Katika Dilexi Te:“Yesu anasisitiza upendo kwa Bwana&upendo kwa Maskini
Na Padre Angelo Shikombe - Vatican.
Mpendwa msomaji na msikilizaji wa Radio Vatican, tunakuletea makala ya Wosia wa Kitume wa “Dilexi Te” yaani “Nimekupenda” wa Papa Leo XIV, uliotiwa saini mnamo tarehe 4 Oktoba 2025, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Francis wa Assisi, na ukiwa Wosia wake wa kwanza katika Upapa wake ambao ni mwendelezo wa Wosia wa Papa Francisko wa “Dilexit Nos” kuhusu “Upendo wa kibinadamu na Upendo wa Moyo wa Yesu Kristo,” uliochapishwa tarehe 24 Oktoba 2024. Kufuatia na mwendelezo huo ulioachwa na Hayati Papa Francisko, Mfuasi wake aliuhitimisha Wosia Mpya.
Mpendwa msikilizaji, Baba Mtakatifu Leo XIV mnamo tarehe 4 Oktoba 2025 alitoa Wosia wake wa Kwanza wenye kichwa cha habari “DILEXI TE” yaani “nimekupenda” unaotokana na nukuu kutoka kitabu cha Ufunuo 3:9 ukisema: “Tazama, nitawafanya waje na kusujudu mbele ya miguu yako, nao watatambua ya kuwa nakupenda”. Maneno haya ya Bwana yanayoilenga Jumuiya ya Kikristo ambayo tofauti na jumuiya zingine haina ushawishi wala vyanzo, lakini ilitendewa kwa ukatili, uonevu na dharau. Hata hivyo, Bwana anaiona kuwa inavyo vichache pamoja na nguvu kidogo, na anaahidi kuyakusanya mataifa bele yake (Ufunuo 3:8-9). Andiko hili linatukumbusha maneno ya wimbo wa Bikira Maria katika Injili ya Mtakatifu Luka 1: 52-53 yanayosema; “amewashusha wenye nguvu kutoka viti vyao vya enzi na akawakweza wanyenyekevu; amewashibisha wema wenye njaa na amewaacha matajiri waende mikono mitupu.
Andiko hili la upendo, linalotoka katika kitabu cha ufunuo, linaaksi fumbo la ajabu ambalo Papa Fransisko alilitafakari katika waraka wake unaoitwa “Dilexit Nos” juu ya upendo wa kibinadamu na upendo wa kimungu wa moyo wa Yesu Kristo. Tunamwona Yesu akijiambatanisha mwenyewe na makundi ya chini katika jamii na kwa namna zake, yalivyo dhaifu, yanavyodharauliwa na kuteswa. Tunapoutafakari upendo wa Kristo, tunavutwa sana kuwa makini hasa tunapoona mahangaiko na mahitaji ya wengine, na tunaimarishwa katika juhudi zetu kuishirikisha kazi yake ya ukombozi kama chombo cha uenezaji wa pendo lake. Kwa mantiki hii, katika mwendelezo wa Wosia wa kipapa wa “Dilexit Nos”, Papa Fransisko kwa nyakati zake za mwisho za utume wake aliliandaa Kanisa kumjali maskini, akiweka kichwa cha habari “Delixi Te” yaani “nimekupenda”, kana kwamba Kristo anaongea maneno haya kwa kila mmoja wetu. Baba Mtakatifu Leo XIV anayo furaha kuendeleza andiko hili katika upapa wao, ili kwamba wakristo wathamini upendo wa Kristo na wito wake wa kumjali maskini. Naye Baba Mtakatifu Leo anasisitiza njia hii ya utakatifu. Ndani ya wito huu, tunaliona pendo la Kristo lililofunuliwa, hisia zake za ndani na maelekeo yake yenye kuigwa na kila mtakatifu.
Ndugu msikilizaji na Msomaji, Wosia wa Papa Leo XIV umegawanywa katika sura tano; sura ya kwanza inajikita kuelezea msingi wa pendo la Mungu kwa maskini, sura ya pili inaelezea namna Mungu anavyomchagua maskini, sura ya tatu inalielezea Kanisa lililo kwa ajili ya maskini, Sura ya nne inajikita katika historia endelevu, na sura ya tano na ya mwisho inaelezea changamoto endelevu. Ndugu msikilizaji, Wosia wa Baba Mtakatifu Leo XIV, unaanza kwa kutafakari juu ya mitazamo kinzani ambayo daima imekuwepo katika historia ya Kanisa. Tukirejea katika kipindi cha maisha ya Yesu; Wanafunzi wa Yesu walimpinga mwanamke aliyempaka Yesu miguu yake kwa marhamu na kuipangusa kwa kichwa chake wakisema: kwa nini mafuta hayo yatumike namna hii? Kwa kuwa marhamu hiyo ingeweza kuuzwa kwa fedha nyingi na pesa wakapewa maskini.
Ndugu msikilizaji, hiyo ndiyo ilikuwa hoja ya Mitume wa Yesu. Hata hivyo Bwana aliwaambia, “mnao daima maskini lakini hamtakuwa daima nami (Mt 26:8-9, 11). Mwanamke huyo anayeongelewa katika Injili ya Matayo 26: 8-9, 11, alimwona mnyonge na maskini ndani ya Masiha msulibiwa ambaye kwake angempa pendo lake lote. Hivyo mwanamke huyo aliona ni faraja kubwa ambayo angemjalia yule amabaye angevikwa taji la miiba. Lilikua ni tendo dogo la kujali ambalo lingeleta faraja kubwa kwa anayeteseka. Yesu alilijua hilo na akawaambia wanafunzi wake kuwa tendo hilo litakumbukwa daima wakati Injili hii itakapohubiriwa ulimwenguni kote na yeye atakumbukwa (Mt 26:13). Usahili wa alama hii ya mwanamke unasema mambo mengi. Hakuna alama ndogo ya kujali inayosahauliwa, hasa wanapotendewa wenye mahangaiko, wapweke, na wahitaji kama Bwana alivyofanya kipindi chake.
Ikumbukwe kuwa; Yesu anasisitiza upendo kwa Bwana na badaye upendo kwa maskini. Ni Yesu anayetuasa kuwa maskini tunao siku zote (Mt 26:11) naye pia anawaahidi wafuasi wake atakuwa nao (Mt 28:20). Tunapotafakari mafundisho yake yanayosema: utakavyomtendea mmoja wa hawa walio wadogo umenitendea mimi (Mt 25:40), tujue wazi kuwa; si ukarimu wa kibinadamu peke yake unaohitajika, bali ni ufunuo unaowagusa wasiojiweza na njia ya kukutana na Bwana wa historia. Kwa njia ya maskini Mungu anaongea nasi. Papa Fransisko akielezea namna alivyochagua jina, baada ya kuchaguliwa kuwa Papa, Kardinali rafiki yake alimkumbatia na kumwambia: “usiwasahau maskini”. Vivyo hivyo viongozi wa Kanisa walivyomfanyia Mtakatifu Paulo alipoenda Yerusalem kuthibitisha utume wake (Gal 2:10). Hata baada ya miaka kupita, Mtume Paulo alithibitisha ari yake ya kufanya hivyo.
Huduma kwa maskini ilikuwa kipaumbele cha Mtakatifu Fransisko wa Assis. Katika nafsi ya mwenye ukoma, Kristo mwenyewe alimkumbatia Francisko na kuyaongoa maisha yake. Hata leo, Mtakatifu Fransisko, kama maskini wa Assis, anaendelea kututia hamasa kwa mifano yake. Baada ya karne nane kupita, Mtakatifu Fransisko alihamasisha upyaishwaji wa kienjili kwa wakristo na jamii ya wakati huo. Kwa umahiri mkubwa Mtakatifu Fransisko aliguswa sana na mazingira ya umaskini katika jamii yake. Maisha yake yanaendelea kukonga nyoyo za waamini wengi na wasioamini huku ikibadilisha historia. Mtaguso wa Vatacan II uliendeleza hatua hii, pale Papa Paulo VI alipochaguliwa alinukuu kuwa: Mithali ya zamani ya Msamaria ilitumika kama mwongozo wa maisha ya kiroho ya Baraza huku akiwahakikishia kuwa, kuwaelekea maskini ni chanzo cha uhuisho, si tu kwa Kanisa, bali kwa jamii pia kama kila mmoja wetu atajibandua kutoka kwenye makandokando ya ubinafsi na kufungua masikio yetu kusikiliza kilio cha wahitaji.
Ndugu msikilizaji na Msomaji, tumefikia hapa kwa leo katika mwanzo na mwendelezo wa Wosia wa Kitume, usikose kutufuatilia katika vipindi vijavyo.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here