Tafuta

2025.11.26 Udienza Generale

Katika Dilexi Te:Huduma ya Maskini katika nyumba za kitawa

Maisha ya kimonaki,ambayo yalianzia katika ukimya wa jangwa,yalikuwa tangu mwanzo ushuhuda wa mshikamano.Watawa na wa kiume na kike waliacha kila kitu, utajiri,ufahari,familia,sio tu kwa sababu walidharau fahari za kidunia yaani; “contemptus mundi”bali pia walitaka kukutana na Kristo maskini katika kifungo hiki kikubwa cha kujibandua.

Padre Angelo Shikombe - Vatican.

Mpendwa msomaji/msikilizaji wa Radio Vatican, tunakuletea mwendelezo wa makala ya wosia wa “Dilexi Te” yaani “Nimekupenda” wa Papa Leo XIV, uliotiwa saini mnamo tarehe 4 Oktoba 2025, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Fransisko wa Assis. Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa waraka huu unaoitwa “DILEXI TE” yaani “nimekupenda” akinukuu kutoka kitabu cha ufunuo 3:9 sehemu inayosema: “…tazama, nitawafanya waje na kusujudu mbele ya miguu yako, nao watatambua ya kuwa nakupenda”. Leo tuendelee sura ya tatu inayoelezea Kanisa lililo kwa ajili ya maskini.  Ndugu msomaji/msikilizaji, tuanze kwa kuitazama Maisha ya kimonaki, ambayo yalianzia katika ukimya wa jangwa, yalikuwa tangu mwanzo ushahidi wa mshikamano. Watawa na wa kiume na kike waliacha kila kitu, utajiri, ufahari, familia, sio tu kwa sababu walidharau fahari za kidunia yaani; “contemptus mundi” bali pia walitaka kukutana na Kristo maskini katika kifungo hiki kikubwa cha kujibandua.

Mtakatifu Basil Mkuu katika Utawala wake, hakuona ukinzani katika maisha ya watawa ya sala na kutafakari na kazi zao kwa maskini. Kwake yeye, ukarimu na huduma kwa wahitaji vilifungamana na sehemu ya maisha ya kiroho ya kimonaki na kitawa, hata baada ya kuacha kila kitu ili kukumbatia umaskini, ilibidi kuwasaidia maskini zaidi katika kazi zao, kwa sababu “ili kujitoshereza kuwasaidia wahitaji… ni lazima kufanya kazi kwa bidii... Njia hii ya maisha ni ya faida si tu kwa kuutiisha mwili, bali pia kuwa na upendo kwa jirani, ili kwa njia yetu Mungu awalishe vya kutosha ndugu zetu walio dhaifu”.

Huko Kaisaria, ambako aliishi Askofu Basili Mkuu, alijenga mahali palipojulikana kwa jina la Basiliadi, palipojumuisha nyumba za kulala wageni, hospitali na shule za maskini na walemavu. Mtawa, hakuwa mtu wa kujinyima tu, bali pia ni mtumishi. Mtakatifu Basil alionesha dhahiri kuwa, ili kuwa karibu na Mungu, ni lazima mtu awe karibu na maskini. Upendo wa kweli ni kigezo cha utakatifu. Yaani kusali na kujali, kutafakari na kuponya, kuandika na kukaribisha: kila kitu kilikuwa fundisho la upendo uleule wa Kristo. Katika nchi za Magharibi, Mtakatifu Benedicto wa Norcia alitunga kanuni ambayo ingekuwa uti wa mgongo wa roho ya kimonaki-Ulaya. Kuwakaribisha maskini na mahujaji ni kipaumbele: “Maskini na mahujaji wanapaswa kupokelewa kwa uangalifu na ukarimu wote, kwa kuwa ndani yao ndiko Kristo amepokelewa”.

Ndugu msomaji/msikilizaji, haya hayakuwa maneno tu: kwa karne nyingi monasteri za wabenediktini zilikuwa mahali pa kimbilio la wajane, watoto walioachwa, mahujaji na ombaomba. Kwa Benedicto, maisha ya pamoja ni shule ya upendo. Kazi ya mikono haikuwa na kazi ya vitendo tu, bali pia iliunda moyo wa huduma. Hii iliwafanya watawa kushiriki katika kuwatunza wagonjwa na kuwasikiliza walio hatarini zaidi ili kumkaribisha Kristo anayekuja katika nafsi ya maskini na mgeni. Leo, katika Monasteri za Benedictini ukarimu umebaki kuwa ishara ya Kanisa linalofungua milango yake, kukaribisha bila kuuliza, na kuponya bila kudai chochote kama malipo. Kwa muda mrefu sasa, monasteri za wabenediktini zimebaki kuwa mahali pa kuishi pamoja ambapo watawa wa kiume na kike wanaima, wanazalisha chakula, wanatengeneza dawa na kuwapa maskini, wanaishi maisha ya unyenyekevu, wakitoa huduma kwa wahitaji zaidi.

Kazi yao ya kimya kimya imekuwa chachu ya ustaarabu mpya, ambapo maskini hawatazamwi kama tatizo la kutatuliwa, bali ni ndugu wa kukaribishwa. Kanuni ya kugawana, kufanya kazi pamoja na kuwasaidia wanyonge imekuwa chanzo cha uchumi wa mshikamano, tofauti na mantiki ya kujirimbikizia mali. Ndugu msomaji/msikilizaji, ushahidi wa watawa unaonesha kwamba umaskini wa hiari, sio taabu, bali ni njia huru na shirikishi. Watawa hawa hawajiwekei kikomo katika kuwasaidia masikini: bali wao ni majirani na ndugu katika Bwana mmoja. Ukarimu ni chemichemi ya vifungo vyao vinavyounda fumbo la uwepo wa Mungu kwa wadogo. Mbali na utoaji wa nyenzo, monasteri zimesaidia sana kukua kwa utamaduni na malezi ya kiroho ya fadhila ya unyenyekevu. Wakati wa tauni, vita na njaa, monasteri pamekuwa mahali ambapo wahitaji walipata mkate na dawa, lakini pia walipata hadhi na uhuru wa kuongea na kupaza sauti zao.

Ndugu msomaji/msikilizaji, hapa ndipo watoto yatima walisomeshwa, wakajifunza kilimo, ujenzi na kupata mafunzo na mbinu mbalimbali za kimaarifa ikwemo kusoma na kuandika. Maarifa yalishirikiwa kama zawadi na wajibu. Abate alikuwa mwalimu na baba, na monasteri ilikuwa ni shule ya kitawa, mahali pa uhuru kwa njia ya ukweli. Kama Yohana Cassian aandikavyo; “mtawa lazima kuwa na sifa ya “unyenyekevu wa moyo… ambao unaogopa majivuno, na kufumbatia maarifa angavu yenye utimilifu wa mapendo”.  Kwa kuunda dhamiri na kushirikisha hekima, watawa walichangia ufundishaji wa ukristo mwambata. Utamaduni wa kiimani, ulishirikishwa kwa usahili. Maarifa, yakiangazia tendo la hisani na kuwa huduma. Maisha ya kitawa yalijidhihirisha yenyewe kama mtindo wa utakatifu na njia thabiti ya majiundo ya kijamii.

Ndugu msomaji/msikilizaji, tamaduni ya kimonaki inatufundisha kwamba sala na upendo, ukimya na huduma, zahati na hospitali zinaunda “corporale” yaani kitambaa cha kiroho. Monasteri ni mahali pa kusikiliza na kutenda, mahali pa kuabudu na kushirikishana. Mtakatifu Bernard wa Clairvaux, mwanamapinduzi mkuu wa majiundo ya ki-Cistercian, alitibitisha hitaji la kuwa na kiasi katika maisha, hasa katika vyumba vya ndani vya kitawa, yaani chumba cha mapokezi, chumba cha kubadilishia mavazi ya kimonaki, na chumba cha starehe, huko pia wamjali maskini”.

Kwake yeye, huruma haikuwa chaguo, bali njia ya kweli ya kumfuata Kristo. Kwa hiyo, endapo maisha ya kimonaki ni aminifu kwa wito wake wa asili, yanaonesha kwa dhati kuwa Kanisa ni bibi arusi wa Bwana pale tu linapokuwa dada wa maskini. Clauzura si tu kimbilio kutoka kuepa malimwengu, bali pia ni shule ambayo mtu hujifunza kutumikia vyema. Pale ambapo watawa na wa kiume na kike wamefungua milango yao kwa masikini, ndipo Kanisa lilipojifunua kwa unyenyekevu na uthabiti na kuwa, tafakari hazizuii huruma, bali zinadai huruma iwe tunda lake safi kabisa.

Ndugu msikilizaji, tumefikia hapa kwa leo katika mwendelezo wa barua ya kitume, usikose kutufuatilia katika vipindi vijavyo.

DILEXI TE 8

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here

 

26 Novemba 2025, 13:57