Umuhimu wa Maji Safi na Salama Kwa Ustawi, Maendeleo, Mafao na Haki Msingi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maji ni muhimu sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Maendeleo fungamani ya binadamu kwa siku za mbeleni yatategemea kwa kiasi kikubwa jinsi ambavyo Jumuiya ya Kimataifa itaweza kuyatunza na kuyatumia maji kwa ajili ya: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Afya bora, maji safi na salama ni mahitaji msingi ya binadamu, lakini pia yana umuhimu wake kwa viumbe wote wanaoishi duniani. Kumbe, kuna umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na maboresho makubwa yatakayowawezesha walimwengu kufaidika na haki hii msingi katika maisha yao. Uhaba wa maji safi na salama unaweza kuwa ni chanzo cha migogoro, kinzani na vita kwa siku za usoni, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa haitasimama kidete kulinda, kutunza na kuendeleza vyanzo vya maji pamoja na kutambua kwamba, maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Kumbe, huduma bora za maji safi na salama ni kichocheo kikuu cha maisha na afya bora zaidi. Dhana ya maji kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu ni agenda iliyoibuliwa hivi karibuni, lakini inaendelea kushika kasi kubwa sana katika Jumuiya ya Kimataifa kutokana na unyeti wake unaofungamanishwa na maisha ya binadamu. Ndiyo maana kuna haja ya kuwa na miundo mbinu ya kisheria, kiufundi, kijamii na kisiasa ili kuanzisha mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa utunzaji bora wa vyanzo vya maji. Kwa njia hii, amani duniani inaweza kuimarishwa kwa kuzuia vita, kinzani na migogoro inayoweza kufumbatwa katika mafao ya kisiasa na kiuchumi kwa kubeza: haki msingi, utu, heshima na maisha ya binadamu. Huduma ya afya bora, maji safi na salama ni wajibu wa Serikali husika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwani huu ni wajibu wa watu wote, ili kusaidia mchakato wa kijamii na maendeleo fungamani ya binadamu.
Kumbe, maji safi na salama hayawezi kugeuzwa kuwa sawa na bidhaa nyingine yoyote kwa sababu ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, uratibu wa maji unaunganishwa na wajibu wa kijamii kwa kuwa na mwelekeo sahihi wa kiikolojia sanjari na ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu miongoni mwa nchi mbalimbali duniani. Kwa njia hii, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kufanikiwa kuwa na matumizi bora zaidi ya maji safi na salama pamoja na kudumisha utunzaji bora zaidi wa vyanzo vya maji. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, changamoto mbalimbali zinazomwandamana mwanadamu katika ulimwengu mamboleo, zinahitaji umoja, ushirikiano na mshikamano, kwa kuendelea kutafuta njia bora na rafiki zitakazomsaidia mwanadamu kukabiliana na changamoto hizi katika uso wa dunia. Ni katika muktadha wa umuhimu wa maji katika ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu, kuanzia tarehe Mosi, hadi tarehe 3 Oktoba 2025 kumefanyika Mkutano wa Maji Ukanda wa Amazonia huko Iquitos nchini Peru, kwa kunogeshwa na Nyaraka za Kitume za Baba Mtakatifu Francisko: Laudato si, yaani: “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote,” “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote;” pamoja na Wosia wa Kitume mara baada ya Sinodi: “Querida Amazonia” yaani “Amazonia Mpendwa.”
Wajumbe wa mkutano huu, waliiangalia changamoto ya maji safi na salama kwa jicho la imani na kwamba, maji ni zawadi kutoka kwa Mungu na chemchemi ya uhai. Maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu na ni sehemu muhimu sana ya kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Lakini jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, kuna mamilioni ya watu sehemu mbalimbali za dunia hawana maji safi na salama. Hii ni kutokana na uchafuzi mkubwa wa maji unaofanywa kutokana na: shughuli za uchimbaji wa madini na nishati, ukataji mkubwa miti na misitu, biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote. Changamoto kubwa kwa sasa ni baadhi ya nchi kutaka kugeuza rasilimali maji kuwa ni biashara na watetezi wa maji kama haki msingi za binadamu, wanaendelea kupotea katika mazingira ya kutatanisha na kwamba, kuna migogoro na kinzani ya ugawaji wa rasilimali maji. Waathirika wakuu ni wanawake na watoto na hivyo kukwamisha kizazi kipya kisiwe na uhakika wa maji safi na salama, utu na heshima yao kwa siku za usoni.
Wajumbe katika angalizo lao wanaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwa na sheria, sera na mbinu mkakati wa utunzaji bora wa maji, ili watu waweze kuwa na uhakika wa maji safi na salama; Jumuiya ya Kimataifa ijenge mtandao wa ushirikiano na mshikamano wa Kimataifa ili kuipatia ufumbuzi wa kudumu hii changamoto ya maji safi na salama. Kuna haja ya kuanzisha elimu ya ikolojia makini, itakayosaidia kuwajengea watoto na vijana dhamiri nyofu ya ikolojia inayosimikwa katika imani na utambulisho wa kitamaduni. Watu mahalia wajifunze kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Mwelekeo huu pia unapaswa kukita mizizi yake katika wongofu wa shughuli za kichungaji, ili kuweza kuwa na uhakika wa mazingira bora zaidi ya kuishi; watu wakiwa na maji safi na salama, misitu itakayoziwezesha jumuiya kujenga na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Watu wasimame kidete kulinda na kutunza maji kama chemchemi ya uhai na maisha kwa ajili ya kizazi kijacho, kwani bila maji safi na salama, uhai uko hatarini na kwamba, bila maisha hakuna matumaini.