Katika Dilexi Te:Kanisa linafungamanisha na wanyonge katika kiini chake
Na Padre Angelo Shikombe-Vatican.
Mpendwa Msomaji/ msikilizaji wa Radio Vatican, tunakuletea mwendelezo wa makala ya wosia wa “Dilexi Te” yaani “Nimekupenda” wa Papa Leo XIV, uliotiwa saini mnamo tarehe 4 Oktoba 2025, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Fransisko wa Assis. Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa waraka huu unaoitwa “DILEXI TE” yaani “nimekupenda” akinukuu kutoka kitabu cha Ufunuo 3:9 sehemu inayosema: “…tazama, nitawafanya waje na kusujudu mbele ya miguu yako, nao watatambua ya kuwa nakupenda”. Leo tuendelee sura ya tatu inalielezea Kanisa lililo kwa ajili ya maskini.
Ndugu msomaji/msikilizaji, siku tatu baada ya Baba Mtakatifu Fransisko kuchaguliwa, mtangulizi wake alionesha hisia na shauku yake ya kuhudumia maskini, taswira iliyo wazi kanisani na kutaka kuona Kanisa linalomwelekea maskini na liko kwa ajili ya maskini. Shauku hii inaakisi uelewa wa Kanisa likiwakumbuka maskini wanaoteseka kwa mfano wa mwanzilishi wake aliyeteseka. Kwa kuwa Kanisa limeitwa kujifungamanisha na wanyonge katika kiini chake hakuna mashaka juu ya ujumbe wake kwa maskini. Tunautangazia ulimwengu kuwa “hakuna utengano kati ya imani na maskini”. Kwa mlengo huu, tunao ushahidi wa kutosha kutoka kwa wanafunzi wa Yesu Kristo ulioenea takribani kwa milenia mbili.
Ndugu msomaji/msikilizaji urithi wa kweli wa Kanisa ni uwepo wa maskini. Mtakatifu Paulo anatukumbusha kuwa kati ya jamii chipukizi za kikristo, si wengi walikuwa wenye busara kadiri ya matakwa ya kimwili, si wengi walikuwa wenye nguvu, na si wengi wlizaliwa katika familia tajiri (1Cor 1:26). Hata hivyo, pamoja na umaskini wao jamii ya kwanza ya wakristo walijua hitaji la kuwajali walio katika mahangaiko. Mwanzoni mwa ukristo Mitume waliwawekea mikono wale watumishi saba waliochaguliwa kutoka kwenye jamii. Na wakawapokea katika huduma, huku wakiwapa majukumu ya kuhudumu katika jamii kama mashemasi “diakonia” (kwa kigriki) wa Mitume (Acts 6:1-5). Umuhimu wao ulikuwa ni kuwapa nafasi Mitume kuhudumu kikamilifu juu ya Neno na kutoka kundi hili Stefano alimwaga damu kwa ajili ya Kristo. Ushuhuda wake wa kumjali maskini na ufia dini vimeunganika. Baada ya karne mbili kupita Shemasi Laurence alionesha uaminifu wake kwa Kristo kwa namna ya kuunganisha kifo dini na huduma kwa maskini.
Katika simulizi la Mtakatifu Ambrojo, tunajifunza kuwa Shemasi katika mji wa Roma katika upapa wa Papa Sixtus II, alilazimishwa na utawala wa Roma kufungua hazina ya Kanisa. “Siku hiyo hiyo alichukua maskini akaenda nao. Alipoulizwa ni wapi wametunza hazina ya Kanisa aliwaonyesha kuwa ni maskini hawa ndiyo hazina ya Kanisa. Naye Mtakatifu Ambrojo anasema ni hazina ya namna gani inayoweza kulinganishwa na wale Yesu aliowapendanda mwenyewe? Ikumbukwe kuwa wahudumu wa Kanisa hawapaswi kupuuzia huduma kwa maskini na kujirimbikizia mali kwa manufaa yao wenyewe. Kazi hii ya kuwatunza maskini inatekelezwa kwa imani na hekima na yeyote anayejinufaisha nayo anatenda kosa la jinai, lakini kama anashiriki kwa uaminifu kuwapatia maskini riziki yao anatenda tendo la huruma.
Ndugu msomaji/msikilizaji, Mababa wa Kanisa walihusiana kwa karibu sana na maskini. Kutoka karne ya kwanza, Mababa wa Kanisa wanatambua ndani ya maskini namna ya upendeleo wa kipekee wa kumfikia Mungu. Ukarimu unaotolewa kwa wenye shida haukutazamwa kama fadhila ya kimaadili, bali ulikuwa ni kielelezo wazi cha imani juu ya Neno aliyefanyika mwili. Jamii ya waamini, inayoongozwa na nguvu ya Roho Mtakatifu ina chimbuko lake katika ukaribu na maskini, ambaye si nyongeza bali ni sehemu ya mwili hai wa fumbo la Kristo. Kwa mfano, Mtakatifu Inyasi wa Antiokia alipokuwa anakabiri kifo-dini aliiandikia Jumuyiya ya Smyrna ili isipuuze sughuli za ukarimu kwa wahitaji, akiwaonya wasikengeuke na kuishi kinyume cha matakwa ya Mungu, bali wawachukulie wale wenye maoni tofauti kwa heshima kwa ajili ya neema ya Kristo aliyekuja kwetu. Huenda maoni yao yakawa kinyume na mpango wa Mungu, maoni yasiyo ya upendo, yasiyojali maskini, yatima, wanaonyanyaswa, wenye njaa, wenye kiu yanapingana na mpango wa Mungu. Askofu Polycarp wa Smyrna alieleza kuwa wahudumu wa Kanisa wawahudumie maskini, nao makuhani wanapaswa kuwaonea huruma wote wakiwakusanya waliotawanyika, wakiwatembelea wagonjwa, na kuwakumbuka wajane, yatima, na maskini, na kuwashibisha kwa neema zinazotoka kwa Mungu na ukarimu wa watu. Kwa ushuhuda wa aina hizi mbili tunalitazama Kanisa kama “Mama wa maskini, sehemu yenye haki na yenye mapokezi yenye weledi.
Ndugu msikilizaji, Kanisa liko kwa ajili ya maskini. Mtakatifu Justini kwa upande wake, aliyeandika ungamo lake la kwanza kwa mfalme Adrian, Seneti na watu wa Roma, akieleza kwamba wakristo huleta yote wawezayo kwa wale wenye uhitaji kwa sababu wanawaona kuwa ni kaka na dada katika Kristo. Akiandika juu ya kusanyiko lililokusanyika katika maombi siku ya kwanza ya Juma, alisisitiza kwamba katika moyo wa liturujia ya Kikristo, haiwezekani kutenganisha ibada kwa Mungu kutokana na utoaji wa huduma kwa maskini. Kwa maana hii, wale wenye uwezo wanaweza kujitolea kwa namna inayofaa na kile kitakachopatikana kipelekwe kusaidia yatima, wajane, wagonjwa, wafungwa, na wenye mahitaji mbalimbli. Kwa taswira hii, Kanisa la kwanza linaonekana kutokujitenga na shughuli za kijamii na imani. Imani ambayo haina ushuhuda katika maisha halisi ya kijamii imekufa alifundisha Mtume Yakobo (Yak 2:17).
Ndugu msikilizaji, Mtakatifu Yohana Krizostom ni miongoni mwa mababa wa mashariki, huenda pia alikuwa kati ya wahubiri maarufu juu ya haki-jamii. Mtakatifu Yohana Krizostom, alikuwa Askofu Mkuu wa Cosntantinopo aliyeishi kati ya mwaka 300 na 400 AD. Katika homilia zake, aliwaasa waamini kumtambua Kristo katika mahitaji. Hasa anapouliza; “Unataka kuuheshimu mwili wa Kristo? Usiruhusu utukanwe ndani ya washiriki wake, yaani ndani ya maskini, )asio na nguo za kujifunika, usiuheshimu mwili wa Kristo hapa kanisani kwa vitambaa vya hariri, huku nje ukiupuuza unapoteseka na baridi na uchi… (Mwili wa Kristo juu ya madhabahu] hauhitaji mavazi, bali roho safi; wakati mtu wa nje anahitaji uangalizi mkubwa. Basi, tujifunze kumfikiria na kumheshimu Kristo kama apendavyo. Heshima inayopendeza zaidi unayoweza kumpa yule kumheshimu ni kufanya matamanio yake mwenyewe, si yale tunayoyawazia sisi... Vivyo hivyo nanyi mpeni heshima aliyoamuru, na mwacheni maskini afaidike na utajiri wenu. Kwani Mungu hahitaji vyombo vya dhahabu, bali roho za dhahabu.”
Akithibitisha hilo anaendelea kufundisha kwa ushujaa kuwa; “Ikiwa waamini hawatakutana na Kristo katika maskini wanaosimama mlangoni, hawatakutana naye pia katika kumwabudu madhabahuni” Yohane Krizostom anaendelea kusema: “Kristo ana faida gani akiadhimishwa kwenye meza ya dhabihu katika vyombo vya dhahabu, huku yeye mwenyewe akifa kwa njaa mbele ya maskini? “Walisheni wenye njaa kwanza, na baadaye ipambeni madhabahu kwa masalia.” Aliyeielewa Ekaristi kama Sakramenti, mapendo na haki vinavyoitangulia na kuikamilisha. Upendo na haki unapaswa kudumisha Ekaristi kwa njia ya upendo na umakini kwa maskini. Kwa hiyo, ukarimu si jambo la hiari bali ni takwa la ibada ya kweli.
Mtakatifu Chrizostom kwa nguvu alishutumu utajiri wa kupindukia unaohusishwa na kutowajali maskini. Kuwaelekea maskini kwa moyo wote na si kutimiza hitaji la kijamii, ni sharti la wokovu, ambalo linalaani utajiri usio wa haki. "Inapotokea kuna baridi kali na maskini amelala kwenye mitaro akijifunika vitambaa, anatetemeka, anaganda, pengine hata kufa, hata hivyo, wewe unampita huku umelewa, unatarajia nini mbele ya Mungu? Unatarajiaje Mungu kukukomboa na balaa?... Unaipamba maiti isiyo na hisia, na kuivisha nguo za thamani miili yenye kuharibika isiyoelewa tena maana ya heshima, wakati huo unamdharau yule anayejisikia maumivu, aliyeraruliwa, anayehangaika na njaa na baridi.” Mwono huu wa kina wa kijamii unamfanya Mtakatifu Krizostom athibitishe kwamba “kutowapa maskini ni kuwaibia na kuwanyang’anya mali zao”. “Wao wanaishi, kwa sababu tulicho nacho ni mali yao”.
Ndugu msikilizaji, tumefikia hapa kwa leo katika mwendelezo wa barua ya kitume, usikose kutufuatilia katika vipindi vijavyo.