Jubilei ya Miaka 30 ya Uhusiano wa Kidiplomasia na 50 ya Uhuru wa Msumbiji
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kuanzia tarehe 5 Desemba hadi tarehe 10 Desemba 2025 anafanya hija ya kitume nchini Msumbiji kama sehemu ya maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 30 tangu Vatican ilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Msumbiji tarehe 14 Desemba 1994, miaka 30 iliyopita sanjari na Jubilei ya Miaka 50 tangu Msumbiji ijipatie uhuru wake wa bendera. Tayari Kardinali amekwisha kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Serikali ya Msumbiji, wakiongozwa na Rais Margarida Adamugy Talapa. Dominika tarehe 7 Desemba 2025 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji sanjari na kufunga Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kitaifa. Kardinali Parolin, ametembelea Kituo cha Huduma Kwa Maskini, “Casa Mateus25. Tarehe 8 Desemba 2025, Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ammetembelea Jimbo Katoliki la Pemba na hatimaye, kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali na wa kidini na hatimaye, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu.
Sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha. Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, tarehe 9 Desemba 2025 amekutana na watu wasiokuwa na makazi maalum nchini Msumbiji na baadaye, amefanya majadiliano ya kiekumene na kidini na viongozi mbalimbali nchini Msumbiji. Kardinali Parolin katika hotuba yake kama sehemu ya kumbukumbu ya Maadhimisho ya Miaka 30 ya Uhusiano wa Kidiplomasia Kati ya Vatican na Msumbiji na Jubilei ya Miaka 50 tangu Msumbiji ijipatie uhuru wake, amekazia kuhusu umoja na ushirikiano kati ya Vatican na Msumbiji kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Msumbiji, hali inayodhihirishwa na uwepo wa Balozi mkazi kutoka Msumbiji mjini Vatican. Haya ni mahusiano yanayosimikwa katika utu, heshima, uhuru wao wa kidini, utetezi pamoja na haki zao msingi sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Katika diplomasia Kanisa daima linamtazama Kristo Yesu, ambaye mbele ya Pilato alijitangaza kuwa Mfalme, lakini wa Ufalme ambao si wa ulimwengu huu. Rej. Yn 18:36-37. Na kisha, alipoulizwa kuhusu sababu ya Ufalme wake kati ya wanadamu, Yesu alieleza akisema: “Kwa ajili ya hili nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie ile Kweli.” Yn 18:37.
Kardinali Parolin anasema, Kanisa Katoliki, kama jumuiya ya kiulimwengu inayowaleta pamoja waamini kutoka mabara yote, watu, lugha na tamaduni zote, lina wito mzito wa kujenga na kudumisha umoja na ushirika. Kanisa linaungana na kukusanya; haigawanyi wala kupinga. Linatafuta njia za uelewano na ushirikiano wa amani, likijitahidi, pamoja na njia zinazoweza kupatikana, kuepusha migogoro, migawanyiko, vita na uharibifu katika familia kubwa ya binadamu. Miaka 30 ya ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Msumbiji na Vatican ni ushuhuda kwamba Msumbiji inatambua na kuthamini: mwelekeo wa kidini na kimaadili wa matatizo ya binadamu, ambamo Kanisa linapania pamoja na mambo mengine kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika: ukweli, upendo na imani; Uadilifu na utu wema. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1988 alitembelea Msumbiji kama alivyofanya Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika Hija yake kitume nchini Msumbiji kuanzia tarehe 4-6 Septemba 2019 ikiongozwa na kauli mbiu “Matumaini, amani na upatanisho." Papa Francisko alipenda kuonesha uwepo wake wa karibu, upendo na mshikamano na familia ya Mungu nchini Msumbiji. Alikazia umuhimu wa kujenga amani na upatanisho wa kidugu; mchakato wa maendeleo sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na kwamba, viongozi wa wakuu wa Serikali ya Msumbiji kwa nyakati tofauti wametembelea Vatican. Papa Leo XIV anakazia pamoja na mambo mengine umuhimu wa kutafuta, kulinda na kudumisha Injili ya Amani na kwamba, Msumbiji ina kiu kubwa ya amani.
Kardinali Parolin amekumbushia kwamba, mwaka mmoja uliopita, kufuatia uchaguzi mkuu, Msumbiji ilitumbukia katika mzozo mkubwa ulioandamana na ghasia na vifo. Katika nyakati hizo ngumu na zenye msukosuko, Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji, lilitoa wito kwa kila mtu kutokubali kushindwa na kishawishi cha vurugu na vita, na hivyo, kuwaalika Wakatoliki na wananchi wote wa Msumbiji wenye mapenzi mema kujitolea kila siku kusali kwa ajili ya amani. Baada ya miezi hiyo, Msumbiji ilifunguka kwa matumaini na dhamira ya sasa ya kisiasa ya "Mazungumzo Jumuishi ya Kitaifa," yenye lengo la kufikia makubaliano ya mapitio ya Katiba na marekebisho ya vipengele mbalimbali vya mfumo wa serikali, ambayo inapaswa kukuza uwazi wa kitaasisi na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Hii ni fursa nzuri ambayo haiwezi kupotezwa. Historia inawakumbusha kwamba: ufunguo wa utulivu wa kisiasa na kijamii ni kujua jinsi ya kutarajia na kujibu mahitaji ya jamii kupitia utekelezaji wa mageuzi ya taratibu ambayo yanaboresha maisha ya watu. Hivi ndivyo msemo wa zamani unavyofundisha: "Ili kuepuka mapinduzi, mageuzi ni muhimu."
Ili yote haya yaweze kutokea ni muhimu kusikiliza na kujibu kwa umakini sauti za wananchi wote wa Msumbiji, hasa sauti za vijana, wanawake, na maskini zaidi na wasio na uwezo. Kanisa Takatifu daima linaunga mkono mazungumzo kama njia muhimu ya kufikia upatanisho, umoja na amani. Kwa nia ya mazungumzo jumuishi, Maaskofu wa Msumbiji wamechapisha kitabu kilichoelekezwa kwa jumuiya za Kikristo na watu wote wenye mapenzi mema: ili kuwatayarisha kushiriki kikamilifu, kwa uangalifu, na kuwajibika katika mchakato huu. Kama Maaskofu wanavyoonyesha, lengo ni kukuza ujenzi wa jamii yenye uadilifu zaidi, uaminifu, shirikishi na utu. Inafaa kutaja kwa namna ya pekee kabisa Jimbo la Cabo Delgado, mwathirika wa ukosefu wa usalama, ghasia pamoja na vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kugumisha mahusiano, watu kukimbia makazi yao pamoja na vifo vya maelfu ya watu, changamoto na wito kama uliotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV wa kurejesha usalama na amani katika eneo hilo. Jimbo la Capo Delgado ni eneo ambalo limeharibiwa sana na chuki za kidini kati ya Waislam na Wakristo. Ukristo na Uislamu ni dini ambazo zimeishi Msumbiji kwa amani, maelewano na kuheshimiana. Misimamo mikali ya kidini na ugaidi si sehemu ya nafsi ya waamini wa dini za Msumbiji; wao ni aina za dini potovu na ngeni kwa utambulisho wa ndani kabisa wa watu wa Msumbiji, ambao ni watu wenye amani, furaha, na wakarimu. Katika hali hii ngumu, Kanisa Katoliki limekuwa mstari wa mbele kuwahudumia wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, wanaokaribiwa na hatari.
Kardinali Parolin amesema, Kanisa Katoliki halitafuti upendeleo, bali linatamani kuweza kutekeleza utume wake wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili kwa kujikita katika ushirikiano na Serikali ya Msumbiji. Ili kuthamini utekelezaji wa mikataba mbalimbali ya Kimataifa tarehe 7 Desemba 2011, Serikali ya Msumbiji na Baraza la Kitaifa ilitia saini “Makubaliano ya Kanuni na Masharti ya Kisheria” ambayo yanapaswa kudhibiti uhusiano wao na “kukuza ushirikiano wenye afya kati ya Msumbiji na Kanisa Katoliki, kwa kuheshimu uhuru wa kila upande katika nyanja yake.” Katika kipindi chote cha miaka kumi na minne ya uhalali, Mkataba huu umethibitisha manufaa na thamani yake. Sasa, wote wanataka kusonga mbele zaidi katika utekelezaji kamili wa Mkataba huo, kwa lengo la kuwezesha huduma ambayo majimbo, taasisi za kidini na wamisionari kwa ukarimu na kwa upendo wa Kikristo hutoa kwa watu wa Msumbiji, hasa maskini zaidi, watoto, wazee, wagonjwa na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amehitimisha hotuba yake kwa kuwasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Leo XIV katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Msumbiji ijipatie uhuru wake wa bendera. Hii ni fursa nzuri ya kuendeleza zaidi ushirikiano chanya na wenye matunda kati ya Kanisa Katoliki na Serikali, kwa ajili ya: Ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Msumbiji na kwamba, anapenda kutoa baraka zake za kitume. Anawaombea amani na kwamba, Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2025 iwe ni chemchemi ya: Amani na imani, matumaini na mapendo; Umoja na mshikamano wa pamoja unaosimikwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na kukuza utamaduni wa amani.