Kard.Parolin:Mchango wa kila mtu unahitajika kwa amani nchini Ukraine
Vatican News
"Mchango wa kila mtu unahitajika kweli ili kuchukua hatua kuelekea amani" nchini Ukraine. Kuanzia Marekani, hadi Ulaya iliyoitwa kuchukua "jukumu kubwa la kuongoza," hadi China na Mashariki, ambapo Rais wa Marekani Donald Trump mwenyewe yupo kwa sasa. Alisema hayo Kardinali Pietro Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican ambaye alishiriki katika tukio katika Hospitali ya Watoto ya Bambino Gesù, akiashiria kumbukumbu ya miaka arobaini ya kutambuliwa kwake kama Taasisi ya Kisayansi ya Kulazwa Hospitalini na Matibabu.
Ahadi ya Kibinadamu
Akijibu maswali ya waandishi wa habari kando ya tukio hilo, kadinali aliita kituo hicho "mfano wa ubora" katika huduma ya afya ya Kikatoliki na Italia. "Huu ni wakati muhimu," alisema, "kusisitiza uwepo na jukumu la Bambino Gesù katika huduma ya afya, ya Kikatoliki na ya kitaifa." Na alikumbuka kazi ya kibinadamu ya hospitali hiyo, ambayo imewakaribisha watoto sio tu kutoka Palestina bali pia kutoka nchi zingine zinazopitia migogoro. "Bambino Gesù, inafanya kazi kubwa ya kibinadamu," Kardinali alisema. "Tumejitolea kwa hili, tukiamini kwamba juhudi za kibinadamu, katika kuwatunza wahanga wa vita na katika kubadilishana wafungwa, zinaweza kuwa njia ya amani." Kardinali Parolin aliongeza kwamba Vatican inahisi "imejitolea sana" katika uwanja huu, "ambao ni eneo la kiutamaduni ambalo diplomasia ya Vatican imekuwa ikifanya kazi tangu Vita vya Kwanza vya Dunia."
Juhudi za pamoja za kukomesha migogoro
Kuhusu vita nchini Ukraine, Katibu Mkuu wa Vatican alihimiza tahadhari lakini pia matumaini: "Si rahisi kujibu" ni hatua gani zinahitajika kwa ajili ya mapatano: "Kama ningelijua, tungekuwa tayari tumezitekeleza. Ninaamini baadhi ya mazungumzo yanaendelea, labda si hadharani." Akirudia kueleza matumaini yake kwamba mazungumzo haya yatazaa matunda, Kardinali kisha akasisitiza hitaji la ushiriki mpana kutoka katika jumuiya ya kimataifa: "Ushiriki wa Marekani hakika unahitajika, na tunatumaini kwamba Ulaya itachukua jukumu muhimu zaidi. China pia ina la kusema; kiukweli, Rais Trump kwa sasa yuko China na Mashariki ya Mbali kushughulikia suala hili. Mchango wa kila mtu unahitajika kweli ili kuchukua hatua kuelekea amani."
Mkutano na Orbán
Hatimaye, alipoulizwa kuhusu mkutano wake Jumatatu tarehe 27 Oktoba 2025, kwa Waziri Mkuu wa Hungari, Bwana Viktor Orbán, Kardinali Parolin aliuita mkutano huo "mkutano mzuri," akielezea kwamba "kila mtu aliweza kutoa maoni yake." Na alipoulizwa kama nafasi hizo zilikuwa "mbali," alijibu: "Tunajaribu kuzileta karibu zaidi."