Katika Dilexi Te:Tusisahau wanaoteseka zaidi ni wanawake kutengwa&kutendewa ukatili
Padre Angelo Shikombe -Vatican.
Mpendwa Msomaji/Msikilizaji wa Radio Vatican, tunakuletea mwendelezo wa makala ya Wosia wa Kitume wa “Dilexi Te” yaani “Nimekupenda” wa Papa Leo XIV, uliotiwa saini mnamo tarehe 4 Oktoba 2025, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Francis wa Assisi. Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa waraka huu unaoitwa “DILEXI TE” yaani “nimekupenda” akinukuu kutoka kitabu cha ufunuo 3:9 sehemu inayosema: “…tazama, nitawafanya waje na kusujudu mbele ya miguu yako, nao watatambua ya kuwa nakupenda”. Leo tunaendelea na Sura ya Kwanza baada ya kuona utangulizi, inayojikita kuelezea msingi wa pendo la Mungu kwa maskini.
Ndugu Msomaji/msikilizaji, tukitazame kwa pamoja kilio cha maskini. Katika maandiko matakatifu ambamo Mungu anajifunua mwenyewe kwa Musa katika kichaka kinachowaka, yaweza kuwa sehemu ya kunyanyuka na kuanza upya kwa jitihada zetu. Hapo Mungu anasema: “Nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri; nimesikia kilio chao dhidi ya watawala wao. Hakika, Najua kuwa wanateseka na nimeshuka kuja kuwaokoa. Kwa hiyo, njoo, nikutume wewe” (Kut 3: 7-8: 10). Mungu anaonesha kujali kwake katika mahitaji ya maskini. Wayahudi walipomlilia Mungu aliwatumia waamuzi (Waamuzi 3:15). Ili kusikia kilio cha maskini tunapaswa kuingia ndani moyo wa Mungu anayejali daima mahitaji ya watoto wake, hasa walio katika mahangaiko makubwa. Kama tunaendelea kutokuwajibika kwa kilio hicho, maskini ataendelea kumlilia Mungu dhidi yetu nasi tutahesabiwa kuwa wakosaji (Kumb 15: 9) na kujitenga na moyo wa Mungu.
Hali ya maskini ni kilio ambacho katika historia ya mwanadamu kila mara kinabadili maisha yetu, jamii zetu, siasa na mifumo ya kiuchumi, na hata Kanisa. Katika uso wa maskini tunayaona mahangaiko ya mwenye haki, ambayo ni mahangaiko ya Kristo. Wakati huo huo tunaweza kuongelea hali sura mbalimbali za maskini na umaskini kwa kuwa ni jambo lenye sura nyingi. Hakika, ziko tabia mbalimbali za umaskini; kuna umaskini wa wale wanaokosa mahitaji yao ya msingi, kuna wale waliotengwa na jamii na hawana njia za kuutetea utu na uwezo wao, kuna umaskini wa kimaadili na umaskini wa kiroho, kuna umaskini wa kiutamaduni, umaskini wa wale wanaojikuta katika kifungo cha kufuata masharti ya watu au kifungo cha udhaifu jamii yao, kuna umaskini wa wale wasio na haki, wasio na nafasi, na wasio na uhuru.
NduguMsomaji/msikilizaji, katika mkitadha huu, ni hakika kuwa jitihada ya maskini wenyewe na udhibiti wa mifumo kandamizi ya kijamii inayosababisa umaskini zimeibuka kuwa vipengere muhimu katika nyakati zetu ambavyo bado havitoshelezi. Hii ni kwa sababu jamii zetu mara nyingi hupendelea vigezo vya ustawi wa maisha vinavyofungamana na siasa zenye itikadi za ukosefu wa usawa. Matokeo yake mifumo ya zamani ya umaskini inayojulikana ambayo tunaishambulia inaungana na mifumo mipya ambayo kwa wakati mwingine ni hatari na mibaya zaidi. Kwa mtazamo huu, tunakubaliana na malengo na harakati za umoja wa Mataifa (UN) zenye malengo ya kutokomeza umaskini katika karne yetu.
Mfano halisi wa kumsaidia maskini lazima uambatane na badiliko la kimtazamo ambalo linaathiri ukuaji wa utamaduni. Upotofu wa furaha inayotokana na starehe za maisha unawasukuma watu wengi kuangukia katika maisha ya ubinafsi na kujirimbikizia mali huku wakinia kufanikiwa kwa njia yeyote ile, hata kwa gharama ya wengine na wakitumia nafasi za udhaifu wa mifumo ya kijamii na mikakati ya kisiasa na kiuchumi inayowalinda wenye nguvu. Hivyo, katika ulimwengu ambamo idadi ya maskini inaongezeka, tunaona ukuaji wa kikundi cha wasomi wakiishi katika viunga vya maisha ya faraja na anasa, katika ulimwengu mwingine unaotofautiana na ulimwengu wa watu wa kawaida. Hii inaakisi kuwa tamaduni zinaendelea na wakati mwingine kutushawishi tuwatupilie mbali wengine bila hata kujua na kujali kuwa mamilioni ya watu wanakufa kwa njaa, ama anaishi katika mazingira magumu yasiyostahili mtu kuishi.
Miaka michache baadaye, picha inayoonesha maiti ya mtoto iliyokutwa kando ya fukwe kuonekana kama hadithi ya kutunga. Tusilegee linapokuja jambo la umaskini, tunapaswa kujihusisha juu ya mazingira hatarishi yanayowakumba watu wengi ambao wanakosa chakula na maji. Pia kwa nchi tajiri, idadi ya maskini inayoongzeka si jambo la kufumbia macho. Barani Ulaya, familia nyingi zinashindwa kujimudu kwa mwezi, hakika tunashuhudia aina nyingine ya umaskini, si wa mtu mmoja mmoja bali ni umaskini wa mfumo wa kiuchumi unaoifukarisha jamii, na kuongeza mpasuko katika mkitadha wa hali ya juu. Tusisahau kuwa wanaoteseka zaidi ni wanawake wanaopitia hali za kutengwa, kutendewa kwa ukatili, kwa sababu tu ya kukosa utetezi wa haki zao.
Hata hivyo, tunaendelea kushuhudia mifano mizuri na ya kishuja kati yao ya kutetea na kulinda familia zao changa. Huku mabadiliko yakipamba moto katika baadhi ya nchi, shirika linaloshughulika na haki za kijamii ulimwenguni bado halijapambanua kuwa wanawake wana haki sawa na heshima sawa ya utambulisho kama walivyo wanaume. Tunaongea kitu kwa maneno, na tunaamua na kutekeleza vinginevyo katika uhalisia hasa tunapojihusisha na mazingira ya kimaskini.