Tafuta

2025.11.19 Moja ya picha ya Katekesi. 2025.11.19 Moja ya picha ya Katekesi.  (@Vatican Media)

Katika Dilexi Te:Watu wote wana heshima,uhuru sehemu zao za kuzaliwa,tofauti hazikwepeki

"Tukinuia kufungua zama za utawala wa haki,udugu na mshikamano,Mungu ana nafasi ya pekee moyoni mwake kwa wale wanoteswa na kubaguliwa na anatutaka sisi tulio Kanisa lake,kufanya maamuzi madhubuti yenye kuwaelekea wanyonge." Haya na mengine yamo katika Wosia wa Kitume wa"Dilexi Te"yaani"Nimekupenda"wa Papa Leo XIV."Mungu aliye ngao ya maskini anatangaza kwa njia ya nabii wake Amos ina Isaya,maovu waliyotendewa maskini na kuliasa taifa la Israeli kuwa na wongofu wa ndani."

Padre Angelo Shikombe -Vatican.

Mpendwa Msomaji/msikilizaji wa Radio Vatican, tunakuletea mwendelezo wa makala ya Wosia wa “Dilexi Te” yaani “Nimekupenda” wa Papa Leo XIV, uliotiwa saini mnamo tarehe 4 Oktoba 2025, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Fransisko wa Assis. Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa waraka huu unaoitwa “DILEXI TE” yaani “nimekupenda” akinukuu kutoka kitabu cha ufunuo 3:9 sehemu inayosema: “…tazama, nitawafanya waje na kusujudu mbele ya miguu yako, nao watatambua ya kuwa nakupenda”. Leo tunaendelea na sura ya kwanza inayojikita kuelezea msingi wa pendo la Mungu kwa maskini.

Ndugu Msomaji/msikilizaji, leo tukitazame kipengele cha ubaguzi wa kiitikadi ambacho kimeibuka kidedea katika nyakati za usoni. Tukirudi kwenye kumbukumbu ambazo wakati mwingine “zinatafsiriwa” ili kutushawishi kuwa hali ya maskini si mbaya kiasi hicho, zinapotosha uhalisia. Baadhi ya sheria za kiuchumi zimeweza kukua bila kugusa mfungamano wa ukuaji wa maendeleo ya kiutu. Uchumi unakua na kusababisha ukosefu wa kiusawa ambao unajitanabaisha na mifumo mipya ya umaskini iliyoibuka hivi siku za usoni. Uvumi unaosema kuwa ulimwengu mambo leo umepunguza umaskini unatokana na vyanzo vya taarifa zilizopitwa na wakati, ambazo siyo za uhalisia wa leo. Wakati mwingine, kwa mfano, kukosekana kwa nishati ya umeme haikuchukuliwa kama alama za umaskini, wala haikuwa alama ya mahangaiko kwa kukosa hitaji msingi. Umaskini unapaswa kufafanuliwa katika mkitadha wa upatikanaji wa fursa halisi katika kila wakati wa historia.

Ndugu msomaji/msikilizaji, tukirudi nyuma kidogo kuangalia maisha halisi ya miaka ya 1984 makala ya Jumuiya ya Ulaya ilitangaza kuwa “maskini ni mtu, familia na vikundi vya watu ambao rasilumali zao za vitu, kiutamaduni na kijamii hazitoshelezi kutimiza mahitaji yao ya msingi ndani ya nchi yao wanamoishi. Kama tunakubaliana kuwa watu wote wana heshima iliyo sawa, uhuru wa sehemu zao za kuzaliwa, tofauti zilizopo katika ya nchi na nchi hazikwepeki.

Ndugu msomaji /msikilizaji, maskini hawako pale kwa bahati mbaya, au kwa upofu na dhamira mbaya. Ni dhahiri, kati ya maskini kuna wale wasio jishughulisha kufanya kazi, pengine kutokana na historia ya mababu zao waliokufa wakiwa maskini. Hata hivyo, kuna watu wengi sana wake kwa waume, wanaofanya kazi tangu asubuhi mpaka liamba na kuambulia kitu kidogo kisichoweza hata kukidhi mahitaji yao ya msingi. Pamoja na kufanya kazi kwa bidii kubwa wanaishia kuokota kitu kidogo kisichoweza kuimarisha maisha yao. Na wala haikubaliki kuwa maskini alidhike na mfumo huo duni na kandamizi wenye fikra za kibepari.

Ndugu Msomaji/msikiliza, tukubali kuwa, wakristo pia, wameshindwa kupambana na mitazamo ya wanazuoni au ile ya wanasiasa na mbinu za kiuchumi inyojumuisha na kuishia kwenye hitimisho potofu. Wengine huupuuza na kughairi kazi za hisani kana kwamba hawako kwenye utume wa Kanisa na hitaji la Injili. Maskini hawezi kutelekezwa kama tutalinda uhai wa Kanisa ambao una chanzo chake kutoka Injili na huzaa matunda yake kila wakati na kila mahali.

Ndugu Msomaji/msikilizaji, tukitazame kipengere cha kuchaguliwa kwa maskini kuwa na upendeleo wa kipekee mbele za Mungu. Mungu ni mwenye huruma na mpango wake wa huruma ambao hujifunua na kukamilishwa katika historia ni kwa vizazi na vizazi juu ya kutuokoa kutoka utumwa wa mauti. Kwa pendo hilo huwatazama viumbe wake kuwatunza katika umaskini wao. Ili kushirikishana hali hii ya udhaifu wa mwanadamu, Yeye mwenyewe alijifanya maskini na kuzaliwa ki mwili kama sisi.

Tunamtambua katika utoto wake akiwa amelazwa kwenye pango la kulishia wanyama na katika unyonge uliokithiri wa msalaba, ambapo alishiriki umaskini wetu ambao ni kifo. Hapa inakuwa rahisi kuelewa tunapoongea kitalimungu juu ya upendeleo na nafasi ya Mungu kwa maskini, kielelezo ambacho katika bara la Marekani na hasa katika mkutano wa Puebla ambao mafundisho yake yamepokelewa na Kanisa. 

Ndugu Msomaji/msikilizaji, neno “upendeleo” lilivyotumika katika mktadha huu halimanishi ubaguzi wa makundi mengine ambayo siyo tabia ya Mungu, bali linamaanisha hamasa juu ya matendo ya Mungu yenye huruma katika umaskini na hali duni.  Tukinuia kufungua zama za utawala wa haki, udugu na mshikamano, Mungu ana nafasi ya pekee moyoni mwake kwa wale wanoteswa na kubaguliwa na anatutaka sisi tulio Kanisa lake, kufanya maamuzi madhubuti yenye kuwaelekea wanyonge.  Ni katika mktadha huu tunaweza kuelewa sehemu kubwa ya Agano la kale ambapo Mungu alijifunua kama rafiki na kimbilio la maskini, Yule anayesikiliza kilio cha maskini na kuwaokoa (Zab 34:7). Mungu aliye ngao ya maskini anatangaza kwa njia ya nabii wake Amos ina Isaya, maovu waliyotendewa maskini, na kuliasa taifa la Israeli kuwa na wongofu wa ndani katika ibada zake.

Ndugu msikilizaji, tumefikia hapa kwa leo katika mwanzo na mwendelezo wa barua ya kitume, usikose kutufuatilia katika vipindi vijavyo. 

Dilexi Te III

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here

 

 

19 Novemba 2025, 14:24