Tafuta

2025.11.16 Chakula cha Papa na Maskini. 2025.11.16 Chakula cha Papa na Maskini.  (@Vatican Media)

Katika Dilexi Te:Msisitizo wa“kumpenda jirani yako kama nafsi yako”

Mahusiano yetu na Bwana katika ibada,yanalenga kutuokoa na hatari ya kuishi maisha yetu tukifuata vionjo vyetu wenyewe.Badala yake tunashirikishwa hali ya neema ambayo huwazunguka wale wanaopendana na kushirikiana kwa kila jambo.Katika mazingira haya,Yesu anatushauri;unapokuwa na sherehe,usialike rafiki zako,ndugu zako,au watu matajiri,ambao pia wanaweza kukualika na hivyo kupata malipo yako.

Na  Padre Angelo Shikombe – Vatican.

Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, tunakuletea mwendelezo wa makala ya Wosia wa “Dilexi Te” yaani “Nimekupenda” wa Papa Leo XIV, uliotiwa saini mnamo tarehe 4 Oktoba 2025, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Fransisko wa Assis. Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa waraka huu unaoitwa “DILEXI TE” yaani “Nimekupenda” akinukuu kutoka kitabu cha ufunuo 3:9 sehemu inayosema: “…tazama, nitawafanya waje na kusujudu mbele ya miguu yako, nao watatambua ya kuwa nakupenda.” Leo tuendelee kutazama sura ya Pili inayoelezea namna Mungu anavyomchagua maskini na kumtazama kwa namna ya pekee, hasa katika mafundisho ya mababa wa Kanisa.

Ndugu Msomaji/msikilizaji, huruma kwa maskini katika Maandiko Matakatifu imefafanuliwa kinagaubaga na waandishi mbalimbali, na katika nyakati mbalimbali. Mwinjili Yohane anaandika: wale asiowapenda ndugu zao ambao wanaonekana hawawezi kumpenda Mungu asiyeonekana (1Yh 4:20). Vivyo hivyo, akijibu swali la waandishi, Yesu ananukuu amri kuu mbili za zamani yaani ile amri inayosema; “mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote (Kumb 6:5) na ile amri inayosema “umpende jirani yako (Wal 19:18), huku akizifanya kuwa amri moja. Mwinjili Marko anaitumia amri hii ya mapendo yaani; kumpenda Mungu kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote, na amri ya pili ni kumpenda jirani yako kama nafsi yako (Mk 12:29-31).  Sehemu ya kitabu cha Walawi inatufundisha upendo kwa jirani ambapo mahali pengine inakazia juu ya heshima kwa jirani na pengine kumpenda hata adui yako. Kama punda wa adui yako anapotea mrudishe, na kama punda wa adui yako anaelemewa na mzigo mfungue (Kut 23: 4-5). Inasisitizwa thamani ya heshima kwa wengine hata kama ni adui anastahili kusaidiwa.

Ndugu Msomaji/msikilizaji, mafundisho ya Yasu juu ya ukuu wa upendo kwa Mungu yanatimilika pale anaposisitiza kuwa huwezi kumpenda Mungu bila kuwapenda maskini. Upendo kwa jirani unadhihirisha namna tunavyompenda Mungu, kama Mwinjili Yohane anavyoshuhudia kuwa; hakuna mtu aliyewahi kumwona Mungu; kama tukipendana sisi kwa sisi, maana yake Mungu anaishi ndani yetu na pendo lake limekamilika ndani yetu…kwa maana Mungu ni upendo, na wale wanaofumbatia upendo wanamkaribisha Mungu ndani yao (1 Yoh 4:12, 16). Amri hizi mbili za upendo ingawa zinatofautiana lakini zimeungana na hazitenganishwi, hata katika mazingira ambapo Mungu hatajwi waziwazi, bado kazi ya ukarimu wa Mungu hutendeka. Yesu aliwaambia wanafunzi wake; “Amini nawambieni, mnapomtendea mema kati ya hawa walio wadogo mnanitendea mimi” (Mt 25:40). Kwa mantiki hii, matendo ya huruma ni alama inyohalalisha ibada ambayo katika kumsifu Mungu inatuwezesa kupokea mabadiliko ya kiroho yanayoletwa na Roho wa Mungu ili tuweze kuwa taswira ya Kristo na huruma yake kwa wanyonge.

Ndugu Msomaji/msikilizaji, mahusiano yetu na Bwana katika ibada, yanalenga kutuokoa na hatari ya kuishi maisha yetu tukifuata vionjo vyetu wenyewe. Badala yake tunashirikishwa hali ya neema ambayo huwazunguka wale wanaopendana na kushirikiana kwa kila jambo. Katika mazingira haya, Yesu anatushauri; unapokuwa na sherehe, usialike rafiki zako, ndugu zako, au watu matajiri, ambao pia wanaweza kukualika na hivyo kupata malipo yako. Badala yake, alika maskini, vilema, vipofu, na utabarikiwa, kwa kuwa hawa hawana cha kukulipa (Lk 14: 12-14).  Mwaliko wa Bwana katika kumjali maskini unatimilika katika ile mithali ya hukumu ya mwisho (Mt 25: 31-46), ambayo inatoa maelezo juu ya heri ya mwenye huruma. Katika methali hii, Bwana anatoa ruksa ya kukamilisha maisha yetu. Kama tunatafuta utakatifu unaopendeza machoni pa Mungu, kipengere hiki kinafafanua namna tutakavyohukumiwa mbele ya Mungu. Injili inapaswa kuwekwa katika matendo bila “uwalakini wowote”. Bwana wetu anasistiza kuwa utakatifu haupo bila kutimiza haya masharti. Katika jamii ya kwanza ya wakristo, matendo ya huruma yalikuwa ndiyo msingi wa maisha ya kila siku na siyo kitu cha kusomea na kuweka mikakati endelevu. Walimwiga Yesu kristo kama alivyofanya katika injili.

Ndugu Msomaji/msikilizaji, waraka wa Yakobo unafafanua kwa kina tatizo la kimahusiano kati ya tajiri na maskini huku wakiulizwa waamini juu ya uhalali wa kimaadili na kiimani: ina maana gani ndugu kama ukisema una imani ambayo haifanyi kazi? Hiyo imani inaweza kukuokoa? Kama ndugu yako yu uchi au hana chakula na ukamwambia; nenda na amani; ua jifunike na aule ushibe, wakati haumpi chochote cha kumsaidia katika mahitaji yake. Nini wema wake? kwa hiyo, imani kwa namna ilivyo, kama haifanyi kazi imekufa (Yak 2: 14-17). Mtume Yakobo anaendelea “dhahabu na almasi yako imeharibika na itakugharimu. Umejiwekea hazina kwa siku za soni, Sikiliza! Mishahara ya wakulima mliokata mashamba yao, mkiwazuia kwa hila, wanapiga kelele, na vilio vya wavunaji vimefika masikioni mwa Bwana wa majeshi. Mmeishi duniani kwa anasa; na mmejinenepesha mioyo yenu katika siku ya machinjo” (5:3-5). Haya ni maneno mazito hata kama hatuyapokea.

Ndugu msomaji/msikilizaji, sehemu nyingine ni ile ya waraka wa kwanza wa Yohane inayokanusha kuwepo kwa upendo wa kimungu kwa mtu mwenye uwezo anayemtupilia mbali maskini (Yoh 3:17). Ujumbe wa Mungu ni “wazi na wa moja kwa moja, rahisi sana na wa ufasaha, hivi kwamba hakuna tafsiri ya kikanisa ina haki ya kuurekebisha. Tafakari ya Kanisa juu ya maandiko haya haipaswi kufichwa au kudhoofishwa, badala yake ituhimize tukubali mashauri yake kwa ujasiri na bidii. Nadharia zipo kuelezea uhalisia na kutuunganisha na uhalisia huo na sio kututenga nao. Tunayo mifano hai ya Kanisa katika ukarimu na utoaji huduma za jamii za kikristo. Tunaweza kuona jamii ya kwanza ya wakristo ilivyowajali wajane (Act 6:1-6).

Halikuwa tatizo dogo kutokana na ukweli kwamba baadhi ya hawa wajane walitoka nchi zingine na walitengwa kwa sababu walikuwa wageni. Kwa kweli, kipindi kinachosimuliwa katika Matendo ya Mitume kinaangazia jambo fulani kutoridhika kwa upande wa Wagiriki na Wayahudi ambao walikuwa Wagiriki kitamaduni. Mitume hawajibu kwa maneno ya kufikirika, bali kwa hisani wakitambua huduma kwa wajane wakiiomba jamii kutafuta watu wenye hekima na busara ambao wangeweza kuwapa chakula huku Mitume wakiendelea kuhubiri Neno. Mtume Paulo alipoenda Yerusaleme kuongea na Mitume ili aone kama mwelekeo wake ni sahihi alikumbushwa kutowasahau maskini. Kwa hiyo aliweka mpango mkakati wa ukusanyaji wa misaada ili kuhudumia jamii za maskini, huku akifundisha kuwa “Mungu humpenda mtu atoae kwa ukarimu (2Cor 9:7).

Ndugu Msomaji/msikilizaji, Neno la Mungu linatuasa tena kufungua mioyo yetu na kuonesha matendo ya ukarimu ambayo yatawasaidia wanaoteseka, kwani Mungu anawapenda kwa namna ya pekee. Maandiko yamesheheni ahadi mbalimbali kwa wale wanaosaidia wahitaji kwa moyo wote. Anayemkarimu maskini anawekeza mbele ya Mungu na atalipwa kwa ukamilifu (Mithali 19:17). “Toa tu, nawe utarudishiwa…kwa kiwango unachomtendea mwingine nawe utatendewa vivyo hivyo” (Lk 6:38).  Hapo ndipo mtaweza kung’aa kama pambazuko, na uponyaji wenu utaenea kwa haraka (Is 58:8). Kwa jambo la ukarimu jamii ya kwanza ya wakristo haikuwa na mashaka. Maisha ya jumuyiya ya kwanza ya mitume yaliyoandikwa katika Biblia na kurithishwa kwetu kama ufunuo wa Neno la Mungu, ni mfano wa kuigwa, na ushuhuda wa imani inayofanya kazi kwa tendo la ukarimu na kuvutia wengi kwa vizazi vingi. Neno hili limevutia mioyo ya watu wengi, kama mbegu ya tunda ambayo haitakoma kuzaa matunda mengi.

Ndugu msikilizaji, tumefikia hapa kwa leo katika mwendelezo wa barua ya kitume, usikose kutufuatilia katika vipindi vijavyo.  Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Angelo Shikombe. 

Dilexi Te 5

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here

21 Novemba 2025, 11:49