Tafuta

2025.08.03 Picha ya Siku ya vijana wakati wa Misa huko Tor Vergata. 2025.08.03 Picha ya Siku ya vijana wakati wa Misa huko Tor Vergata.  (@Vatican Media)

Katika Dilexi Te:“Injili inatuonesha kuwa umaskini uko katika kila hatua na utume wa maisha ya Yesu

Ukamilifu wa upendeleo wa Mungu kwa maskini unatimilika katika maisha ya Yesu wa Nazareti anapojifunua kuwa ni masiha mteseka.Kwa umwilisho wake,alijitoa kikamilifu,huku akichukua hali ya mtumwa na kuzaliwa kama mwanadamu na kwa hiyo akatuletea ukombozi.Umaskini wake unajenga msingi wa kuufunua mpango wa upendo wa Mungu kwa neema zake Bwana wetu Yesu Kristo,ambazo,pamoja na kuwa tajiri lakini alijifanya kuwa maskini,ili kwa umaskini wake tupate kuwa matajiri.

Na Padre Angelo Shikombe Vatican.

Mpendwa Msomaji/msikilizaji wa Radio Vatican, tunakuletea mwendelezo wa makala ya wosia wa “Dilexi Te” yaani “Nimekupenda” wa Papa Leo XIV, uliotiwa saini mnamo tarehe 4 Oktoba 2025, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Fransisko wa Assis. Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa waraka huu unaoitwa “DILEXI TE” yaani “nimekupenda” akinukuu kutoka kitabu cha ufunuo 3:9 sehemu inayosema: “…tazama, nitawafanya waje na kusujudu mbele ya miguu yako, nao watatambua ya kuwa nakupenda”. Leo tuitazame sura ya pili inayoelezea namna Mungu anavyomchagua maskini na kumtazama kwa namna ya pekee.

“Ikumbukwe kuwa Yesu Masiha ni maskini.”

Ukamilifu wa upendeleo wa Mungu kwa maskini unatimilika katika maisha ya Yesu wa Nazareti anapojifunua kuwa ni masiha mteseka. Kwa umwilisho wake, alijitoa kikamilifu, huku akichukua hali ya mtumwa, na kuzaliwa kama mwanadamu (Filp. 2:7) na kwa njia hiyo akatuletea ukombozi. Umaskini wake unajenga msingi wa kuufunua mpango wa upendo wa Mungu kwa neema zake Bwana wetu Yesu Kristo, ambazo, pamoja na kuwa alikuwa tajiri lakini kwa ajili yake alijifanya kuwa maskini, ili kwa umaskini wake tupate kuwa matajiri (2Kor 8:9). Injili inatuonesha kuwa umaskini uko katika kila kipengere na utume wa maisha ya Yesu. Tangu alipoingia ulimwenguni, Yesu alijua ugumu wa kukataliwa. Mwinjili Luka anatusimulia namna Yusufu na Maria alipokuwa mbioni kujifungua, walivyofika Bethelehemu, na anaendelea kusema kwa uchungu kuwa, hawakupata mahali pa kujihifadhi (Lk 2:7). Yesu alizaliwa katika mzingira ya kawaida kabisa na kulazwa katika pango la kulishia wanyama; na ili wamwokoe asiuwawe, walikimbilia Misri (Mt 2:13-15).

Ndugu Msomaji/msikilizaji, mwanzoni mwa maisha ya Yesu ya kijamii, baada ya kutangaza mwaka wa Bwana katika sinagogi la Nazareth ambao ungeleta neema na furaha kubwa kwa maskini, hakika umetimia ndani yake, na baada ya hapo alifukuzwa mjini (4:14-30). Alikufa kama kafiri, akitolewa nje ya Yerusalemu ili asulibiwe (Mk 15:22). Hivyo ndiyo umaskini wa Yesu unavyoweza kusimuliwa: alitengwa kama maskini wengine wanavyotengwa na kutelekezwa pembezoni mwa jamii. Yesu ni ufunuo wa upendeleo wa maskini (privilegium pauperum). Alijifunua mwenyewe kwa ulimwengu kama Yeye ni Masiha maskini, anayetoka kwa maskini na yuko kwa ajili ya maskini. Yako mambo mengi juu ya maisha ya kijamii ya Yesu. Mosi, alifanya kazi ya useremala, yaani “téktōn” (cf. Mk 6:3). Hawa walikuwa watu wanaojipatia ridhiki yao kwa jasho la mikono yao. Hawakumiliki ardhi, wahesabika kuwa duni zaidi ya wakulima.

Wakati mtoto Yesu alipotolewa Hekaluni, Yusuf na Maria, wazazi wake walitolea sadaka ya maskini, yaani njiwa wawili na hua wawili (Lk 2:22-24), ambayo kwa maelezo ya kitabu cha Walawi (2:23-28) ilikuwa ni sadaka ya maskini. Tena iko sehemu nyingine ya Injili inayosimulia namna Yesu na Mitume wake walipopita mashambani wakakusanya masuke ya nafaka ili wale (Mk 2: 23.28). Ni maskini tu waliruhusiwa kufanya hivyo mashambani. Tena, Yesu anasema mwenyewe “Mbweha wana mapango, na ndege wana viota vyao; lakini Mwana wa mtu hana mahali pa kulaza kichwa chake” (Mt 8:20; Lk 9:58). Kwa namna hii, Yeye ni mwalimu machinga ambaye umaskini ni kifungo cha umoja wake na Baba. Kuna masharti pia kwa wale wanaopenda kumfuasa katika njia ya ufuasi, ambapo wanapaswa kujikana wenyewe, kutojifungamanisha na vitu, utajiri na ulinzi wa walimwengu kama ishara wazi ya kujikabidhi katika ulinzi na uweza wa Mungu.

Ndugu Msomaji/msikilizaji, mwanzoni mwa utume wake, Yesu alionekana Hekaluni Nazareth akisoma gombo la nabii Isaya na kuutumia utabiri wa kinabii kuwa umetimia ndani yake. “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenipaka mafuta na kunituma niwantangazie maskini habari njema” (Lk 4:18, Is 61:1). Kwa hiyo alijifunua mwenyewe kama ndiye ambaye ajaye ulimwenguni kuwaletea habari njema ya ukaribu wa pendo la Mungu ambalo kwalo ni ukombozi wa waliofungwa na uovu, walio dhaifu na maskini. Ishara zinazoambatana na mahubiri ya Yesu pia ni ufunuo wa pendo na huruma ambao ndani mwake Mungu anawajali wagonjwa, maskini na wadhambi ambao, kwa sababu ya hali yao walisukumwa pembezoni mwa jamii na hata nje ya jamii ya waamini. Anafungua macho ya kipofu, anamponya mkoma, anamfufua mfu na kumtangazia habari njema maskini; ya ukaribu wa Mungu, Mungu akupendaye (Lk. 7:22). Hii ndiyo maana ya kutangaza; Heri walio maskini, kwa maana ufalme wa Mungu ni wao (Lk 6:20). Mungu anaonesha upendeleo kwa maskini, kwa kuwa Neno la Bwana kwanza limeelekezwa kwao. Kwa hiyo,

Baba Mtakatifu Leo XIV analitaka Kanisa kuwa Kanisa la “heri” linalofungua mianya kwa mdogo na maskini kutembea pamoja na maskini mwenzake, ambapo maskini ana nafsi ya upendeleo (Yk 2: 2-4). Wakati huo, maskini na mgonjwa, wanapokosa mahitaji yao ya kila siku, mara nyingi hujikuta wamelazimika kuomba. Hivyo, hubeba hali ya aibu katika jamii wakiamini kuwa ugonjwa na umaskini uliambatanishwa na dhambi. Yesu kwa ujasili anakabiliana na fikra hii akisisitiza kuwa Mungu huwaangazia jua lake na kuwanyeshea mvua wema na waovu (Mt 5: 45). Kwa kufanya hivyo, anapindua kabisa dhana ambayo tunaiona katika hitimisho la mithali ya tajiri na maskini akisema; “mwanangu, kumbuka kuwa uliyapokea mema yako ukiwa ulimwenguni na lazaro akipokea mabaya, sasa anafarijiwa na wewe unateseka (Lk 16: 25).

Ni dhahiri kuwa “imani yetu katika Kristo, ambaye alijifanya kuwa maskini, na alikuwa daima karibu na maskini na waliosetwa, ni msingi wa wajibu wetu kwa maendeleo na ustawi wa jamii ambayo watu wake wametengwa. Mara nyingi nashangazwa kuona kuwa, pamoja na maandiko matakatifu kufafanuliwa kwa uwazi kiasi hiki juu ya maskini, kwa nini watu wengi wanaendelea kufikiri wako salama hata wasipomjali maskini. Hata hivyo, kwa wakati huu, tuzameni katika maandiko yanayotuambia juu ya mahusiano yetu na maskini pamoja n anafasi yao katika taifa la Mungu.

Ndugu Msomaji /msikilizaji, tumefikia hapa kwa leo katika mwendelezo wa Wosia wa Kitume, usikose kutufuatilia katika vipindi vijavyo.

Dilixi te 4

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here

 

20 Novemba 2025, 09:14