Wamisionari wa Ekaristi Takatifu na Uinjilishaji Mpya Nchini Tanzania
Na Sr. Gisela Upendo Msuya, - Vatican.
Ukarimu, huruma na mshikamano wa upendo ni nguzo kuu zinazotegemeza shughuli za kimisionari ndani ya Kanisa. Huu ndio ujumbe wa mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV, Dominika 5 Oktoba 2025 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Wamisionari na Wakimbizi. Kuna umuhimu wa kutangaza na kushuhudia furaha na faraja ya Injili, kwa watu wanaoteseka, na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Huu ni wakati wa kufungua ukurasa mpya wa utume wa Kimisionari ndani ya Kanisa kwa kutoa huduma kwa maskini wanaowazunguka watu wa Mungu, ili kuwakirimia matumaini na kutambua kwamba, furaha ya Injili ni kwa ajili ya watu wote. Rej. Evangelii gaudium, 23. Lengo ni kujenga utamaduni mpya wa udugu wa kibinadamu, kwa kuondokana na maamuzi mbele kwa kujikita katika wongofu wa kichungaji na kimisionari, kwa ushirikiano wa kimisionari pamoja na kukuza wito wa kimisionari hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Hii ni changamoto kwa waamini kuwa ni wadau katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika kweli na uzima; ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Hii ndiyo changamoto iliyoko mbele ya Shirika la Masista Wamisionari wa Ekaristi Takatifu na Uinjilishaji Mpya lililoanzishwa kunako tarehe 2 Februari 2016. Mtakatifu Paulo Mtume ndiye Msimamizi na Mwombezi wa Shirika la Masista Wamisionari wa Ekaristi Takatifu na uinjilishaji Mpya. Masista wapya walikuwa ni: Sr. Brighntney Komu, Jimbo kuu la Arusha; Sr. Happyness Chuwa Jimbo Kuu la Arusha; Sr. Jonesia Ngonzi Jimbo Katoliki la Bukoba; Sr. Paskalina Sumaye, Jimbo Katoliki la Mbulu.
UJUMBE WA ASKOFU MKUU ISAAC AMANI MASSAWE: Binti zangu, ninyi mmeamua kumfuasa Yesu Kristo katika nyakati hizi ambapo mioyo ya watu wengi imejawa baridi na mkato wa tamaa umeshamiri katika jamii kama ilivyokuwa kwa wana wa Israeli kule Misri. Ila, Mungu hakutuumba ili tuishi kwenye mkato wa tamaa, bali alitumba ili tuwe na uzima, na tuwe nao tele! Katika somo la kwanza, Kutoka 3: 5-15, Mungu anajifunua kwa Musa, lakini baadaye Mungu anapo mtuma Musa Kwenda kuwakomboa wana wa Israeli kutoka utumwani Misri, Musa anamuuliza Mungu: mimi ni nani hata niende kwa Farao? Mungu anamjibu Musa kwamba, asiogope Kwenda kufanya kazi anayompatia kwani atakuwa pamoja naye ikiwa Musa atakubali kuongozwa na Mungu. Hivyo basi, hata Wamisionari wa Ekaristi Takatifu na Uinjilishaji Mpya wamejiandaa kwa kipindi chote cha malezi kwa ajili ya kwenda kufanya kazi ya kuwakomboa watu wa Mungu katika utumwa wa nyakati hizi: ulevi wa kupindukia, matumizi haramu ya dawa za kulevya, uvivu wa kufanya kazi na kutaka vitu vya haraka haraka ambavyo hawajavifanyia kazi, kukwepa majukumu na kutokutimiza wajibu katika familia, Kanisa na jamii kwa ujumla. Mkawe chachu na mwanga na matumaini mapya kwa hao watumwa! Msikate tamaa, mtumainineni Mungu na muwe radhi kwenda popote atakapowatuma. Masista wapya wanahimizwa kutokuogopa kwani Yesu Kristo, yule aliyejifunua kwa Saulo ndiye huyo huyo aliye pamoja nasi katika Ekaristi Takatifu. Hivyo basi, waendelee kumchagua kama Bwana na Mkombozi wa maisha yao na kukaa katika pendo lake na hatimaye, kumtangaza na kumshuhudia katika maisha ya jumuiya na katika utume wao popote watakapotumwa. Wanadhiri wapya, wamelifanya Shirika liwe na watawa 14 tangu kuanzishwa kwake hapo tarehe 02/02/2016. Vijana waliopo kwenye malezi ni 33 kwa sasa. Wanovisi 7, wapostulanti 12, wakandidati 14. Jumla tuko watawa 45.
UTUME WA SHIRIKA: Tangu kuanzishwa kwake, shirika limekuwa likijishighulisha na kazi mbalimbali za kitume ili kukidhi vigezo vya karama ya shirika ambayo ni Uinjulishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Kwa namna ya pekee wanashirika wanajishughulisha na utume wa kufundisha dini katika shule mbalimbali za msingi na sekondari katika maeneo ya Moshono, ndani ya jimbo kuu Katoliki la Arusha pamoja na utoto mtakatifu katika Parokia ya Mtakatifu Yakobo Mtume. Hali kadhalika, shirika linaguswa na shughuli za kijamii katika mahitaji yake. Kwa namna ya pekee, shirika limwezesha upatikanaji wa maji safi na salama katika Mtaa wa Sorenyi, kata ya baraa Moshono. Maji hayo yananufaisha kaya nyingi za mtaa huo pamoja na shule mbalimbali za msingi na sekondari.
Pia Shirika limefanikiwa kujenga Chuo cha ufundi stadi – VETA kinachojulikana kwa jina “Simona Andrini Vocational Training Centre.” Chuo hicho kinatoa mafunzo kwa kozi zifuatazo: Ushonaji, upishi, ufundi bomba, umeme wa majumbani na kompyuta. Lengo la chuo hicho ni kuwawezesha vijana ambao hawakuweza kuendelea na masomo ya elimu juu ili waweze kujipatia ujuzi utakao wawezesha kujikomboa kutoka hali ya umaskini wa kupindukia na kujipatia kipato kidogo kwa ajili ya kujikimu. Hizi zote ni juhudi za kumkomboa mwanadamu katika uduni wa maisha ili naye aweze kuwa na uhai kamili na kutoa mchango wake katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika jamii inayo mzunguka. Ni mategemeo yetu kuendelea kukua na kupanuka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili iletayo uhai ili kuwapeleka watu wengi kwa Yesu Kristo kupitia utume wetu wa Uinjilishaji Mpya unaopata chimbuko lake katika kuabudu na kuiishi Ekaristi Takatifu! Tunamwomba Bwana wa mavuno aendelee kuongeza wafanyakazi katika shamba lake, ambao wamejawa na ari ya kumtumikia kwa unyofu na unyenyekevu. “Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki. Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu. Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika; wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama.” Lk 5:4-5.