Tafuta

Mtakatifu Vincenza Maria Poloni, Mwanzilishi wa Shirika la Masista wa Huruma wa Verona (Misericordia) : 1802-1855 Mtakatifu Vincenza Maria Poloni, Mwanzilishi wa Shirika la Masista wa Huruma wa Verona (Misericordia) : 1802-1855 

Mtakatifu Vincenza Maria Poloni: 1802-1855: Shujaa wa Upendo!

Sr. Vincenza Maria Poloni akafariki dunia tarehe 11 Novemba 1855: urithi wa maisha yake ya kiroho: Upendo na Ukimya. Tarehe 28 Aprili 2006 akatambuliwa na Mama Kanisa kuwa ni Mtumishi wa Mungu. Baba Mtakatifu Benedikto XVI akamtangaza kuwa ni Mwenyeheri tarehe 21 Septemba 2008. Na Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe 19 Oktoba 2025 akamtangaza kuwa ni Mtakatifu. Kanisa litakuwa linafanya kumbukumbu yake, kila mwaka ifikapo tarehe 11 Mwezi Novemba.

Na Christine Masivo Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema: Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu dhaifu na mdhambi. Mwenyezi Mungu anajisikia kuwajibika, kwa maana ya kwamba, anatamani kuwaona watu wake wakiwa na afya njema, furaha na amani tele nyoyoni mwao. Hii ni njia ambayo upendo wa huruma ya Wakristo unaopaswa pia kujimwilisha. Huruma ndiyo msingi thabiti wa uhai wa Kanisa. Kazi zake zote za kichungaji zinapaswa kufungamanishwa katika upole linalouonesha kwa waamini; hakuna chochote katika mahubiri na ushuhuda wake kwa ulimwengu kinachoweza kukosa huruma. Umahiri wa Kanisa unaonekana kwa namna linavyoonesha huruma na upendo. Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kujisikia ndugu na watoto wapendwa wa Baba wa milele kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu, shilingi na kondoo aliyepotea. Huruma ya Mungu inawawezesha watu kutambua na kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao hasa wale wanaohitaji kuonjeshwa faraja na upendo. Kimsingi, huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa; ushuhuda makini wa Ufufuko wa Kristo Yesu. Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu awasaidie waamini: kuamini na kuyaishi yote haya kama mashuhuda wa Injili ya huruma, furaha na mapendo.

Mtakatifu Vincenza Maria Poloni 1802-1855
Mtakatifu Vincenza Maria Poloni 1802-1855

Sr. Vincenza Maria Poloni, Mwanzilishi wa Shirika la Masista wa Huruma wa Verona (Misericordia) alizaliwa tarehe 26 Januari 1802, huko Verona, Kaskazini mwa Italia, aliyeanzisha Shirika hili tarehe 10 Septemba 1848 akishirikiana na Mwenyeheri Carlo Steeb, Padre na mshauri wake wa maisha ya kiroho. Katika maisha na utume wake, alitambulikana na wengi kuwa ni “Shujaa na Malaika wa Upendo” kutokana na sadaka na majitoleo yake kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa na maskini. Fumbo la Ekaristi Takatifu lilikuwa ni chanzo na hatima ya maisha na utume wake, kwani hapa alichota nguvu ya utume wake na kwamba, daima alipenda kuhakikisha kwamba, Mwenyezi Mungu anapewa kipaumbele cha kwanza kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wagonjwa, kielelezo cha ukuu na utukufu wa Mungu. Daima alikuwa anasema, “Maskini ni mabwana wetu: tuwapende na kuwatumikia kama vile tungemtumikia Yesu Kristo mwenyewe mubashara.” Sr. Vincenza Maria Poloni akafariki dunia tarehe 11 Novemba 1855 na kuacha kama urithi wa maisha yake ya kiroho mambo makuu mawili: Upendo na Ukimya. Tarehe 28 Aprili 2006 akatambuliwa na Mama Kanisa kuwa ni Mtumishi wa Mungu. Baba Mtakatifu Benedikto XVI akamtangaza kuwa ni Mwenyeheri tarehe 21 Septemba 2008. Na Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe 19 Oktoba 2025 akamtangaza kuwa ni Mtakatifu. Kanisa litakuwa linafanya kumbukumbu yake, kila mwaka ifikapo tarehe 11 Mwezi Novemba.

Mtakatifu Vincenza Maria Polini Shujaa wa Upendo
Mtakatifu Vincenza Maria Polini Shujaa wa Upendo

Baada ya kifo chake, Shirika la Masista wa Huruma wa Verona (Misericordia) likaenea sehemu mbalimbali za dunia na Barani Afrika wanatekeleza amana na utume wao huko nchini Burundi, Angola na Tanzania hasa Jimbo kuu la Dodoma, Jimbo kuu la Dar Es Salaam na Singida. Kwa hakika Mama Vincenza Maria Poloni, amekuwa ni shuhuda wa maisha ya kitawa na kielelezo cha uongozi bora katika maisha na utume wake, ukimya, kama kielelezo cha nguvu ya ndani yenye nguvu ya kuleta mabadiliko. Ushuhuda wa utakatifu wake unakita mizizi yake katika huduma kwa wagonjwa na maskini; maisha ya sala; Ibada kwa Ekaristi Takatifu na tafakari ya kina ya Neno la Mungu. Kwa hakika Mtakatifu Vincenza Maria Poloni, Mwanzilishi wa Shirika la Masista wa Huruma wa Verona ni zawadi safi kwa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, aliyethubutu kumwilisha katika maisha na utume wake tunu msingi za Kiinjili, akawa ni shuhuda amini wa ufunuo wa Uso wa huruma ya Mungu kwa binadamu, unaoweza kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya walimwengu, kwa kupenda kwa akili, moyo na nguvu zote na kuhudumia kwa kutumia akili ya Kiinjili.

Misericordia

 

22 Oktoba 2025, 15:05