viongozi wa kidini, wawakilishi wa raia, wasomi, na wanaharakati wa amani katika sherehe ya kidini zilizoongozwa na mada: "Mahujaji wa Matumaini - Dini Zinazosafiri kwa Amani," iliyofanyika katika Ukumbi wa Mtakatifu Andrew huko Mumbai nchini India. Hafla hiyo iliandaliwa na Jimbo Kuu la Bombay kama sehemu ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei 2025. Akifungua hotuba yake, Mkuu wa Baraza la Mazungumzo ya Dini Mbalimbali aliangazia umuhimu wa siku hiyo, sanjari na sikukuu ya Mtakatifu Fransisko wa Assisi, ambaye alimtaja kuwa “mtakatifu wa upendo wa kindugu, usahili na furaha,” na mwanzilishi wa mazungumzo ya kidini ambaye “alipanda mbegu za amani.”
Mazungumzo ya kidini
Kardinali pia alitafakari kuhusu kumbu kumbu ya miaka 60 tangu Waraka wa Nostra Aetate, Enzi zetu , ambao ni waraka wa kihistoria wa Papa Mtakatifu Paulo VI wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican uchapishwe ambao ulifungua njia ya mazungumzo ya kisasa kati ya dini. "Tunafurahi kwa jukumu kubwa la hati hii katika kukuza mazungumzo kati ya watu wa dini tofauti ulimwenguni kote," alisema, akibainisha kwamba kanuni za Nostra Aetate zinaendelea kuhimiza "udugu, urafiki, umoja na mshikamano kwa manufaa ya ubinadamu." Akimnukuu Papa Francisko juu ya umuhimu wa kudumu wa Waraka wa Nostra Aetate, Kardinali alithibitisha: "Roho Mtakatifu anafanya kazi, kama kitovu cha amani na upendo," akiakisi dhamira ya Kanisa katika kutambua uzuri na ukweli katika dini zote wakati wa kuendeleza mazungumzo. Pia alitaja maneno ya Papa Benedikto XVI kuhusu mazungumzo ya kidini kama "safari ya pamoja, hata yenye picha tofauti za Mungu, kuelekea chanzo cha Nuru." Kardinali Koovakad alielekeza fikira kwenye changamoto za kisasa zinazowakabili wanadamu, kutia ndani kutovumilia, ubaguzi, na jeuri, na kuwahimiza washiriki wawe “mahujaji wa matumaini.”
Dini si chanzo cha migogoro bali ni nafasi ya kuimarisha upatanisho
Kardinali Koovakad lifafanua, “Kama waamini, tumeitwa kuwa wanaume na wanawake wa matumaini wenye kuleta matumaini kwa wale walioyapoteza, hasa maskini, wanaoteseka, waliotengwa, wanaobaguliwa, wanaoteswa na walio hatarini zaidi katika jamii. Alisisitiza kuwa, dini kupitia rasilimali zao za kiroho na kimaadili zina nafasi ya pekee katika kuimarisha upatanisho na uponyaji. Akinukuu maneno ya Papa Leo XIII, alithibitisha kwamba “dini, kimsingi, si chanzo cha migogoro bali ni kisima cha uponyaji na upatanisho.” Aliongeza kwamba mazungumzo kati ya dini mbalimbali huruhusu waumini “kutoa ushuhuda wa ukweli kwamba imani huunganisha zaidi kuliko inavyogawanya” na huimarisha “tumaini letu la ulimwengu bora na wenye haki zaidi.”
Kudumu katika kutafuta amani
Kwa kuhitimisha hotuba yake, Kardinali Koovakad aliwahimiza washiriki wote kudumu katika juhudi zao za kutafuta amani licha ya matatizo na mashaka. Aliwakumbusha wasikilizaji kwamba “mazungumzo baina ya dini ni sharti la lazima kwa amani duniani” na kuwataka wote waendelee kuwa “mahujaji wa matumaini na wajenzi wa amani” wanaopanda mbegu za wema popote waendako.
Asante sana kusoma makala yetu. Kama unataka kujisasisha, unaweza kujiandikisha kwa makala zetu za kila siku hapa: Just click here